‘Nyakuanyakua’ na tochi za usiku ziwazindue madereva

20Dec 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
‘Nyakuanyakua’ na tochi za usiku ziwazindue madereva

KATIKA jitihada za kukabiliana na ajali za barabarani, askari wa polisi wa usalama barabarani au trafiki, wameanza kuwanasa madereva wanaoendesha magari kwa kasi kubwa usiku, kinyume na inavyoelekezwa kisheria.

Lengo la kufanya hivyo, ni kukomesha mchezo huo ambao ni chanzo cha vifo vya watu wasio na hatia.

Trafiki wamekuwa wakikagua magari usiku, baada ya kubaini kuwapo uvunjaji wa sheria, kwa vile baadhi ya madereva wanafanya hivyo, wakidhani kwamba askari hao hawapo kazini usiku.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu, amekaririwa na vyombo vya habari akisema kuna juhudi za kikosi chake katika kukabiliana na ajali hizo za barabarani.

"Tunawanyakua wakati wowote, kwa sababu mwendokasi wa mchana, sasa wameuhamishia usiku. Haiwezekani ajali ziendelee kupoteza maisha ya watu kwa uzembe wa mtu mmoja," anasema Kamanda Musilimu.

Nikirejea katika hoja ya msingi, ni kwamba juhudi hizo za trafiki ni budi ziungwe mkono, ili kukomesha mtindo huo wa baadhi ya madereva hao, kwa kuwa ni kweli wakati wa usiku baadhi yao wanaendesha mabasi kwa fujo, kufidia muda uliopotea mchana, hali inayochangia madhara makubwa iwapo hawatadhibitiwa mapema.

Ikumbukwe inapotokea ajali usiku, inaweza kuchangia hali mbaya zaidi kwa abiria, kwa kuwa majeruhi wanapkosa msaada wa haraka, unakuwa mtihani mkubwa.

Ingawa ni kweli ‘ajali haina kinga,’ lakini kinga vilevile ni bora. Ninaamini hatua ya ‘kuwapiga tochi’ madereva wanaoendesha mabasi kwa kasi kubwa nyakati za usiku na kuwanyakuwa, kunaweza kusaidia abiria kuwa na uhakika wa kufika salama safari yao.

Ni vyema, kila mmoja wetu atambue kwamba ajali za barabarani zinaua watu wengi na hasa watoto na vijana, pia inadaiwa zinazidi hata vifo vinavyotokana na maambukizi mbalimbali.

Kwa mfano, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), linataja ajali za barabarani kuwa ndio zinasababisha vifo vingi vya watoto na vijana duniani, hao ni watoto na vijana wenye umri kati ya miaka mitano hadi 29.

Wakati Afrika ndio ina ajali nyingi barabarani, inaelezwa Waafrika na Wamarekani Kusini, wakiwa hawana sheria nzuri za kudhibiti mwendokasi.

Kama nilivyosema awali kuwa ajali haina kinga, kimsingi vifo hivyo havikubaliki, hakuna sababu inayotetea matukio hayo, kwa sababu hilo la tatizo linatafutiwa ufumbuzi, kazi inayofanywa hivi sasa na trafiki.

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), iliwahi kusema asilimia 76 ya ajali za barabarani nchini, zinatokana na makosa ya binadamu. Kati ya hizo asilimia 40 ni uzembe wa madereva.

Kutokana na hali hiyo, madereva wamekuwa wakihimizwa kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani, ili kuepusha ajali zisizo za lazima, ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

Taarifa za Jeshi la Polisi nchini, zinaonyesha kuwa ajali za barabarani mwaka huu zimepungua kuliko za mwaka jana. Hiyo inaweza kuwa habari njema iwapo ajali zitaendelea kupungua zaidi na zaidi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi, anasema kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, zilitokea ajali chache sana, kuliko za mwaka jana.

Anasema, ajali za mwaka huu zilipoteza maisha ya watu 1,661, huku za mwaka jana waliokufa walikuwa 2,250, hivyo idadi ya ajali na vifo vimepungua.

Nashauri hilo lisiwafanye madereva kubweteka, bali waendelee kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani.

Wakifanya hivyo, watachangia kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani, zinazotajwa kuua watu wengi kuliko ugonjwa hata maradhi hatari.