Ronaldo azika uadui na Messi

20Jan 2016
Nipashe
Ronaldo azika uadui na Messi
  • *** Mreno huyo amesema alimsaidia hasimu wake huyo wa muda mrefu kutatua changamoto ya lugha na sasa anasubiri malipo.

NYOTA wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, amesema kuwa sasa anafurahia uhusiano mzuri alionao na Lionel Messi, huku akidokeza kuwa bado anasubiri malipo ya huduma ya ukarimani aliyoitoa kwa nyota huyo wa Barca wakati wa utoaji wa tuzo ya Ballon d'Or hivi karibuni.

Lionel Messi na Christiano Ronaldo

Wawili hao wamekuwa mahasimu kwa muda mrefu kutokana na kuzidiana kete katika tuzo mbalimbali za soka, wakitinga fainali ya kusaka mataji nane yaliyopita ya Ballon d'Or.
Lakini, akizungumzia ushindi wa wa mabao 5-1 wa Madrid dhidi ya Sporting Gijon juzi, Mreno huyo alisisitiza kuwa sasa anakaribisha sapoti kwa nyota huyo wa Barcelona.
"Tumekuwa karibu, tumekuwa tukifurahia uhusiano mzuri, lakini labda katika miaka michache iliyopita hatukuwa karibu sana," alisema.
Messi na Ronaldo walikuwa kwenye steji moja pamoja na Neymar wakati wa tuzo ya Ballon d'Or mjini Zurich, na nyota huyo wa zamani wa Manchester United aliweka wazi kuwa sasa hana uhasama tena na nyota hao wawili wa Barcelona.
"Wakati tukiwa juu ya steji, si Messi wala Neymar aliyejua kuongea Kiingereza, na nilikuwa mkarimani wao," alicheka.
"Niliongea nao baadaye na kuwakumbusha kwamba walitakiwa kunilipa baada ya kumalizika kwa hafla ya tuzo kwa vile nilikuwa mkarimani wao!" (Intereconomia).

Habari Kubwa