Aali hupatikana kwa ghali

23Oct 2021
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Aali hupatikana kwa ghali

KITU kizuri au bora huwa ghali au hakipatikani kwa urahisi. Hii ni methali ya kutumiwa kuwaonya watu kuwa sharti wawe tayari kuvumilia shida au matatizo kabla ya kufanikiwa wajue kuwa kitu kizuri hakipatikani hivi hivi tu.

Nchi ni eneo la ardhi lenye utawala wake; dola. Sehemu ya ardhi ambayo imegawanywa kwa mipaka ya kisiasa na inayotambulika kwa jina la taifa lake. Kwa mfano Tanzania, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, China, India, Marekani, Ufaransa, Italia n.k. Wazawa wa nchi huitwa wananchi yaani raia wa nchi husika.

Kwa maana nyingine ni kama nasaba yaani uhusiano wa kizazi baina ya watoto na wazazi au wazee wao; = uzawa;
utungo.

Pia uhusiano wa watu wenye uzao mmoja, uhusiano wa watu wanaotokana na ukoo mmoja. Kwa hiyo ingawa Tanzania ni nchi yenye mikoa mingi kama zilizvyo nchi zingine duniani, twapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali yetu ambayo ni chombo kikuu kabisa chenye mamlaka ya kuendesha utawala wa nchi, chenye wizara mbalimbali.

Udugu, pia undugu ni uhusiano wa watu wanaotokana na uzawa mmoja; =ujamaa. Ndo maana marehemu Rais Julius Kambarage Nyerere (Mungu amrehemu) alisema makabila yote 120 yaliyokuwapo wakati ule yazungumze lugha moja yaani Kiswahili ili tuelewane. Hakuishia hapo kwani alisema watu wote tuitane ndugu bila kubaguana na ikawa hivyo.

Kwa ajili hiyo watu hawaoani kikabila kama ilivyokuwa zamani. Hakuna kubaguana kwani sote ni ndugu. Lugha ya Kiswahili yazungumzwa na makabila yote nchini na huelewana hata kama si wote wanaozungumza kwa ufasaha.

Upendo ni hali ya kuvutia moyoni na mtu au kitu; huba, mapenzi. Hali ya mtu kuvutiwa kimapenzi na kitu, mtu au jambo. Ni kweli kuwa Yanga na Simba zilikuwa moja mwaka 1935 kisha kutengana mwaka 1936 na sasa utadhani ni timu za nchi tofauti zenye uhasama usiozuilika.

“Ajabu” ni kitu kisicho cha kawaida, cha kushangaza na kustajabisha, -kigeni, si -a kawaida -a pekee, -a kioja.
Inanilazimu kueleza yote haya kwani Simba na Yanga utadhani ni watu wa mataifa mawili waliohujumiana, kupigana na kuwekeana shonde yaani hali ya watu kutozungumza pamoja kutokana na kugombana.

Sivyo bwana. Hawa ni watu wa Taifa moja la Tanzania tena wa mkoa mmoja na jiji moja liitwalo Dar es Salaam na kama haitoshi, makao ya vilabu vyao vipo maeneo ya Kariakoo. Kinachowafanya waingize tofauti zao mpaka kwenye timu za Taifa ni nini?

Ndio maana “Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.” Maana yake ukishangaa kutokana na miujiza ya Musa utashtuliwa na matendo ya Firauni. Matumizi yake ni sawa na: “Ukistaajabu ya chawa huona ya kunguni.”

Ni ajabu na kweli kwamba wanaokwenda kuangalia mechi za Simba na Yanga uwanjani ni wengi maradufu (ongezeko la mara mbili la kitu cha awali) kuliko wanaokwenda kuziangalia timu zetu za Taifa zinapopambana na timu ngeni za mataifa ya nje!

Hapana shaka huwa tunachekwa na kudharauliwa sana na timu za mataifa mengine zinapokuja kupambana na timu zetu humu nchini! Twachekwa kwa ujinga wetu.

Timu zetu za Taifa zinapopambana na timu za mataifa mengine, ni watu wachache wanaokwenda uwanjani kushangilia, tofauti kabisa zinapopambana Simba na Yanga ambazo hujaza watu pomoni yaani jaa hadi juu, tele, sufu sufu. Katika hali ya kujaa au kuwa -ingi. Ni ajabu lakini ndio ukweli wenyewe!

Kumbe ndo maana wahenga walisema: “Akili ni mali.” Kwamba akili ni sawa na mali. Haiwezekani mtu akafanya jambo likawa kama hana akili. Methali hii hutumiwa kumrejelea mtu ambaye anatenda mambo ya kufikiri au kutumia akili.

Pia husemwa: “Akili ya mtu ndio wazimu wake.” Yaani akili ya mtu yaweza kuwa wazimu wake pia. Methali hii hutumiwa kuelezea kuwa akili ya binadamu inaweza kuzua mema na mabaya pia.

Bila shaka methali hii inayofuata itatutoa usingizini kwamba: “Mtambua ndwele (ugonjwa) ndiye mganga.” Maana yake anayegundua ugonjwa ndiye tabibu anayeweza kuirekebisha. Kwa maana hiyo tunapaswa kuzinduka ili tujirekebishe na kuondokana na ubozi (upumbavu) wetu.

Je, mwajua kuwa “urafiki ni mzuri lakini udugu huzika mtu?” Maana yake urafiki ni kitu kizuri lakini tunapaswa kuwathamini jamaa zetu kwa kuwa ndio wanaoweza kutufaa wakati wa shida au hata kutuzika tunapofariki.

[email protected]

0784 334 096