Ilivyokaa tafsiri benki, chimbuko lake na safari yake ilikofika nchini

24Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ilivyokaa tafsiri benki, chimbuko lake na safari yake ilikofika nchini

MTU anaweza kuhoji benki ni nini? Inaangukia katika tafsiri ni taasisi ya kifedha iliyopewa jukumu kuu la kuweka amana za fedha za watu na kutoa mikopo kwa wateja wake na inalipa riba kwa amana.

Jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Pia, benki ina jukumu la kutoa ushauri wa kifedha na miradi, pale kunakohitajika.

Majukumu mengine ni huduma za usimamizi wa mali, ubadilishaji fedha kama za kigeni na kuna aina kuu za benki; biashara, kijamii kama ushirika vijijini na uwekezaji

Hata hivyo, kwa hatua zilizopigwa hivi sasa, kuna benki za mtandaoni na za imani za kidini, zikizingatia taratibu za jamii wateja wake kupata huduma za kibenki.

Majukumu makuu ya benki za biashara ni kutoa mikopo ya muda mfupi, kutoa na kuweka amana za wateja mbalimbali wenye akaunti.

Benki za rasilimali zenyewe zinaenda mbali zaidi ya mkopo na uwekaji amana, kusaidia maandiko mbalimbali ya kibiashara, katika kufanikisha matumizi ya mkopo wanayoitaka.

Lakini, benki zinawajibika na kusimamia kiwango cha fedha za kimataifa sokoni, kudhibiti mfumuko wa bei na kiwango cha pesa kilichopo katika mzunguko.

Hata hivyo, aina ya benki kitaifa unategemea sera na malengo ya nchi na hali ya soko la sekta hiyo katika wakati husika, mathalan Tanzania katika zama za Sera ya Ujamaa na Kujitegemea.

Hadi sasa benki kuu zilizoko katika orodha ya kuwa na mtaji mkubwa duniani ni za nchi za Marekani, Uingereza, Japan, Uswisi, na China.

Katika hatua za awali za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yenye umri zaidi ua miaka 50 sasa, majukumu yake makuu yanayomuisha benki zingine nchini, utoaji wa sarafu na noti, kushauri serikali kuhusu masuala la fedha na mkopeshaji.

DEREVA WA UCHUMI

Benki ni moja wa madereva muhimu wa uchumi kitaifa, kupitia utoaji ukwasi unaohitajika kwa familia na biashara kuwekeza na sasa kuna benki zinazotoa huduma za mtandaoni, akiba na mikopo zinategemea rehani zilizopo.

Benki za biashara, kimsingi zinazingatia biashara, pia zinatoa huduma zaidi na wateja binafsi na kujenga uhusiano nao. Hata hivyo, ni utendaji unaosimamiwa na benki kuu inayosimamia mengi, ikiwamo mitaji yao na sera za uendeshaji wake.

NCHINI TANZANIA

Historia ya milki za benki nchini inaanzia mwaka 1965 ya kupitishwa kisheria na kutekelezwa mwaka 1966. Hapo ndipo kukashuhudiwa kuundwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Ni katika kipindi nchini ikatawaliwa katika mfumo wa uchumi wa kijamaa.

Sura nyingine ni zao la kutanuka benki kupitia utekelezaji wa Azimio la Arusha mwaka 1967 na kuzaliwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ambayo ikawa na matawi mengi nchi nzima.

Ni benki ambayo ilipewa jukumu kubwa la kusukuma mageuzi katika utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Uchumi wa Miaka Mitano (1964-1969) katika kutafuta upatikanaji huduma za msingi.

Ilikuwa wakati kunaundwa viwanda vipya vya kuzalisha mahitaji ya kila siku kwa lengo la ‘kutumia tunavyozalisha’ na si ‘kutumia tusivyozalisha.’ Ni zama iliyojengwa viwanda vingi sana nchini.

Ilipofika awamu ya pili ya utekekelezaji Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ( 1969 - 1974), ilikuwa ni mwendelezo wa mpango uliopita, ulioshuhudia maboresho zaidi, ikiwamo katika sekta ya viwanda.

Ni awamu iliyoanzishwa benki maalum za kuboresha mahitaji ya mkakati ya kisekta ya serikali. Itakumbukwa, Benki ya Nyumba Tanzania (THB), yenyewe ilibuniwa kuboreskha mkakati wa kiserikali ulioanza tangu baada ya uhuru.

Mfano mmojawapo ni mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba, kupitia kuwakopesha wananchi mwaka 1966, na wanapitia taratibu, mfano hai jijini Dar es Salaam, katika maeneo kama Kinondoni, Mwananyamala, Magomeni, Temeke na llala.

 

Ni zama kulikoanziswa shirika la Msajili wa Majumba, ambalo ni zao la Azimio la Arusha, sambamba na kuwapo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Wananchi walijengewa nyumba mbalimbali kwa mikopo nafuu serikalini na hivyo katika mipango ya maendeleo ya baadaye ikawa ni zaidi ya miaka 10 ya uhuru, THB ikatanua wigo wa jukumu hilo kwa kuendeleza sekta ya ujenzi, ikiwa kwa mwezeshaji muhimu.

Aidha, sekta ya kilimo na mifugo, ikaundiwa Benki ya Ushirika na Mendeleo Vijijini (CRDB), ambayo ilifanywa mwezeshaji maalum katika eneo hilo muhimu la kiuchumi na mwajiri mkuu wa kitaifa, kukibatizwa “uti wa mgongo wa taifa,”

Katika hatua nyingine, mipango mikubwa ya serikali kama vile ya kuinua viwanda vikubwa kitaifa, ukiwamo uliopangwa kuwa Mpango wa Maendeleo wa Viwanda na uendelezaji wa huduma za Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) kwa tija zaidi ziliundwa muwezeshaji ambaye ni Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB).

BAADA MAGEUZI

Mageuzi ya kiuchumi duniani ya mwaka 1985, yana historia kubwa katika mageuzi ya sekta ya kifedha nchini, zikiwamo benki.

Hapo kukawapo hata mapitio ya majukumu ya BoT katika kusimamia benki kitaifa. Hadi kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1990 kulishuhudiwa sheria mpya za fedha na kibenki kitaifa.

Ni wakati kulikoanza kushuhudiwa soko huria la fedha za kigeni, jambo ambalo awali lililokuwa jukumu maalum la BoT, tena ziliuzwa kwa kibali malaum.

Ndani ya muda mfupi maduka ya fedha za kigeni ambayo yametoweka katika siku za karibuni, yalitapakaa katika sehemu nyingi za nchini, sambamba na uuzwaji huo katika benki, hapo ikajenga maana ya benki mbalimbali kuanzisha vitengo vya kusimamia uzaji fedha za kigeni.

Wakati huo, pia serikali ilikuwa inafanya mageuzi makubwa kupitia iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma(PSRC), kwa kubinafissha taasisi za umma.

Sekta ya Benki haikubaki salama, kwani iliyokuwa benki ya THB ilifikia hatua kutoweka sokoni, kutokana hali yake kiuchumi kulega mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Hata baadhi ya mitaji ya kigeni haikuwa salama, kwani kuna benki ya Greenland mwishoni mwa miaka ya 1990, ililazimika kufungwa ndani ya saa 24 na BoT, ambayo ina mamlaka kwa mujibu wa sheria.

NBC ambayo ilikuwa benki kubwa zaidi nchini, ilivunjwa kuzalisha taasisi tatu, ikiwamo NBC (1997) Limited na National Microfinance Bank (NMB), ambayo ilibaki na sehemu ya asilimia ya miliki ya serikali.

Aidha, CRDB ilibinafishwa na hisa zake kuingia katika mikono ya miliki binafsi na katika mbinu ya kibiashara kutopoteza nembo ya soko la asili, NBC na CRDB hazikubadili sana majina yao kwa kiasi kikubwa.

NBC na CRDB katika majina yao mapya, yaliondokana na ufafanuzi wa kirefu cha majina yao ya awali.

Pia, ni mageuzi yaliyofika mbali kwa mageuzi ya baadhi ya majukumu maalum kuachwa na zote kuwa katika mwonekano zaidi kujikitia katika maisha mapya sura ya benki ya biashara.

Vivyo hivyo, mchakato wa kubinafsishwa benki hizo, uliendana na kuweka kando baadhi ya majukumu ambayo si ya asili kibenki kama vile kumiliki majengo.

TIB ndio haikuguswa na mageuzi hayo, ila baada ya kulega kwa muda mrefu, serikali ilipatia mtaji mkubwa katika njia ya kuchangia kuinua mitaji, rasilimali na uwekezaji kitaifa.

Ni mageuzi ambayo Benki ya Posta, iliyoanzia kitengo katika Shirika la Posta Tanzania (TPB), nayo ilipata uhai kamili kama shirika la umma, katika hadhi ya kibenki inayoendelea kukua.

Baada ya miaka nenda rudi, Benki ya Maendeleo ya Kilimo nayo imeundwa nchini, ambayo pengo lake liliachwa na CRDB iliyokuwapo kabla ya ubinafsishaji.

Mageuzi ya hivi karibuni ya kijinsia, yalisukuma kuundwa Benki ya Wanawake, ambayo katika tathmini kiataifa, ilihamishiwa kuwa sehemu ya benki nyingine, aina ya msukosko uliyoikuta benki ya Twiga.

Baada ya mageuzi ya kibenki nchini, ndipo kumeshuhudiwa utitiri wa taasisi hizo zikianzishwa kila mahali, kutoka mitaji ya nchini na ya kigeni ikiwamo, za jumuiya ya kijamii.

Kimsingi, BoT ambayo zaidi ya miaka 5o ilikuwa na majukumu makuu sita, hivi sasa yameongezeka maradufu kulingana na mahitaji na mageuzi yanayoendelea nchini na duniani.

Mojawapo ya majuku yake ni hatua yake ya karibuni iliyochukua kufungia maduka ya fedha za kigeni kutokana na ilichokiona kuwapo ukiukaji wa maslahi ya umma.

JUKUMU LA BOT

Kwa mujibu wa tovuti yake, jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania, ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.

Kazi Zingine: Kutoa sarafu ya nchi ambayo ni Shilingi ya Tanzania.

Kusimamia mabenki na taasisi za fedha

Kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini

Kuhifadhi akiba ya nchi ikiwamo fedha za kigeni

Kutoa ushauri juu ya masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Benki ya Serikali, na

Benki ya Mabenki.

Habari Kubwa