Polisi wadhibiti wimbi la ujambazi wa bodaboda

31Dec 2015
Editor
Nipashe
Polisi wadhibiti wimbi la ujambazi wa bodaboda

Katika siku za karibuni, kumekuwa na ripoti nyingi za kuibuka upya kwa ujambazi kwa kasi na hasa ule wa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda.

boda boda

Inataka kufanana na mwaka 2005 wakati Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alipoingia madarakani kuliibuka wimbi la ujambazi na hali hiyo imejirudia tena mwaka huu baada ya Rais Dk. John Magufuli, kushika wadhifa huu.

Majambazi inaaminika wanatumia pikipiki na hasa zile zenye mwendo kasi kutokana na kutokamatwa kirahisi na polisi.

Mfano juzi limetokea tukio la kusikitisha la kuuawa kwa mfanyakazi wa kampuni ya simu za mikononi, Gabriel Raphael, jijini Dar es Salaam akitokea benki kuchukua fedha.

Matukio kama haya yamekuwa yakitokea sehemu mbalimbali nchini huku matokeo yakiongezeka bila ya kudhibitiwa.

Imefika wakati kwa vyombo vya dola kuchukua hatua za haraka kudhibiti tatizo hili ili kuwanusuru wananchi na hali hii.

Katika siku za karibuni, imekuwa inatia woga kwa wananchi kwenda benki kutokana na kuhofia usalama wao.

Vyombo vya dola vinapaswa kuingia kwa undani na kuchunguza tatizo hili kujua wahusika wakuu wa uhalifu huu.

Maana inakuwaje mtu anapotoka kufanya shughuli zake benki na hasa wale wanaochukua fedha, kujikuta wakivamiwa na kuporwa fedha zao?

Kuna dalili kuwa kuna mtandao mkubwa wa uhalifu unaohusisha watu wa kawaida hata baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao si waaminifu.

Imefika wakati kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuja na mkakati mkubwa wa kukabiliana na tatizo la ujambazi na hasa huu wa kwenye benki.

Mathalan, kwa kuwa benki zinajihusisha na masuala ya fedha, zingefunga kamera za kulinda usalama wa umbali wa hata mita 100 ili kuangalia wale walio karibu na maeneo hayo nyakati za kazi.

Pia kwa kuwa pikipiki ndiyo zinatumika zaidi kwa mambo hayo pia zinapaswa kupigwa marufuku kwenye maeneo ya mabenki.

Usajili wa pikipiki unapaswa kuangaliwa upya ili kudhibiti zisitumiwe kwa mambo ya uhalifu.

Utaratibu wa sasa wa uandikishaji wa pikipiki kwa kiasi kikubwa unatoa mwanya kwa watu wasio waaminifu kuzitumia kufanya uhalifu.

Bahati mbaya katika miaka ya karibuni, suala la waendesha bodaboda limekuwa likitumiwa na wanasiasa ili kujijenga.

Kwa mfano, wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, tulisikia lugha kuwa waendesha bodaboda wasibughudhiwe.

Hali hiyo ilianzia kwa wagombea urais, ubunge hadi madiwani, ambao wote walikuwa wanasisitiza kuwa waendesha bodaboda wasiguswe.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya watu wasio waaminifu wanatumia mwanya huo kufanya uhalifu kwa kutumia pikipiki.

Tanzania inasifika kwa kuwa na askari wazuri na mahiri kwa masuala ya ulinzi na usalama.

Ndiyo hata polisi na wanajeshi wetu wamekuwa wakitumiwa na Umoja wa Mataifa kulinda amani sehemu mbalimbali duniani.

Tunaomba vyombo vya dola vije na mkakati maalum wa kuhakikisha vinadhibiti ujambazi huu unaotishia maisha ya wananchi.

Ujambazi huu hauishii tu kwenye mabenki, bali hata kwenye maduka na yale yanayoshughulika na utumaji wa fedha kupitia simu za mkononi.

Ukiangalia idadi kubwa ya wizi huu unapofanyika unahusisha zaidi pikipiki aina ya bodaboda.

Suala la udhibiti halipaswi kuchukuliwa kisiasa tu, bali mkakati wa kiusalama unapaswa kuandaliwa ili kudhibiti hali hiyo.

Habari Kubwa