Pata somo la umasikini, tabia zake na namna ya kuukabili

24Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Pata somo la umasikini, tabia zake na namna ya kuukabili
  • Huu hapa ushuhuda wa vigezo nane.

UMASIKINI ni nini? Huo ni ukosefu wa mahitaji ya msingi ya binadamu kama vile chakula, maji salama, huduma za afya, mavazi na nyumba kutokana na kukosa uwezo wa kuvinunua. Pia, inajulikana kama umasikini uliokithiri au fukara.

Shughuli za uwajibikaji, kuufuta umaskini na kuutafuta mafanikio ya kiuchumi. Inaacha maswali katika kufikia safari ya mafanikio kiuchumi. PICHA ZOTE: MTANDAO.

Ni kadri kuwa na rasilimali chache zaidi au mapato madogo zaidi kulingana na watu wengine katika jamii au nchi au hali ya wastani duniani. Hali hiyo pia inajulikana kama umaskini halisi au unyonge.

Hali hiyo ni hali ya kuwa na rasilimali chache au kipato cha chini kuliko wengine kwenye jamii au nchi, au ikilinganishwa na wastani duniani kote.

Umaskini unajumlisha, pia matokeo yake upande wa siasa na jamii.

Kupunguza ufukara ni kati ya malengo makuu ya taasisi nyingi za kimataifa, kama vile Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia, inayokadiria watu milioni 702.1 waliishi kifukara mwaka 2015 na ilopofika mwaka 1990, walikuwa bilioni 1.75, kati yao milioni 347.1 walikuwa Afrika Kusini kwa Sahara.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (Unicef), inakadiria nusu ya watoto duniani wanaishi kifukara.

ASILI YAKE

Asili ya umaskini inatajwa ni kiwango cha chini cha utajiri na uzalishaji, pia mfumuko wa bei wa bidhaa duniani; vikwazo kwa uzalishaji; kukosekana nia ya serikali na wenye mamlaka kuwajali wa chini.

Kuwapo afya duni na ukosefu wa elimu nafuu kunaathiri uzalishaji chakula cha kutosha na kinachoipatia umma mlo sahihi na unaotakiwa.

Katika mataifa yanayoendelea, inakadiriwa asilimia 40 ya watoto wenye umri wa miaka minne kwenda chini wana ugonjwa wa anaemia utokanao na kukosa madini ya chuma.

Vilevile ulevi wa pombe na dawa ya kulevya, unaweza kuwaweka watu katika umaskini unaoendelea, ikongezwa na maradhi ya kuambukizwa kama vile malaria na kifua kikuu, yote yanasababisha umaskini kwa umma.

Hiyo ni kwa sababu ya kutumika rasilimali za kifedha, ambazo zingetumika katika uwekezaji na uzalishaji. Lingine ni vita, migogoro ya kisiasa na uhalifu, inayojumuisha vikundi haramu vinavyozua vurugu na vikundi vya walanguzi wa dawa ya kulevya pia vinaweka vikwazo kwa uwekezaji.

Kuna ripoti, vita vya wenyewe na migogoro Afrika vimeligharimu dola bilioni 300 kati ya mwaka 1990 na 2005 na kiwango cha umaskini kinaongezeka.

Vipengele vya utamaduni, kama vile ubaguzi wa aina mbalimbali, nao unatajwa kuathiri uzalishaji.

Upungufu wa mahitaji ya msingi Kupanda kwa gharama ya maisha, kunawafanya umaskini kuzidi, bajeti za watu maskini kutumika kununua chakula zaidi, ikilinganishwa na wenye nacho.

HAIBA YA MASKINI

Kuna tabia kadhaa zinazoelezwa na watafiti kumtawala masikini. Moja, anajenga tabia ya muda mwingi anajikita kuangalia televisheni, sinema na tamthiliya, badala ya kufanya shughuli za kuingiza kipato au hata shughuli za ziada zenye manufaa fulani.

Pili, ni ununuzi wa chakula zilizoandaliwa kama chipsi pizza na ‘baga’: Hiyo ni tabia nyingine inayotajwa kumsukuma mtu katika umaskini, ikiwa dalili mbaya inayohitaji marekebisho ya haraka.

Hivyo vyakula vyenye mafuta mengi na kusababisha magonjwa kama uzito uliopitiliza na moyo. Yote yanampunguzia mtu ufanisi wa kazi, hata kuwa na madhara katika uchumi, akili, kijamii na hata uhusiano binafsi na ina matumizi makubwa ya pesa yanayoepukika.

Tatu, kuchelewa kuamka: Ni tabia inayojitokeza kwa kijana, ni ishara ya kuukaribisha umasikini katika siku za usoni. Vijana wanakuwa wazembe kufanya kazi kwa bidii na kwa vile hawatumii umri wao vizuri, wanakuwa hawajawekeza kwa baadaye.

Inaelezwa hata matajiri duniani kama Bill Gates, Elon Musk, Mark Zuckerberg wana tabia ya kuamka mapema kuanza kufanya kazi zao kwa bidii kila siku

Nne, kulaumu wengine kwa unayopitia: Wataalamu wa uchumi wanaeleza moja ya tabia zinazomfanya mtu awe maskini, ni kulaumu wengine kwa kutofanikiwa kwako na kusahau usemi “Maisha ni jinsi unavyoamua kuyaona.’

Tano, kutoweka akiba ambayo kimsingi ni jambo la msingi sana katika mapato yoyote yanayopatikana, kusaidia pindi likitokea matatizo ya baadaye, kama dharura ya ugonjwa.

Sita, inahusu ununuzi wenye mpangilio: Wataalamu wanashauri kufanya ununuzi ukiwa tayari umeandika orodha ya vitu unavyotaka na siyo kukurupuka bila ya mpangilio. Pia, kama unachukua mkopo, itafakariwe kwa ajili ya nini wenye manufaa gani.

Saba, inagusa uzazi wa mpango: Mtu anatakiwa kuhakikisha hali yako ya uchumi iko imara kabla haujaanza kuzaa watoto hao na inaelezea kitaalamu, watoto wakiwa wengi kwenye familia kuliko uwezo binafsi, umasikini unakuwa jirani kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia kwa wakati.

Saba, inaangukia suala la upimaji afya kila mara: Inawezekana kwa wengi linaonekana sio la msingi kupima afya kila mara, lakini ni la msingi kwa kuwezesha kuishi ukiwa na uhakika wa afya yako, ikiwa ni njia nyeupe kuelekea mafanikio.

Ni kama ilivyo mfano kwa ugonjwa wa saratani unavyohimizwa kwamba, suala la kujua mapema hali ilivyo kiafya, ndio uhakika wa kutibiwa na kupona mapema

Nane, inahusu matumizi ya pesa kabla ya kupata: Tabia ya kukopa pesa kabla hazijapatikana kwa matarajio ya kuzilipa pindi zitakapopatikana, ni dalili ya ama umaskini kunyemelea au kuukaribisha mwenyewe.

Wataalamu wanashauri kufanya kazi kwanza na kupata pesa kisha uendelee na kufanya matumizi unayonuia.

Tisa, kunahitajika kuwa na marafiki wasio na malengo makubwa: Marafiki wanakusaidia kufikia malengo yako uliyojiwekea, pia wana nafasi ya kufanya usifikie malengo. Hivyo, inashauriwa kutumia muda zaidi na marafiki wenye malengo makubwa kimaisha, wanawaza mambo chanya na sio mambo hasi muda wote.

Hilo linasaidia kutunza muda, kutokata tamaa kwenye malengo yako au kuwa mbunifu zaidi, hata kukukosoa kwa tabia zinazorudisha nyumba maendeleo yako.

Kwa mujibu za taarifa mawasilisho ya kitafiti na uchumi.

Habari Kubwa