Hongera Nimri, tiba tezi dume iwe nafuu

24Jan 2020
Mhariri
Nipashe
Hongera Nimri, tiba tezi dume iwe nafuu

TANGU zama za kale binadamu wamekuwa wakitumia dawa za asili ikiwamo mizizi, majani na magome. Dawa zinazotokana na mimea na wanyama zimekuwa zikitumiwa  maliasili nyingine kutoka  baharini, ardhi na kwenye miamba  kutibu na kupambana maradhi.

Matumizi ya dawa za mimea na wanyama wa asili ni jambo jema na la kiafya linalokubalika zaidi kwani halina athari kwa watumiaji. Hata hivyo, suala la kupata dozi halisi na viwango vinavyohitajika kutibu maradhi au kuyakinga ni jambo ambalo lilikuwa halijawa na mafanikio makubwa katika sekta ya dawa hasa  kwenye jamii nyingi za Kiafrika ambazo kukosekana kipimo halisi cha dozi, kunazilazimisha kukimbilia dawa za kisasa au tiba za Kizungu.

Matumizi ya miti ya asili kutibu magonjwa kama tezi dume kunahitaji utaalamu na mkono wa serikali ili kufanikisha utafiti na majaribio ya dawa hizo, hivyo  taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Tiba za Binadamu (Nimri) kuwa inaanza kutumia tiba hizo za asili ni jambo ambalo bila shaka limewagusa na kuwafurahisha Watanzania wengi.

Taarifa ya NIMRI iliyotolewa kwenye mkutano na wanahabari Dar es Salaam wiki hii, inaeleza kuwa  taasisi hiyo imepata dawa kutoka kwenye mimea nchini na imejiridhisha kuwa zina uwezo wa kutibu ugonjwa huo na kupunguza nguvu ya saratani ya tezi dume ambayo imekuwa ni janga linaloathiri wanaume wengi.

Tunaipongeza taasisi hiyo kwa kutuaminisha  kuwa wataalamu wa dawa za asilia wana uwezo wa kutafuta, kuzijaribu na kuzitambua dawa zinazoweza kutibu tezi dume. Tunawapongeza na wagunduzi wengine wazawa ambao wamefanikisha utambuzi  na kuisaidia Nimri kufikia hatua hiyo kubwa kwenye sekta ya dawa.

Tiba zilizotangazwa na taasisi hiyo zinatumia dawa za asilia, ambazo zina umuhimu wa kipekee kwenye historia ya binadamu na  ni mwanzo wa kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia kuwa miongoni mwa mataifa makubwa kama China ambayo yamekubuhu kwenye utafiti na matumizi ya dawa hizo.

 Nchi nyingine ni India yenye tiba ya asili iitwayo ‘Ayurveda’ wakati Korea ina ‘ Kampo’ ambazo ni tiba asilia zinazotumiwa kutibu maradhi mbalimbali na dawa zake zimesambaa sehemu mbalimbali duniani.

Tunashauri kuwa mwanzo huo wa kugundua tiba asilia za kupambana na tezi dume, ufungue mlango wa kuzitafiti na kuandaa vidonge dawa nyingine za asilia kama zile za kutibu malaria, vidonda vya tumbo na kisukari zinazoelezwa kuwa zinatumiwa mikoani  na maeneo mengine mengi nchini.

Hata hivyo, serikali ifanye juu chini kuisaidia Nimri ili kuhakikisha kuwa dawa za asilia zinazozalishwa zinakuwa na gharama ndogo na zinawafikia Watanzania wote kwa bei nafuu hasa kwa wale walioko vijijini.

Upatikanaji wa dawa hiyo uendane na unafuu si kwa tiba pekee bali pia vipimo ambavyo vimekuwa ni changamoto kubwa kwa wagonjwa wa saratani zote ikiwamo hiyo ya tezi dume.Kama ikiwezekana serikali ianzishe mfuko maalumu wa tiba kwa kuwa ugunduzi wa tiba ya kansa ya tezi dume ni pambazuko jipya katika kutiba kansa nyingine zikiwamo ya kizazi, tumbo, ngozi na matezi.

Ni wazi kuwa Nimri imefungua macho na kuona mbali kuhusu tiba hizo za asili, hivyo jitihada hizo ziende pamoja na kuandaa misitu ya kuotosha miti yenye dawa za kutibu saratani, lakini pia na kuandaa benki za jeni (Genebanks) za mimea hiyo ili zihifadhiwe na kuendelezwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Habari Kubwa