Hebu Taifa Stars tuikalie kikao

18Oct 2020
Joseph Kulangwa
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Hebu Taifa Stars tuikalie kikao

WATANZANIA kweli tuna bahati ya mtende. Covid-19 AKA Uviko-19 imetukimbia kama ilivyokuja? Kwa kweli Mungu ashukuriwe kwa hilo na tuendelee kuomba mgeni huyo asirudi tena kutusumbua.

Mnakumbuka tulivyotumbuka macho baada ya kusikia umeingia nchini na watu wanaaga dunia? Mnakumbuka tulivyofokewa kwa kutovaa barakoa? Mnakumbuka tulivyofakamia malimao na kutafuna tangawizi kama ngedere?

Mnakumbuka tulivyojifukiza majani ya miti ya aina mbalimbali bila kujali yana upupu au la? Kisa Uviko aishilie mbali? Mnakumbuka viongozi kila kukicha walivyojitokeza kutufundisha hata kunawa? Fikiria hata kunawa tunafundishwa mizee mizima!

Yaani, mpaka tulifundishwa kutorudia kuvaa nguo? Tukafundishwa kufua nguo? Ukiivaa usiirudie! Maisha haya, kumbe tunaweza kunawa, kumbe tunaweza kuvaa nguo safi. Kwa kifupi tukiamua kujikinga tunaweza, kazi ni kukumbushana tu.

Ukiliona sakata la Uviko ndipo utaona kumbe mengine tunafanya makusudi tu tunaweza kuyaepuka. Tunaweza hata kuepuka kwenda jela, basi tu akili zetu tunazijua wenyewe Wabongo. Lakini Uviko ilitufunza adabu.

Tulikaa bila shule, tulikaa hatuendi kuangalia burudani, wenye kiu hatukwenda baa, maanake kila mahali Uviko alitamalaki. Lakini sasa alhamdulilahi. Michezo imeanza tunashuhudia ligi zetu, watu wanafurika viwanjani. Kubwa kampeni zinashuhudia nyomi bila barakoa.

Tuna michezo ya Kombe la Mataifa ya Afrika imeanza, nasi tunashiriki, kama kawaida tunaangalia tutakachokivuna baada ya kukaa bila kucheza kutokana na Uviko. Tumeunda timu yetu ya Taifa, kama kawaida si ya kudumu sana kama za wenzetu, kwani sisi huokoteza mashindano yakikaribia.

Hatupendi kufanya hivyo, la hasha, lakini tatizo hatuna wachezaji wengi wa kulipwa kama wenzetu Ughaibuni, ambao wanaweza kuwa na timu za Taifa tatu hadi nne nje ya mataifa yao.

Kwao ni rahisi kuitana na kukusanyana leo na kesho kutwa kuingia uwanjani kuonesha maajabu. Sisi tutafikria kina Samatta, Msuva, Mao na wengine wawili watatu hivi, waje tuchanganye na walioko hapa ndipo tukashindane.

Hatuna jinsi, lakini kama tutaamua na kujenga wachezaji wetu wa ndani badala ya kuwajazia wa kigeni kwa kisingizo cha eti wapate changamoto, tunajidanganya. Kuna wakati Waziri Harrison (Huyu si Morrison acheni kutoa mimacho), alifungua uwanja wa majidiliano kuhusu wageni 10 kwenye timu zetu, akalemewa na ubishi wa Wabongo, yakabaki hivyo hivyo.

Angalia timu zetu kubwa hizi hasa Yanga, Simba na Azam, zilizokithiri wageni, utaona ni hao tu ndio wanaocheza na kufunga huku wa ndani wakibaki kutazama tu. Kisa ni kwamba tunajali timu za klabu zishinde, bila kuangalia hatima ya Timu ya Taifa.

Hivi kama washambuliaji tulionao wazawa ni Bocco na sijui mwingine nani, na huyo hachezi mara kwa mara kwa sababu tuna Kagere na Mugalu, au kama Waziri Junior hachezi kwa sababu tuna Sarpong na Kisinda, Chilunda hachezi kwa sababu kuna Dube na Tigere, ni lini wataisaidia Taifa Stars?

Wageni huku wanajijenga na wakiitwa kwao, wanakwenda kuzisaidia timu zao za Taifa, ninyi ndo kwanza mnakusanyana, kujipanga kukabiliana na timu hizo hizo zenye wachezaji hao hao walioko nchini na wanapewa nafasi kucheza.

Basi kama tumeshindwa kufanya la kufanya, basi nyie TFF, waombeni wageni wote walioko nchini, waunde timu yao ambayo itakuwa ikitumika kuipima nguvu Taifa Stars kila mara ikihitajika kuliko kutumia gharama kualika timu ya Taifa lingine kuja kujipima au kuwafuata kwao kwa lengo hilo hilo.

Kuna wachezaji wa kigeni wanaochezea timu za Taifa ambao ni wazuri na wanaotosha kuipima nguvu Taifa Stars na ikajijenga vema, na hivyo isisubiri michuano kuanza, yaani tunakuwa na timu ya Taifa ya kudumu hata kama ni ya CHAN. Mbona Samatta na Kiba wanaweza na Samakiba yao? Wao wanaweza wana nini na sisi tushindwe tuna nini? Alamsiki.

Habari Kubwa