Mwaka mmoja wa Rais Felix Tshesekedi madarakani

25Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mwaka mmoja wa Rais Felix Tshesekedi madarakani

RAIS Felix Tshisekedi, ametimiza mwaka mmoja tangu kukalia nafasi hiyo ya juu katika taifa la Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Rais Felix Tshesekedi akisimikwa kushika wadhifa huo na mtangulizi wake Josephn Kabila mwaka jana

Kuingia kwake madarakani kumezua malalamiko kutoka kambi ya upinzani, lakini wengi walipongeza wakisema ni hatua ya kihistoria kupatikana kwa nguvu ya kura.

Viongozi wote waliomtangulia walikalia kiti hicho baada ya kumwaga damu kwa kufanya mapinduzi.

Kama mgombea mkuu wa chama cha upinzani cha UDPS, Tshisekedi alimshinda Martin Fayulu, mgombea aliyekuwa akipigiwa upatu na mtangulizi wake, Joseph Kabila, katika uchaguzi huo wa mwezi Disemba 2018.

Alipokalia kiti hicho, alikabiliwa na changamoto nyingi ukiwamo kukithiri kwa ufisadi, miundo mbinu mibovu, vita Mashariki mwa nchi hiyo na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Mzozo wa mashariki

Wakati alipotawazwa kuwa rais, aliahidi kujenga Congo yenye udhabiti kwa lengo la kuvutia maendeleo kupitia amani na usalama.

Tshisekedi amejaribu kuimarisha usalama kwa kutoa muda waasi kujisalimisha na wale waliokaidi waliamrisha jeshi kufanya operesheni kuwaondoa msutuni.

Pamoja na juhudi hizo, wananchi wana hofu kutokana na kusuasua kwa operesheni hiyo pamoja na idadi kubwa ya raia wanaouawa na waasi.

Jeshi limefanikiwa kulirudisha nyuma kundi la wapiganaji wa ADF, kundi la waasi ambalo linatoka Uganda lakini sasa limepiga kambi katika jimbo la Beni nchini humo.

"Wakati wa kampeni zangu za uchaguzi , nilipata fursa ya kutembelea ,maeneo haya na nilikumbwa na tatizo hili ambalo linaniumiza moyo sana'' , Tshisekedi ameambia BBC.

''Nilichukua jukumu wakati huo la kufanya kila kitu ili kuleta amani''.

Rais huyo aliliamuru jeshi kuweka kambi yake mjini Beni ambao umeshamiri mashambulizi ya  ADF. Baadhi ya wanajeshi walibadilishwa, na kuleta nguvu mpya katika vita dhidi ya wanamgambo hao.

Katika vita vyake dhidi ya kundi jingine, viongozi wawili muhimu wa waasi wa Kihutu nchini Rwanda (FDLR) waliuawa.

Makundi mengine madogo ya wanamgambo bado yanaendeleza kuwa tishio katika jimbo hilo huku wengine wakihusishwa na biashara haramu ya madini.

Mashambulizi dhidi ya raia yanaendelea huku makundi ya waasi ambayo hujihami na mapanga yakitekeleza mashambulizi wakati wowote.

Mlipuko wa Ebola

Wakati alipochukua madaraka , Tshesekedi  alikabiliwa na tatizo la kuenea kwa virusi vya ebola , mashariki mwa taifa hilo.

Umekuwa mlipuko mbaya wa Ebola duniani , ambao shirika la afya duniani WHO liliutangaza kama janga la kiafya linalohitaji dharura.

Kulingana na Shirika hilo, watu 3,416 waliathiriwa na ugonjwa huo, 2,237 walikufa na wengine 1,136 walinusurika.

Kutoaminiana kati ya wenyeji na maofisa wa afya , kunakosababishwa na mila, ukosefu wa habari, pamoja na mashambulizi dhidi ya maofisa wanaokabiliana na ugonjwa huo kulizorotesha kazi ya kupambana na Ebola.

Serikali ya Tshisekedi  ikiwa imepata usaidizi kutoka kwa mashirika ya kigeni na inaonekana kwamba kiwango cha maambukizi kimepungua, lakini WHO inasema ni vigumu kuthibitisha hilo kwa kuwa kuna maeneo kadhaa hayajafikiwa.

Surua yaleta uatata mpya

Rais Tshisekedi pia amelazimika kukabiliana na ugonjwa wa Surua. Virusi hivyo vimesambaa kwa kasi na kuambukiza zaidi ya watu 300,000 tangu kulipuka kwa ugonjwa huo mwaka 2019.

Taarifa inasema ugonjwa huo umeenea katika mikoa 26 ya taifa hilo.

Takriban watu 6,000 wamefariki, idadi ambayo inazidi ya wale wa Ebola, kulingana na WHO na kufanya ndio mlipuko mbaya zaidi kuwahi kutokea kote duniani.

Serikali ya Tshisekedi, WHO na mashirika mengine ya kimataifa imewapatia chanjo zaidi ya watoto milioni 18 walio chini ya umri wa miaka mitano nchini humo.

Lakini ukosefu wa fedha za kununua chanjo za kutosha na barabara mbaya umezuia uwezo wa wahudumu wa afya kumfikia kila mtu.

Kukabiliana na njaa

Kutokana na mapato ya mtu wa kawaida, DR Congo ni mojawapo ya mataifa yalio na umasikini mkubwa zaidi duniani licha ya kuwa na utajiri wa madini.

Raia wengi wa Congo huishi chini ya dola mbili kwa siku. kulingana na takwimu ya benki kuu ya dunia, lakini taifa hilo lina hatua kubwa za kupiga.

Rais anasema kwamba anataka kukabiliana na umasikini na katika juhudi hizo ameongeza matumizi ya serikali.

Katika kipindi cha miezi 12, bajeti ya serikali iliongezeka kutoka dola biloni sita, hadi kufikia 11.

Ulipaji kodi katika maeneo mengine , ikiwamo katika majengo, umeongezeka ili kulipia matumizi. Lakini watu wengi wa wanasubiri kuona iwapo hali yao ya kiuchumi itaimarika.

Wasiwasi wa kisiasa

Licha ya kushinda urais, Tshisekedi amelazimika kukabiliana na nguvu ya mtangulizi wake Joseph Kabila, ambaye anamiliki idadi kubwa ya wabunge bungeni.

Majadiliano kati ya vyama hivyo viwili yalichukua takriban miezi saba, kabla ya makubaliano kuafikiwa kwa lengo la kuunda serikali.

Uhusiano kati ya vyama hivyo ulisababisha wasiwasi mkubwa katika kipindi cha mwaka mmoja huku wanasiasa wa pande zote mbili wakilumbana mara kwa mara na wakati mwingine kupigana.

Lakini inaonekana kuna juhudi za kuhakikisha kwamba mambo yanafanyika.

Wafungwa wa kisiasa wameachiliwa huru, huku wapinzani wa  kisiasa waliokuwa wakiishi nje ya nchi hiyo wamesamehewa na kurudi nyumbani.

Habari Kubwa