‘Asante Mzee Mwinyi unavyokuza Kiswahili’

12May 2021
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
‘Asante Mzee Mwinyi unavyokuza Kiswahili’

UANDISHI wa vitabu kwa Kiswahili ni kati ya mikakati inayoweza kutumiwa na Tanzania kukuza lugha hiyo kwa vile ni njia mojawapo inayokiwezesha kusomwa na kizungumzwa na watu wengi zaidi duniani.

Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, ni mmoja wa viongozi ambao wameendelea kukikuza Kiswahili na safari hii ameandika kitabu chake kwa Kiswahili.

Mwinyi anayeweza kuitwa Baba wa Kiswahili ujuzi wake wa kuidumisha lugha hiyo unaonekana kila anapohutubia au kuzungumza na ameendelea kuwavutia wengi kutokana na umahiri wake wa kuongea na kutamka.

Mvuto wa hotuba zake hutokana na namna anavyoyatamka maneno kiufasaha na lafudhi yake ya Kiunguja huvutia zaidi.
Mwishoni mwa wiki kwenye uzinduzi kwa kitabu chake, kiitwacho ‘Mzee Ruhksa: Safari ya Maisha Yangu’, anaelezea masuala mbalimbali kwenye kitabu hicho kilichoandikwa kwa ufasaha kwa Kiswahili.

Uamuzi wa kuandika kitabu hicho kwa Kiswahili unalenga kufikia wasomaji wengi ambao wanaikubali kuwa ndiyo lugha yao ya mawasiliano.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), linakikubali Kiswahili likisema kinazungumzwa na watu milioni 180 duniani.

Mzee Mwinyi akielezea baadhi ya sababu za Kiswahili kutumia kwenye kitabu chake anasema ni pamoja na kukikuza na kuunga mkono juhudi za serikali kukiendeleza.

Anasema Kiswahili amekitumia kwa sababu ya ujuzi alionao kwenye lugha hiyo na kwamba mwaka 1968, aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili na kuongeza: “Ujuzi wangu wa kutumia lugha hii umenifanya nichague Kiswahili kwenye kitabu changu.”

Aidha, uzinduzi huo uliokwenda sambamba na kusherehekea miaka 96 ya kuzaliwa kwake uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na katika kumshukuru anasema:

“Natambua uzito wa majukumu yako, lakini umekuja kunizindulia kitabu. Muda wa Rais kutokana na majukumu huwa ni mchache. Rais hana nafasi ya anasa, wakati wa marais  ni mdogo,” anasema Mzee Mwinyi, akitoa hotuba yake.

“Uliona kitabu hiki kina umuhimu wa kuzinduliwa kwenye awamu yako, kuwa Rais ni hidaya (kitu unachopewa bure). Nimetunukiwa uongozi bila rushwa wala uchawi ni mapenzi ya Mungu. Neema hizi ninazo kwa sababu ya hofu kwa Mwenyezi Mungu.”

Aidha, Prof. Rwekaza Mukandala, akitoa muhtasari wa kitabu hicho, anasema, kati ya yale yaliyomo kwenye kitabu hicho ni historia ya tangu kuzaliwa, elimu, kazi hadi maisha ya kustaafu ya Mzee Rukhsa.

Anasema Mzee Mwinyi ambaye alizaliwa Mei 8, mwaka 1925, Kijiji Kivule, wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, kitabu chake kina maneno yapatayo 100,000 kilicho na maelezo ya ufasaha ya Kiswahili na kwamba lengo ni kufikia wasomaji wengi wa lugha hii.

Anasema Kiswahili kinachotambulika kwa baadhi ya nchi duniani, hususan Afrika, kimewaunganisha Watanzania tangu uhuru, kinatumika kwenye baadhi ya mikutano ya kimataifa barani Afrika ikiwamo mikutano ya Umoja wa Afrika (AU).

Mwaka 1986, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO)lilipitisha azimio la kutumia Kiswahili kwenye vikao vyake vyote pia katika vile vya AU lugha hiyo inatambulika.

Inaelezwa na UNESCO kuwa Kiswahili kinazungumzwa hasa katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kati na mataifa ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Afrika ya Kati, Zambia, Comoro, Malawi, Afrika Kusini na Zimbabwe.

Lugha hii pia imeendelea kusambaa zaidi duniani kupitia vyombo vya habari hususan idhaa za kimataifa ikiwamo Sauti za Amerika (VOA), Ujerumani (DW), redio na televisheni ya BBC na Shirika la Redio na Televisheni la Uturuki (TRT).

Kukua kwa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kunaelezwa kuwa ni fursa nyingine ya kukuza lugha hiyo kupitia majukwaa ya mitandaoni.