Abiria achague kinyaa cha ‘helmeti’ au kifo

17Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Abiria achague kinyaa cha ‘helmeti’ au kifo

LICHA ya utetezi kuwa Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973 haimlazimishi abiria wa bodaboda kuvaa kofia ngumu au helmeti, ni vyema watu kuvaa kofia hizo kwa ajili ya usalama wao.

Umuhimu unajitokeza zaidi wakati huu wa sikukuu za Noeli na Mwaka Mpya, ambazo zina changamoto nyingi barabarani kutokana na ulevi, uendeshaji mbaya unaosababisha ajali ambazo kwa upande wa pikipiki maisha yangeokolewa kwa kuvaa helmeti.

Ni wakati wa kuamua kupoteza maisha au kujidanganya kuwa unaionea kinyaa au kuivaa kofia ngumu kunakuweka kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa ya ngozi.

Ni upungufu ambao umezungumziwa mara kadhaa kuwa sheria hiyo, inamtaka dereva pikipiki au bajaji kuvaa kofia ngumu, lakini haisemi kuhusu abiria anayetumia vyombo hivyo.

Ndiyo maana pengine ni wakati wa watu kuwajibika na kuamua kulinda maisha yao hata kama kuna upungufu kisheria.

Ripoti za Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, zinaeleza kuwa kutovaliwa kwa kofia hizo, ni sababu za vifo kwenye ajali za pikipiki.

Kwa mfano mwaka 2017 kulikuwa na ajali 1,459 zilizosababisha vifo 728 na majeruhi 1,090, takwimu za ajali kwa mwaka 2018 zilikuwa 876 zilizosababisha vifo 366 na majeruhi 994.

Zaidi takwimu zinaonyesha kuwa kutovaa kofia ngumu kunachangia vifo hivyo.

Msimu huu wa sikukuu una hatari nyingi hivyo ni vyema kuepusha kuwaumiza watoto ambao wanapandishwa kwenye pikipiki lakini bila kofia.

Ni vyema mamlaka za usafiri ardhini Latra na kikosi cha usalama kufikiria uwezekano wa kuwahimiza waendesha pikipikia na wazazi pamoja na walezi kuwa na kofia kwa ajili ya watoto.

Pamoja na kuwahimiza walezi na wazazi kuwa na kofia hizo ni wakati wa mamlaka za kusimamia usafiri kuwa na mikakati ya ukaguzi inayowabana waendesha pikipiki kuwa wasafi na kusafisha kofia ili kuepusha vifo vya abiria wanaokimbia helmeti chafu.

Abiria wanakiri kuwa kofi ngumu wanazopewa na waendesha pikipiki ni chafu, zinanuka, zina ukoko na baadhi zina chawa.

Ni tatizo kwa watu walionyoa kipara wanapata magonjwa yakiwamo mapunye, upele na chawa na vimelea vingine vya maradhi hasa mba.

Licha ya kwamba watu wangependa kuzivaa, lakini waendesha pikipiki ni wazembe na wasiojali kuwa kofia zao zinahitaji kufanyiwa usafi pia na kwa ujumla abiria wao ni wakazi wa miji yenye watu wa aina mbalimbali.

Mathalani Dar es Salaam, Tanga na Pwani ni maeneo yenye joto usafi wa kofia hizo ni muhimu kwa sababu zinabakiwa na jasho la abiria wanaozitumia.

Hata hivyo bora kufanya maamuzi na kuepusha kupoteza maisha. Kama unakusudia kuvaa kofia ni vyema kutembea na kofia nyingine laini ndani badala ya kujidanganya kuwa utachafuka lakini ukapoteza maisha.

Licha ya bodaboda kuchukuliwa kuwa ni hatari na zinaweza kusababisha ajali msimu huu wa sikukuu unawahusu watumia barabara wote ili kujiepusha na ajali.

Ni wakati wa kuendesha kwa makini na kuachana na mazoea ya kutumia babarabara kwa uhuru kupindukia.
Ujeuri huu unaonekana kwa baadhi ya madereva ambao hawajali na kujifanya wafalme wa barabara.

Mbali na kujitumbukiza barabarani hata ndani ya njia za mabasi ya mwendokasi ya Dar es Salaam.

Ubabe na kutumia barabara bila kujali wengine unawaponza watu wasiokuwa na hatia wakiwamo watoto na wenye ulemavu ambao hujeruhiwa na wengine hupoteza maisha.

Polisi wanaweza kusaidia kupunguza athari kwa kutumia kipimo cha ulevi barabarani ili kuepusha hatari ya wengi kupoteza maisha.