Mazao ya mkakati, pacha na Tanzania ya Viwanda

24Jan 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Mazao ya mkakati, pacha na Tanzania ya Viwanda

KILIMO ni uti wa mgongo wa taifa na ndiko kwenye ajira nyingi, kutokana na ukweli kwamba ndio shughuli za Watanzania wengi, yakiwamo ya chakula na biashara.

Mbali na kuwa uti wa mgongo wa taifa, kilimo kimepewa kaulimbiu mbalimbali. Hapo tunataja 'kilimo cha kufa na kupona' na 'siasa ni kilimo' hata 'kilimo kwanza' na nyinginezo.

Hizo zote zinaonyesha jinsi gani kilimo kilivyo na umuhimu na sasa serikali imeamua kuyawekea mkakati baadhi ya mazao ya biashara, ili kuhakikisha wakulima wanafaidi jasho lao na yenyewe inapata kodi.

Korosho, pamba, tumbaku, chai na kahawa ni mazao matano ya biashara, ambayo serikali imeyawekea mkazo maalum kuyaendeleza kwa kasi, lengo ni kuongeza pato la wakulima.

Mbali na hilo, serikali imeamua kufanya yawe chanzo cha kuaminika cha malighafi, katika uchumi wa viwanda na inaendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni.

Hatua hiyo inaongeza usimamizi katika uzalishaji wa mazao hayo makuu ya biashara na inatokana na ukweli kwamba, ni kipindi kirefu uzalishaji wake ulishuka kutokana na changamoto kadhaa zilizopo.

Katika orodha hiyo ya vikwazo, inatajwa ni baadhi ya wakulima kuacha kulima kwa kukatishwa tamaa kwa sababu mbalimbali.

Mojawapo ni vyama vya ushirika kutotekeleza vyema wajibu wao, wizi, dhuluma na ushiriki mdogo wa maofisa kilimo kusimamia kilimo hicho kitaalamu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika moja ya hotuba zake, anasema serikali itaendelea kuimarisha vyama vya msingi vya ushirika wa mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao hayo ya kimkakati.

Ninaamini, uamuzi huo wa serikali utakuwa na mafanikio hasa kwa kuboresha kilimo, hatimaye kufikia Tanzania ya Viwanda, kwani vina uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya kilimo, sekta iliyoajiri Watanzania wengi.

Lakini hali hairidhishi, watu hao wanatumia zana duni, ambazo ni vyema wakaachana nazo na kutumia teknolojia ya kisasa, ili kuzalishaji malighafi zenye tija kwa ajili ya viwanda mahitaji ya kawaida.

Wakati serikali ikiwa inaendeleza juhudi za kuboresha mazao hayo ya kimkakati, ni vyema navyo vyama vya ushirika kutimiza wajibu inavyotakiwa na pia vitendo vya wizi na dhuluma viachwe.

Maofisa kilimo nao wanapaswa kutimiza wajibu wao inavyotakiwa, kwani baadhi yao wanadaiwa kwamba hawataki kuishi vijijini na wakulima wanakosa huduma zao.

Viongozi wa vyama vya ushirika na maofisa kilimo, mnaopotosha mnahatarisha juhudi za serikali kuimarisha mazao hayo matano. Ni vyema wakachukuliwa hatua mapema.

Jambo la msingi, ni kila upande kutimiza wajibu inavyotakiwa, kwa kutambua nchi inaelekea kuwa ya viwanda, hivyo ni muhimu kuimarisha kilimo kiwe na tija, vinginevyo kitakwama.

Ushiriki wa makundi hayo bila ujanja ujanja, utachangia kuwapo kwa hamasa kubwa kwenye kilimo na hatimaye uzalishaji kuongezeka ingawa kwa kutumia zana duni zilizopo, lakini kutakuwa na manufaa.

Inaumiza kuona, mkulima anajitahidi kuzalisha, lakini mwisho wa siku wananufaika na watu wengine wanashindwa kupata mazao ya kutosha, kwa kukosa ushauri wa wataalamu wa kilimo, wasioenda shamba.

Ikumbukwe, kilimo ni sekta mwajiri wa Watanzania wengi na chakula kikuu cha biashara, hivyo ni muhimu, kujiimarisha kufikia ndoto ya kuelekea maendeleo mwaka 2025 , nchi kufikia uchumi wa kati.

Serikali inatoa kipaumbele katika sekta ya kilimo, hivyo hatua ni kuungwa mkono na wadau wote wa kilimo, ili kiendelee kuwa uti wa mgongo wa taifa, badala ya kuyumba.

Kilimo imara kinategemea wadau kwenye sekta ya kilimo, hivyo asiwepo wa kujitenga kwenye jambo hilo.

Nirudie kwa kusisitiza kuwa malighafi nyingi zinazohitajika katika viwanda, zinatokana na mazao ya kilimo, hivyo suala la uzalishaji wa mazao shambani lina uhusiano wa karibu na viwanda.

Habari Kubwa