‘Kuwaadhibu papo kwa papo wasio na leseni ni kuwaonea’

19Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mionzi ya Sheria
‘Kuwaadhibu papo kwa papo wasio na leseni ni kuwaonea’

WIKI hii Waziri wa Mambo wa Ndani, Kangi Lugola, amewaondoa kazini makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Temeke, Ilala na Arusha kwa sababu mbalimbali ikiwamo kupuuza maagizo yake na kumkejeli.

idha, uonevu kwa madereva wa boda boda umetajwa kuwa sababu nyingine, kuchukua rushwa, kusindikiza wahalifu na kujiona miungu watu , badala ya kuwahudumia wananchi.

Hilo ni jema, ila suala jingine ambalo ingefaa Waziri Lugola na Makanda wa Mikoa wakiwamo wa Usalama Barabarani walione ni malalamiko ya kuwatoza watu faini kinyume cha sheria kisa wameshindwa kuonyesha leseni mara moja kwa polisi anapowataka kufanya hivyo.

Nianze kwa kusema pengine wewe ni raia au mmiliki wa chombo cha usafiri na siku moja ukaona malumbano au ukahusika, polisi anataka leseni na dereva anajibu kuwa hajatembea nayo kwa wakati huo na anamtaka aweke gari pembeni.

Swali ni hili, hivi ni kosa kwa dereva, anaposimamishwa na trafiki, kushindwa kutoa leseni ndani ya muda unaotakiwa kutozwa faina papo hapo? Kusimamishwa na trafiki barabarani na ukawa huna leseni mfukoni kwa muda huo si kosa.

Mwambie huyo polisi kuwa kutokutembea na leseni mfukono hilo si kosa. Sheria inaagiza kutembea na leseni unapoendesha vyombo vya moto, lakini pia haisemi kuwa utakapokuwa hauna leseni pale polisi anatakapoihitaji basi ni kosa la jinai na uadhibiwe.

MWONGOZO KISHERIA

Inayozungumziwa hapa ni Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168. Wapo watu wameandikiwa faini kisa wameombwa leseni wakasema hawana, au wakajibu kuwa wamezisahau majumbani. Hawa waliotozwa faini katika mazingira kama haya wameonewa. Na wanastahili kurudishiwa fedha walizotoa haraka.

Ni kweli kifungu cha 77 cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 kinamtaka kila mwendesha chombo cha moto kutembea na leseni barabarani.Aidha , askari anayo mamlaka kumsimamisha mwendesha chombo cha moto na kumtaka aonyeshe leseni yake, lakini si kweli hata kidogo kuwa mwendesha chombo cha moto asipoonyesha leseni kwa wakati huo basi tayari ametenda kosa. Si sahihi wala si kweli.

Kifungu cha 77(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 kinasema kuwa mtu hatatiwa hatiani, kwa maana ya kulipa faini au kuandikiwa kosa au kuadhibiwa na chombo chochote ikiwamo mahakama, kwasababu tu hakubeba, au hakutoa wala kuonyesha leseni pale alipotakiwa kufanya hivyo.

Aidha, kinaongeza kuwa, isipokuwa ana siku tatu za kutoa au kuonyesha leseni hiyo toka siku hiyo aliposimamishwa na mamlaka na kuhojiwa au kutakiwa kuonyesha.

Hivyo basi, tafsiri iko wazi kuwa unaposimamishwa, ukaombwa kuonyesha leseni, ukawa huna kwa muda huo, unazo siku tatu mbele za kutakiwa kuleta na kumwonyesha trafiki au mamlaka nyingine zilizoulizia uhalali wa nyaraka hizo.

Anachotakiwa kufanya askari si kukuandikia kosa, la hasha, bali ni kukutaka umuonyeshe leseni hiyo ndani ya siku tatu tokea dakika au wakati huo alipokuuliza. Ukishindwa kufanya hivyo ndani ya siku hizo hapo ndipo linaweza kuwa kosa.

Watu wasionewe. Wapo askari wengine pia hawajui hizi sheria. Ni wakati wa madereva kuwaelimisha. Hakuna kudhani kuwa askari anakuonea kumbe naye hajui. Kwahiyo kazi unayo wewe kuhakikisha unamweleza huyo askari kuhusu kifungu hiki na namna kinavyotaka. Wewe ndiye mtetezi wa kwanza wa haki yako kabla ya kutetewa na mwingine.

Na kama itatokea ukaandikiwa adhabu kwa lazima kwa kitu kama hiki, basi unayo haki ya kukataa kulipa na kuomba kufikishwa mahakamani ili sheria ikatafsiriwe.

Mwambie “sitalipa nataka sheria ikatafsiriwe mahakamani”. Kukataa kulipa si kosa au ukorofi na hivyo huna haja ya kuhofu.Kukataa kulipa ni haki katika haki ulizonazo ukihisi umeonewa. Na kama umeshalipa au ulilipa huko nyuma katika mazingira ya jambo kama hili na unao ushahidi basi unayo haki ya kudai hela uliyolipa. Unaweza kuidai huko ulikotozwa au mahakamani.

Sheria imetoa ahueni hii ikizingatia mazingira ya ubinadamu. Huwezi kila unapoamka asubuhi ukakumbuka leseni. Huwezi kila unapokuwa na safari ukakumbuka leseni. Safari nyingine ni za ghafla na za kushtua, mfano kuitiwa msiba,ugonjwa,matatizo kazini,bila kusahau msongo/stress za ada na kodi. Atapata wapi muda wa kukumbuka leseni mtu huyu.

Mwingine amebadilisha nguo na hivyo leseni kubaki kwenye nguo iliyovuliwa, mwingine amebadilisha gari na hivyo leseni kubaki kwenye gari jingine.

Na mazingira mengine kama hayo. Zote hizi ni dharura za kibinadamu zilizowafanya watunga sheria kuweka muda wa siku tatu kwa ajili ya kutoa au kuonesha leseni.

Ni wito, watu wabadilike, madereva na askari wasimamia usalama barabarani. Dereva asiwe mkorofi, kadhalika askari asimwonee dereva au abiria wanapozungumzia suala la leseni.