Makada wa mtindo huu wamekalia kuti kavu

03Jun 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Makada wa mtindo huu wamekalia kuti kavu

WAKATI huu ambao nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu, viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamekuwa wakitoa tahadhari kwa makada wake, ili kuepuka kutumia njia ya mkato kupata uongozi.

Viongozi wa chama hicho wanasema, wako macho dhidi ya wanachama wao, ambao wanavuruga kabla ya uchaguzi huo kwa lengo la kupata viongozi wanaofaa kukiwakilisha.

Kwamba, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM ilichelewa kuwaengua baadhi ya wanachama waliovuruga na kuigawa kwa maslahi binafsi, lakini uchaguzi wa mwaka huu itawaengua mapema.

Hii ni kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, akisema kwamba CCM ilichelewa kuwaondoa wasiofuata taratibu za chama, na kusababisha wakigawe chama, lakini sasa wamewadhibiti. Anasema, hawawezi kujitokeza tena katika uchaguzi ujao na kwamba walioanza kujipitisha kwenye majimbo na kukusanya watu kufanya vikao au kutoa rushwa, hao tayari ‘vichwa vyao vimeliwa'.

Katika kuhakikisha chama kinapata wawakilishi halali, Polepole anasema, mwaka huu kuna mfumo madhubuti wa kupokea taarifa kwa walioanza kampeni mapema kinyume na utaratibu.

Anasema watakaobainika hawatapitishwa na chama hicho kwenye kura za maoni, hivyo ni wazi kwamba 'wamekalia kuti kavu'. Siyo mara ya kwanza chama kutoa kauli kama hiyo, alianza Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, Katibu Mkuu Dk. Bashiru Alli, akasisitiza.

Hivyo ni wakati wa makada wa CCM kusoma ishara za nyakati na kutambua kuwa chama chao hakitaki makandokando bali taratibu zifuatwe ili kupata wagombea waliopitishwa kihalali katika kura za maoni.

Utafutaji wa dhamana ya chama kihalali unamjengea mtu heshima, hivyo ni muhimu wahusika wakazingatia hilo kama wana nia ya kweli ya kuwatumikia wananchi kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.

Kada wa CCM anaweza kupenya kwa kutumia njia ya mkato bila mifumo ya chama kumbaini, lakini mwishowe ataongoza kiujanjaunja na kushindwa kuleta maendeleo, kwa vile nafasi ameipata kupitia njia hiyo.

Ninaamini kwamba kutafuta uongozi kwa kufuata taratibu zilizowekwa kunaweza pia kuepusha makada kukumbana na changamoto mbalimbali zikiwamo za kunaswa katika mitego iliyowekwa na chama.

Vinginevyo wanaong'ang'ania njia za mkato watajikuta wamekalia kuti kavu na hatimaye kukosa uongozi, kutokana na ukweli kwamba hata Katibu Mkuu alishasema chama kinatafuta viongozi siyo warembo.

Kwa maana hiyo wale ambao wameanza kujipitisha kwa wanachama ni sawa na mrembo kujipitisha mbele ya watu ili wamuone, lakini kwenye suala la kutafuta uongozi ni kufuata utaratibu.

CCM inaamini kwamba hadhi yake kwa wananchi, imesharejea, hivyo haitaki makada wa kukiharibia na kuirudisha nyuma, badala yake wafuate taratibu wanaposaka kuongoza.

Ni wazi kada mwenye uwezo wa kuongoza atachaguliwa bila kutumia mbinu, ambazo zinakwenda kinyume na taratibu na kalenda ya chama hicho tawala.

Hivyo kila mwanachama anayetaka nafasi katika uchaguzi mkuu, apitie katika mchakato halali wa kura za maoni ndani ya chama chake, hatimaye apewe nafasi ya kukiwakilisha chama dhidi ya wagombea wa vyama vingine.

CCM ni miongoni mwa vyama vikongwe barani Afrika na hilo halina ubishi, lakini wanapojitokeza makada wanaotumia mbinu zisizofaa kwa lengo la kupata uongozi, wanakiharibia mbele ya umma.

Mkazo unaowekwa na viongozi wa CCM ni kuwataka wanachama kufuata, ni wazi wamedhamiria kuhakikisha chama kinapata wawakilishi wanaokubalika na wenye uwezo wa kuwatumikia Watanzania.

Kuna msemo wa Kiswahili kwamba; 'kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza', hivyo watu wenye nia ya kuwatumikia wananchi hawezi kuanza kuzunguka katika kata na majimbo kufanya kampeni kabla ya muda.

Badala yake watasubiri kalenda ya chama, ambayo ina taratibu zote zinazotakiwa kuzingatiwa, ili hatimaye wapate wawakilishi wanaokubalika na wote.

Habari Kubwa