‘Maajabu wagombea kupakaziana rushwa’

22Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
‘Maajabu wagombea kupakaziana rushwa’

VIONGOZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), wiki hii wamezungumzia kuwepo na madai ya wagombea na watiania kutoa taarifa za uzushi na za kubambikiana zinazowatuhumu wengine kuwa wanatoa na kupokea rushwa.

Hilo ni jambo la kuutahadharisha umma na wagombea kuhusu tuhuma ambazo zinaweza kuathiri mchakato wa uchaguzi unaohusisha kutoa taarifa za kuwasingizia wagombea ili mradi anayetaka kushinda uchaguzi akifanya juu chini kuwaumiza wale anaoona ni mahasimu wake.

Kupinga na kukataa rushwa wakati huu wa uchaguzi ni jambo ambalo kila mmoja anatakiwa kulizungumzia na pia kushiriki vita vya kuikomesha na kusaidia umma kufanikisha juhudi za kuitokomeza ziwe endelevu.

Katika mchakato wa wagombea ubunge kujipitisha majimboni, kuliripotiwa taarifa za kukamatwa kwa baadhi ya wagombea wakituhumiwa kutoa rushwa kwa wajumbe.

Waliotuhumiwa kujihusisha na mlungula walikamatwa na kuhojiwa na Takukuru ili kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo huku wengine wakiachiwa baada ya kubainika hawakujihusisha na vitendo hivyo.

Hayo, yalithibitishwa na Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia John Mbung'o, wakati akihojiwa na Radio One kuhusu changamoto ambazo taasisi yake inakutana nazo katika kupambana na rushwa ndani ya vyama.

Wakati ikifuatilia tuhuma hizo, Takukuru ilibaini kuwapo kwa mtindo wa baadhi ya wanasiasa kubambikiana tuhuma hizo kwa lengo la kuharibiana katika kinyang'anyiro cha kusaka uongozi.

Kiongozi huyo alithibitisha hayo na kuwataka wanasiasa kuacha mtindo huo wa kupakaziana mambo ambayo hayapo, kwa lengo la kuharibiana katika safari ya kusaka ubunge au udiwani.

Mtindo huo unaweza kusababisha au kukwamisha ajenda ya kupata viongozi bora, kwa sababu wachache wenye nia ya kupata madaraka wanaotafuta uongozi hata kwa mbinu za udanganyifu kama hizo.

Anasema mgombea anapotuhumiwa kujihusisha na rushwa, wakati mwingine inaweza kuwa vigumu kuaminika kwa wapigakura hata kama atakuwa amesafishwa kwamba hakuhusika, hivyo kujikuta akikataliwa.

Ili kuondoa changamoto hiyo jambo la muhimu ni kutojihusisha na siasa za kuchafuana baadala yake kila mmoja atafute nafasi ya kuchaguliwa na wanachama wenzake kwa kujenga hoja na ahadi za kweli kwa lengo la kuwaletea maendeleo.

Kwa mfano, CCM kwa upande wake, ilishatoa onyo na kuwataka makada wake kutojihusisha na rushwa, lakini matukio ya baadhi yao kukamatwa kwa rushwa yalisikika kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, katika uchunguzi wake, Takukuru inabaini kwamba tuhuma nyingine ni za kubambikiwa kwa lengo la kuharibiana wenyewe kwa wenyewe, hali ambayo inahatarisha matarajio ya wengine katika siasa.

Yawezekana wapo walionaswa kwa rushwa, lakini kubambikiwa tuhuma za rushwa kwa lengo la kuharibu sifa za mgombea ili fulani apate nafasi ya kuwania ubunge au udiwani, si jambo la kuendekezwa.

Ni muhimu wanachama na makada wakawatambua watu wa aina hiyo na kuwatenga, kwani mtu akituhumiwa kwa jambo ambalo hajafanya hasa kusingiziwa kutoa rushwa ni vigumu kumsafisha kwa wapigakura wakamuelewa.

Lakini, pia wale ambao wameshindwa kuzingatia maelezo ya vyama vyao, inawezakana Takukuru itaendelea kuwakamata, kwani kutoa rushwa au kupakazia wengine kupata uongozi ni sawa na kusema ni siasa za majitaka.

Pamoja na hayo, hata wapokea rushwa wanatakiwa kutambua kuwa mtoa rushwa na mpokeaji, wote kapu lao ni moja, na inawezekana baadhi ya wanasiasa wamenaswa kwa rushwa kwa kushawishiwa na wapokeaji.

Aidha, wapigakura nao wasiwe chanzo cha wagombea kutoa rushwa, kwa ahadi ya kusaidia kuwaunga mkono, katika kinyang'anyiro, badala yake waachwe wajinadi wenyewe ili hatimaye sanduku la kura liamue mbivu na mbichi.