Ardhi ikitwaliwa fidia hizi hutumiwa

22Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ardhi ikitwaliwa fidia hizi hutumiwa

NI kawaida serikali kutwaa maeneo. Huhamisha wahusika au wamiliki na kuchukua ardhi au majengo yao kwa malengo maalum yaliyokusudiwa.

Yaweza kutwaliwa nyumba yako, kiwanja au hata shamba. Mara kadhaa serikali hufanya hivi panapohitajika kwa ajili ya shughuli za umma kama ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, huduma za umeme, maji shule, vyuo, vituo vya afya na miradi mingineyo kwa manufaa ya umma.

Fidia ya Ardhi

Fidia ya ardhi ni stahili ambayo mwenye ardhi au mmiliki anatakiwa kupata pale ambapo ardhi yake inatwaliwa au inachukuliwa na serikali kwa matumizi maalum ya serikali au umma.

Wakati mwingine watu hujiuliza Je, inawezekana kugomea serikali kutwaa ardhi? Ukweli ni kwamba, serikali inapotaka kumhamisha mwananchi na kuchukua ardhi yake kupisha mradi wa umma kisheria mwananchi hana uwezo wa kukataa.

Hii ni kwasababu ardhi yote ni mali ya umma ambayo mdhamini wake mkuu ni serikali kupitia mamlaka ya Rais.

Hivyo tunaweza kusema kuwa ardhi ni mali ya umma inayodhaminiwa na serikali au Raisi wa Tanzania.

Kwa hiyo mwananchi hawezi kuikatalia serikali kuchukua mali hiyo isipokuwa kisheria ni kuwa anayehamishwa analipwa fidia. Hata ukiamua kwenda mahakamani kupinga kutwaliwa ardhi hautapinga kuwa serikali isichukue ardhi yako isipokuwa utapinga kiwango ama kile usichoridhika nacho kwenye fidia.

Inawezekana ukakalalamika kuwa fidia ni ndogo au utaratibu mbovu uliotumika kukadiria fidia, riba na mipaka. Labda utazungumzia pengine kuwapo na uonevu au hila katika kutwaliwa ardhi yako au namna nyingineyo ya nia ovu ndipo unaweza kupinga ardhi yako kutwaliwa.

Lakini haitawezekana kupinga hatua hiyo ikiwa kuna malengo maalum ya kutwaa ardhi kwa ajili ya shughuli za umma. Aina za Fidia Watu wengi wamekuwa wakijua kuwa fidia ni pesa tu japo linapokuja suala la fidia ya ardhi watu hudhani kinachotakiwa kutolewa na serikali ni pesa.

Hili si kweli kwakuwa fidia haimaanishi pesa pekee kama tutakavyoona hapa chini. Fedha Ni aina ya malipo kwa pesa hii ni fidia inayojulikana sana na ambayo imekuwa ikipendwa mno na ndiyo aina ya fidia ambayo hutumiwa na serikali mara kwa mara kuliko fidia nyinginezo.

Maeneo ya watu hukadiriwa na hulipwa fedha taslimu kutokana na bei ya soko ya eneo husika. Imefanyika hivyo sehemu nyingi na inaendelea kufanyika.

Malipo kwa Ardhi:

Hii ni aina ya fidia ambayo huhusisha kupewa ardhi mbadala baada ya ile unayomiliki kutwaliwa.Inachukuliwa kuwa ardhi yako imebadilishiwa umiliki na kuchukuliwa kwa ajili ya shughuli za umma hivyo unapewa ardhi nyingine kufidia iliyochukuliwa.

Muhimu kuwa usipewe ardhi nyingine kama fidia ambayo hadhi yake, ubora wake, matumizi yake, na ukubwa wake uko chini au haulingani na ile ya kwako iliyochukuliwa.

Muhimu Unatakiwa upewe ardhi yenye ubora na ukubwa uleule, matumizi yawe pia yanalingana na ardhi iliyochukuliwa Aidha, hadhi, ubora na ukubwa vinaweza kuzidi lakini visipungue. Ikiwa utapewa ardhi kama fidia na ikawa chini ya ile kiukubwa, ubora na hadhi basi unayo malalamiko ya msingi ambayo utayapeleka kwa Kamishna wa Ardhi au mahakamani ili kupata kiwango cha haki kilichoporwa.

Isitoshe, ni ngumu kusikia mtu yeyote anakwenda mahakamani kulalamika eti amepewa ardhi kubwa zaidi na yenye ubora zaidi kuliko ile ya kwake, iliyochukuliwa hapo awali.

Fidia ya Jengo Unaweza kupata fidia ya malipo kwa jengo, badala yake ni badala ya pesa unaweza kupewa jengo au majengo yanayofanana na lile ambalo limechukuliwa au kubolewa kupisha mradi wa umma.

Kama nilivyoeleza hapa juu kuwa utatakiwa kupewa jengo lenye ubora, hadhi na ukubwa uleule wa mwanzo. Malalamiko utakuwa na haki nayo ikiwa umepewa jengo lililo chini ya ubora na hadhi ya lile lililochukuliwa.

Fidia ya malipo kwa ruhusa ya kutumia mali za umma ni aina ya fidia ambapo baada ya kuchukuliwa ardhi yako,kwa mfano jengo ambalo ulikuwa ukipokea kodi unapewa jengo jingine si kwa kulimiliki bali kulitumia ambapo unaweza kuchukua kodi kama mmiliki kwa muda fulani utakaokubaliwa mpaka hapo kiwango cha pesa ambacho ungelipwa kama fidia kitaisha.

Hii pia hutumika kufidia mashamba ambapo utapangiwa kutumia shamba la umma kwa muda fulani kufidia lile la mtu lililochukuliwa. Fidia ya malipo kwa miche pamoja au mimea, ni namna ya kufidia kunakofanyika kwa mmiliki na njia hii hutolewa panapokuwa na uharibifu wa miche na mimea katika eneo lako.

Yawezekana eneo lililochukuliwa lilikuwa na miche na mimea na imeharibiwa. Si lazima upewe pesa unaweza kupewa miche na mimea yenye hadhi na ubora kama wa ile ya kwako.

Hii hujumuisha fidia ya mazao na nafaka pia. Aina nyingine ya fidia ni kwa njia ya malipo kwa makubaliano maalumu, hapa mdai na Kamishana wa Ardhi hukaa kwenye meza ya mazungumzo na kukubaliana aina ya fidia inayofaa kwa kiwango cha ardhi au jengo lililochukuliwa kupisha mradi.

Hapa fidia inaweza kuwa yoyote kutegemea na makubaliano ya pande hizo mbili. Mwisho, haya yote ni kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 sanjari na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 zote ni za Tanzania.

Habari Kubwa