Aliye juu yu juu

25Jan 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Aliye juu yu juu

HALAHALA Yanga, mgwizi haliwi na funo. ‘Mgwizi’ ni mnyama anayewagwia au kuwakamata wanyama wengine. ‘Funo’ ni mnyama anayefanana na paa.

Aliye juu huwa yuko juu ni kama ilivyo, kwa mnyama anayewala wengine kama simba; hawezi kuliwa na funo. Methali hii hutumiwa hasa pale mtu ameshindwa kupambana na mwingine kwa kuwa ana uwezo kumzidi.

Mpaka nilipokuwa naandika makala haya jana Ijumaa, Klabu ya Simba ndio ilikuwa ikiziongoza timu zingine 19 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kuwa na alama 41 baada ya kucheza michezo 16 ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu inayoendelea sasa.

Katika michezo hiyo imeshinda mechi 13, imekwenda sare michezo miwili na kuwa timu pekee iliyopoteza mchezo mmoja tu. Aidha, ni timu inayoongoza kwa kufunga mabao 35 na kufungwa idadi ndogo zaidi, yaani mabao saba.

Hata ukitoa mabao saba iliyofungwa kati ya iliyofunga, bado itakuwa ikiziongoza timu zote 19 kwa kufunga mabao 28. Simba inastahiki kupewa kongole (asante).

Napata wazo la kutumia methali isemayo “Angurumapo simba mcheza ni nani?” Maana yake ni mnyama gani anayeweza kucheza anaponguruma simba aliye mfalme wa nyika?

Methali hii huweza kutumiwa kuwapigia mfano watu wanaomdharau kiongozi au mkubwa, lakini wanaojikunyata mara atokeapo. Naam, angurumapo simba mcheza ni nani?

Simba ninayoizungumzia si simba mnyama, bali ni timu ya Simba inayonufaika kwa uwekezaji wa bilionea wao, MO Dewji anayoitoa kizani na kuifanya ya kimataifa. Anayebisha na abishe, lakini ukweli ndio huo.

Kwa hatua waliyofikia Simba, maarufu kwa jina la ‘Wana wa Msimbazi,’ nawapa kongole ila wasivimbe vichwa kwani ligi ndo kwanza imeanza hivyo lolote laweza kutokea kwani mpira unadunda na kudundika.

Yanga, ambayo mimi ni mwanachama kindakindaki (halisi), naipa moyo kwa methali isemayo: “Anayetafuta hachoki, akichoka keshapata.” Maana yake mtu anayetafuta kitu (kwa muktadha huu ubingwa), hachoki kutafuta hadi akipatapo.

Methali hii hutumiwa kumhimiza mtu anayefanya jambo fulani na anayeelekea kukata tamaa kumshauri asikate tamaa.

Wachezaji wa Yanga wanapaswa kutambua kuwa huu ni mzunguko wa kwanza na kuna mwingine wa pili unaoitwa ‘lala salama’ kwa hiyo hawana sababu ya kukata tamaa kwani penye nia pana njia.

Ilisemwa na wahenga kuwa “Aliye juu mngoje chini.” Maana yake aliye juu kama mpanda ngazi hakosi atateremka chini.

Mpaka Alhamisi iliyopita, Yanga ilikuwa nafasi ya nne ikitanguliwa na Simba na Azam FC na 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union ya jijini Tanga. Kwa msimamo huo, Yanga (timu ya wananchi) inazitangulia timu 16 ikiwa imecheza michezo 15.

Timu zilizofungwa mabao mengi mpaka Alhamisi iliyopita ni Mbeya City (mabao 24), Singida United 23, Alliance FC (22), Lipuli FC (20), KMC FC (19), Mbao FC na Ruvu Shooting (18).

Kagera Sugar, JKT Tanzania na Ndanda FC zimefungwa mabao 17 kila moja zikifuatiwa na Yanga, Namungo FC, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar na Mwadui FC zilizofungwa mabao 15 kila moja.

Ndanda FC ipo mkiani ikizibeba timu 19 kwa kufunga mabao sita na kufungwa 18 ikiwa na alama tisa.

Wanaozusha kuwa vipigo viwili mfululizo dhidi ya ‘timu ya wananchi’ (Yanga) kuwa kuna ‘mkono wa mtu’ wakimnyooshea kidole Charles Boniface eti anahusika na vipigo hivyo, ni wajinga na wambea wanaotaka kuleta vurugu klabuni.

Hakuna timu yoyote ya kandanda duniani isiyofungika wala hakuna inayoweza kuzitawala zingine zote daima. Kadhalika, hakuna timu inayocheza ili ishindwe; kama ipo humu nchini, ipigwe faini kubwa na kuondoshwa kwenye Ligi Kuu sawia (kwa wakati mmoja).

Jambo linalokera ni timu zetu kuruhusiwa kusajili wachezaji wengi kutoka nje ya Tanzania. Jambo hilo linasababisha wachezaji wetu kutopata nafasi ya kuonesha uwezo wao ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa, ama hawatofautiani na wachezaji wetu au wanapitwa kiuchezaji.

Inaleta picha gani kama timu ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inachezesha wachezaji saba wa kigeni ilhali wanne tu ndio wazalendo? Maana yake ni kwamba Tanzania hakuna wachezaji wanaofaa! Si kweli wala haiwezekani.

“Chako ni chako, cha mwenzako si chako.” Maana yake kitu unachokiita chako ni kizuri na huweza kukufaa na una uhuru nacho kuliko cha mtu mwingine. Twafunzwa kuvitegemea vitu vyetu (kwa muktadha huu wachezaji wazalendo) wala si wageni wanaokuja kuchumia kwetu na kwenda kula kwao!

“Cha wenyewe huliwa na wenyewe.” Maana yake kitu cha wengine huwafaidi wao wenyewe. Hutumiwa kuwahimiza watu wajitegemee.

Hofu yangu ni kwamba kuna wakati tutaomba watu wa nje waje kuiongoza TFF! Tutaondokana lini na fedheha (jambo la aibu; nazaa; izara) hii?

Kadhia (tukio la kuhuzunisha) hii yanifanya nikumbuke enzi za kina Hamisi Mtoto, Yungi Mwanansali, William Nasson, Kilomoni, Aziz, Mbwana Abushiri, Kembo, Hemed Sefu, John Limo.

Pia Salehe Zimbwe na Omari Zimbwe, Sharif Salum, Rashid Sefu, Abdallah Luo, Mweri Simba, Huseni Chuma, Amana, Sembwana, She Mdanzi, Lozi Omari, Wingi Mzenga na wengine kadhaa niliowasahau.

Namshukuru mwalimu wangu wa Kiswahili, Mohamed Sharif wa Tanga aliyenikumbusha majina ya wachezaji, baadhi yao wakiwa wametutangulia mbele ya haki. Mungu awarehemu Inshallah (apendapo Mwenyezi Mungu)!

Habari Kubwa