Tutafakari ya JPM na si kuhemka chanjo corona

08Feb 2021
Nkwazi Mhango
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Tutafakari ya JPM na si kuhemka chanjo corona

RAIS John Magufuli, alizua mjadala mkubwa duniani hivi karibuni, pale alipionya wizara ya Afya kutokurupuka kuingiza chanjo za Covid-19.

Wapo waliomshangaa hata kumlaumu kuwa anaweza kuleta madhara makubwa kwa taifa kwa msimamo huu. Pia wapo waliomuunga mkono kwa kuzingatia uzoefu wa bara la Afrika katika mahusiano yake na mataifa ya magharibi pia mfumo kandamizi wa kidunia.

Hii ni jambo la kawaida katika jambo lolote. Wapo watakaokubaliana na hata kutofautiana nalo. Binadamu siyo kama wanyama. Wana uwezo wa kutofautiana, kuelimishana hata kupotoshana.

Kila mmoja ana uhuru wa kutumia maarifa na utashi wake kuliangalia hili.

Hata hivyo, Magufuli siyo pekee mwenye kushuku chanjo na haraka ya kufanya hivyo. Hivi karibuni, kulikuwa na video fupi ya Dk. Nerves Mumba, Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Zambia, cha the Movement for Multi-Party Democracy (MMD) akitahadharisha serikali ya nchi yake kukurupuka kuagiza chanjo bila ya kujiridhisha kama zinafaa na kuhitajika.

Kuna haja ya kudurusu mantiki ya hoja ya Magufuli kama alivyonukuliwa akisema kuwa “Chanjo hazifai, kama Wazungu wangekuwa na uwezo wa kuleta chanjo, hata chanjo ya Ukimwi ingekuwa imeshaletwa, chanjo ya kifua kikuu ingekuwa kifua ingeshaondoka, hata chanjo ya malaria ingekuwa ishapatikana hata chanjo ya kansa ingekuwa imeshapatikana, lazima Watanzania tuwe waangalifu kwa mambo ya kuletewa letewa.”  Ukifikiria kwa kina kwa kuangalia maswali aliyouliza na hali alizoziongelea na namna mataifa ya magharibi yalivyoyauzia, kuna mashiko kwenye maswali haya.

Je, kwanini wazungu wamekuwa wepesi kuja na chanjo ya Covid-19 wakati hawakuhamanishwa na majanga aliyotaja Magufuli? Mosi, Covid-19 imewaathiri sana kuliko watu wengine duniani kiasi cha kuhaha.

Mara nyingi, kitu kinachowagusa wazungu, hupewa umuhimu kwa vile chini ya mfumo wa kibaguzi na kikoloni unaendesha dunia,  wazungu ndiyo kila kitu.

Pili, wamefanya haraka kuja na chanjo ili kutengeneza fedha. Kwao, kila kitu ni fursa hasa ya kibiashara.

Tatu, pia fursa hii inaweza kutumika kwa kampuni ya madawa si kuuza tu bali kufanya majaribio ya kuboresha na kutumia baadhi ya madawa yake ambayo hayakuwa na soko.

Nne, kutokana na namna Covid-19 inavyoenea haraka, wazungu wasingependa wateketee, wakijiona kama ilivyokuwa kwa waafrika na UKIMWI na Malaria. Kama Malaria ingekuwa inafika Ulaya, bila shaka kinga ingepatikana. Maana ingekuwa inaua ‘binadamu’ na siyo waswahili.

Baada ya Magufuli kutoa mawazo haya, shirika la Afya duniani lilitoa jibu haraka. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao, mkuu wa WHO kanda ya Afrika Dk. Matshdiso Moeti amesema “Tumeanza kuwasiliana upya na ngazi za juu za uongozi, na tunatoa mchango wetu kama ilivyokua hapo mwanzo, na tunataka kushirikiana na Tanzania, kwa niaba ya watu wa Tanzania, nchi jirani na dunia kwa ujumla. Sehemu ya mawasiliano yetu na Tanzania ni kukumbusha serikali kuwa, hii ni sehemu ya makubaliano ya kanuni za afya za kimataifa ambapo nchi wanachama wamekubali kwa pamoja kuzuia kusambaa kwa magonjwa.” Kimsingi, Dk Moeti, hakujibu swali hata moja. Mbona tunapolalamikia matatizo mengine ya kimfumo, mashirika ya Umoja wa Mataifa hayaonekani? Sababu ni rahisi kuwa umaskini siyo sawa na magonjwa hauambukizi wala kuwasumbua matajiri zaidi ya kuwafanya wawe matajiri zaidi. Hivyo, masuala ya kupambana na umaskini pamoja na ukweli kuwa unaua watu wetu wengi, hayawahangaishi wakubwa wa dunia kama yalivyo magonjwa ya kuambukiza tena ambayo yameonyesha kuwaathiri zaidi ya maskini.

Kwanini kuna mantiki?

Ulaya wamekufa sana kuliko Afrika, ­­pamoja na kuwa na huduma bora za kiafya­­­, kuna idadi kubwa ya wazee kuliko Afrika.

Pia ikumbukwe kuwa Ulaya na Amerika ya Kaskazini, hazina vyakula asilia kama ilivyo kwa Afrika. Ulaji unachangia sana kwenye kupambana na magonjwa. Nakumbuka rafiki yangu Adam Ngamange Mkurugenzi Mkuu wa MKIKITA, aliwahi kusema kuwa badala ya kuhangaika na kujenga mahospitali, tutumia fedha na nguvu hii kuelimisha watu wetu juu ya lishe bora jambo ambalo kwa kiwango kikubwa ndilo limeinusuru Afrika.

Mbali na kuwa na vyakula asili na vyenye lishe ambavyo watu wengi wetu hula wakiamini ni vya kimaskini, pia staili za maisha kati ya Ulaya na Afrika ni tofauti.

Ulaya watu wengi wanakufa kwa kula sana tena vyakula visivyo na lishe, huku Afrika watu wakikonda kwa kutokuwa na chakula cha kutosha.

Maisha ya watu wengi Afrika ni zoezi tosha wakati Ulaya watu wanategemea nyenzo kiasi cha kukosa mazoezi. Kutokuwa na magari na vyombo vingine vya moto kunawalazimisha watu wetu wengi kufanya mazoezi bila kutaka wala kujua jambo ambalo kwa Ulaya linakosekana.

Kwanini WHO imekuwa na haraka kuingilia wakati UKIMWI ukifyeka waafrika wala haikuwa na spidi kama hii?

Tumalizie kwa kushauri wahusika kutafakari sana. Kwani janga lipo lakini kwa viwango tofauti kama ilivyo kwa majanga mengine.

Tusiache kujikinga na kuchukua hatua madhubuti lakini bila kukurupuka wala kuhemka yanapotoka mawazo kinzani au fikra mbadala hata kama ni hasi kwa msimamo wa wengine.

Ila hakuna ubishi kuwa kama tutajiridhisha na usalama wa chanjo, tutachanja sawa na wengine. Tanzania siyo kisiwa.

Habari Kubwa