‘Kula urefu wa akili yako, usiibe mitihani’

19Jan 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
‘Kula urefu wa akili yako, usiibe mitihani’

BARAZA la Mitihani Taifa (NECTA), limefuta matokeo ya watahiniwa 215 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.

Katibu Mtendaji wa Baraza, Dk. Charles Msonde, aliyesema hayo wakati akitangaza matokeo ya kitaifa ya upimaji wa maarifa kwa darasa la nne, kidato cha pili na cha nne kwa mitihani huo wa mwaka jana.

Udanganyifu wa mtihani umekuwa jambo la kawaida katika shule mbalimbali nchini, ingawa baadhi ya watuhumiwa wamewahi kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hatua nyingine ambazo zinachukuliwa, ni pamoja na kutoa onyo kabla ya kufanyika kwa mitihani, lakini bado udanganyifu umeendelea kujirudia.

Kwa mfano, mwaka jana, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Kagera, ilikaririwa na vyombo vya habari ikitangaza kuwashikilia watu 67 wakiwamo wanafunzi 59.

Wanafunzi hao walikuwa ni wa vyuo viwili vya ufundi stadi (VETA), wakuu wa vyuo hivyo na wakufunzi sita, kwa tuhuma za kufanya udanganyifu katika mitihani na matumizi mabaya ya ofisi.

Kwa mujibu wa TAKUKURU mkoani humo, walimu walishirikiana na wanafunzi na kutengeneza makundi mawili ya mtandao wa ‘whatsapp’ ambayo yalitumika kutuma majibu.

Si hapo tu, mwishoni mwa mwaka jana, NECTA ilitangaza kuwafutia matokeo watahiniwa 1,059 kutoka shule 38 zilizofanya udanganyifu katika mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka huo.

Nani yuko nyuma ya udanganyifu huo? Kwanini sasa limekuwa kama jambo la kawaida, kila unapofanyika mtihani, wajanja wachache wanapenyeza na kufanya udanganyifu na kuvuruga lengo la kutaka kila mwanafunzi afaulu kulingana na uwezo wake darasani?

Udanganyifu kwenye mitihani nchini umekuwapo na jitihada za kuukomesha zinaendelea, hivyo kuna haja ya kutafuta mbinu nyingine zaidi za kukabiliana nao.

Bila kuwa na ubunifu zaidi kukabiliana na udanganyifu huo, kuna hatari ya kuzalisha wasomi mbumbumbu ambao hawatakuwa na faida kwa taifa lao, kwa kuwa watakuwa na sifa ambazo haziendani na uwezo wa kielimu.

Umefika wakati wadau wa elimu kuanzia wazazi na walezi kuachana na kujiingiza kwenye udanganyifu wa mitihani unaosababisha watoto wao wafaulu japo hawakustahili.

Kila mmoja akitimiza wajibu wake inavyotakiwa, hakutakuwa na udanganyifu unaojirudia kwenye mitihani na kusababisha kiwango cha elimu kushuka kwa kupata wasomi wasio na sifa.

Wadau wa elimu wasiweke pamba masikioni, bali wasikilize kile ambacho kimekuwa kikielezwa na NECTA ili watoe mchango katika kukomesha vitendo hivyo, ambavyo vinadhalilisha elimu.

Haipendezi kuona watu wachache wakiendelea kuwaharibia watoto maisha yao ya baadaye kwa kushirikisha katika udanganyifu wa mitihani, ambao mwisho wake kufutiwa matokeo ya mtihani.

Suala la kuimarisha usimamizi wa mitihani ni la muhimu ili usiwepo mwanya wa kuwafanya wadanganyifu kuendelea kuutumia kwa manufaa yao na kusababisha wanafunzi kufututiwa matokeo.

Kasi ya TAKUKURU kunasa watuhumiwa iendelee kuongezeka, ili kuziba mianya ya wahusika na kuacha kila mwanafunzi afaulu mitihani kulingana na uwezo wake wa darasani alionao.

Watoto ndiyo raia na taifa la kesho, hivyo kuwapa wote elimu ni jambo muhimu lisilo na mbadala, lakini unapoingizwa udanganyifu katika mitihani, hiyo ni sawa na kuwaharibia ndoto zao za baadaye.

Inaumiza kuona mwanafunzi amesotwa kwa miaka yote minne akiwa sekondari, halafu badala ya kufanya mtihani inavyotakiwa, anajiingiza kwenye udanganyifu ili apate ufaulu usiolingana na uwezo wake.

Waswahili wana msemo kwamba; 'mbuzi hula kulingana na urefu wa kamba yake', hivyo hata wanafunzi nao hawana budi kushinda au kufaulu mitihani kulingana na uwezo wa akili zao.

Hivyo wale ambao watafanya mitihani yao kuanzia sasa wajifunze kwa wale ambao wamefutiwa matokeo ili nao yasije kuwakuta kwa kukubali kuingia kwenye mtego huo wa udanganyifu.