2018 isiwepo migogoro wakulima,wafugaji 

31Dec 2017
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
2018 isiwepo migogoro wakulima,wafugaji 

BAADHI ya wilaya hapa nchini zimekuwa zikikabiliwa na migogoro ya ardhi kati ya makundi ya wakulima na wafugaji na kusababisha wengine  kupoteza maisha na uharibifu wa mazao na mashamba.

Mbali na uharibifu wa mashamba, mifugo nayo imekuwa ikiteketezwa katika migogoro hiyo, ambayo kwa sasa ni kama imetulia kiasi, lakini siyo vibaya kuwakumbusha kuzingatia amani.

Migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa ikiibuka mara kwa mara imenisukuma nitoe mtazamo wangu kwamba tunapoingia mwaka mpya hata wakulima na wafugaji nao wafungue ukurasa mpya wa maelewano ya kudumu.

Mungu aliwaumbia  binadamu ardhi akitambua kwamba ina umuhimu kwao na hata kwa viumbe mbalimbali wakiwamo wanyama, ndege, mimea na vingine vingi vilivyopo chini ya jua vinavyoshuhudia uumbaji wake.

Hivyo katika ardhi hiyo ndiyo ambayo binadamu wanaitumia kwa kilimo na matumizi mengine huku wanyama, ndege na viumbe vingine nao wakiitegemea kupata chakula chao na maji ili waendelee kuishi.

Maana yake ni kwamba ardhi ni rasilimali muhimu kwa ajili ya maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi na hasa viwanda, biashara, makazi ya watu na pia malisho kwa ajili ya mifugo.

Hata barabara ziwamo za kiwango cha lami, changarawe, udongo na nyingine nyingi hujengwa kwenye ardhi hiyo kwa ajili ya kurahisishia watu usafiri ukiwamo wa magari, pikipiki, baiskeli na hata kwa wale waendao kwa miguu.

Hivyo ardhi aliyotupa  Mungu inahitajika na vitu vyote hivyo, lakini bahati mbaya hapa imeanza kuonekana kwamba haina baadhi ya vitu hivyo,  hali ambayo inasababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya makundi hayo mawili.

Siku za nyuma ilikuwa ni kama jambo la kawaida kusikia wafugaji na wakulima wameuana au mashamba yamefyekwa na hata wakati mwingine mifugo kuuawa na pia mali za wawekezaji kuharibiwa kwa sababu ya mgogoro wa ardhi!

Kwa sasa  ipo haja kwa serikali kuangalia upya kama bado kuna viashiria vya uvunjifu wa amani miongoni mwa makundi hayo,  vifanyiwe kazi haraka ili kuanzia mwaka 2018 makundi hayo yawe na amani ya kudumu.

Ni vyema ikaeleweka kuwa ardhi ni rasilimali inayohitajika kwa maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi na pia kwa ajili ya binadamu na mifugo yao, hivyo isimamiwe kikamilifu ili kuhakikisha migogoro inakomeshwa.

Katika hili serikali haina budi kuangalia upya uwezekano wa kuzipunguzia majukumu halmashauri kwani Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2007 inaziruhusu kupanga miji huku zikiwa na majukumu mengi zaidi ambayo inaweza kuwa inachangia zishindwe kuwajibika ipasavyo kwenye suala la migogoro ya ardhi.

Wakulima na wafugaji nao wajifunze kutatua migogoro yao kwa njia ya amani badala kushikiana silaha za jadi na kuumizana au kusababisha mauaji yasiyo ya lazima miongoni mwao.

Kila mtu ana haki ya kumiliki ardhi, lakini ajabu ni kwamba wametokea watu wachache wanamiliki ardhi kubwa na kuacha wengi wakiteseka kwa kukosa sehemu ya kulima au kuchungia mifugo.

Ni vyema sasa serikali ikafuatilia na kubaini kama kweli wale waliopewa ardhi kubwa kwa kisingizio cha uwekezaji wanaitumia ilivyokusudiwa? Jambo lingine ni kwamba wafugaji nao wapewe elimu ya matumizi bora ya ardhi kwa kufundishwa ufugaji wa kisasa ili waachane na wingi wa mifungo ambao hufanya wahame kwenda huku na kule kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.

Kama ikiwezekana wawekwe kwenye ranchi zote ili waweze kufugia humo badala ya kuendelea kutangatanga na kusababisha ugomvi kati yao na wakulima kama ambavyo tumekuwa tukisikia ama kushuhudia wakiumizana kwa kugombea ardhi.