Acheni kuwahamasisha watoto kuboronga shuleni

12Jan 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Acheni kuwahamasisha watoto kuboronga shuleni

WAZAZI na walezi ni wadau muhimu wa elimu wenye mchango mkubwa wa kuhakikisha watoto wanafanya vizuri katika masomo na mitihani, kwa ajili ya maendeleo yao ya baadaye.

Hata hivyo, kumekuwapo na madai kwamba, baadhi hushiriki kuhujumu ndoto za watoto wao kwa kuwashawishi wafanye vibaya katika mitihani ya mwisho ili wasiendelea na masomo ya sekondari.

Wanafanya hivyo ili kuwatumia katika mambo yao ikiwamo kuwaozesha na wengine kuwafanyisha kazi za kilimo na ufugaji na kukwamisha kufanikisha ndoto zao za baadaye katika elimu.

Hao wanaofanya hivyo ni wale wenye malengo mabaya kwa watoto wao, na serikali imekuwa ikiwaonya na kuwataka waache mtindo huo, lakini bado wapo ambao wanaendelea kuundekeza upotoshaji.

Juhudi zote zinazofanywa na serikali za kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne, hawazioni, wanajali maslahi yao binafsi ambayo kimsingi hayawezi kuwasaidia watoto wao.

Mfano mmojawapo ni wazazi na walezi wa mkoani Mtwara, hasa katika wilaya za Nanyumbu na Tandahimba, ambao wanadaiwa kufurahia anguko la watoto wao kwa kuwalazimisha kufanya vibaya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kwa muda mrefu.

Hilo linathibitishwa na Ofisa Elimu wa Wilaya ya Nanyumbu akihojiwa na redio moja, kwamba baadhi ya wazazi wa watoto walioshindwa mtihani huo, katika Shule ya Msingi Kilimahewa walifanya sherehe kufurahia kufeli kwao.

Kitendo hicho kinatishia ustawi wa elimu kwa watoto, kwani wazazi na walezi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwaelekeza ama kuwafundisha kuzingatia masomo, kwa ajili ya maendeleo yao ya baadaye.

Wazazi na walezi wana wajibu wa kuhamasisha watoto wao kufanya vizuri katika masomo na mitihani yao ya mwisho, lakini wanapogeuka kuanza kuwashawishi wafanye vibaya, wajue kuwa wanadidimiza elimu.

Ni jambo linaloshangaza katika karne hii kuna mzazi ama mlezi anayefurahia mtoto wake kufanya vibaya kwenye mtihani. Hiyo inaonyesha kuwa watu aina hiyo elimu si kitu chenye umuhimu kwao ndiyo maana wanahamasisha watoto wasifaulu.

Hii siyo karne ya mzazi ama mlezi kuhamasisha mtoto kubaki mbumbumbu akikaa nyumbani ili kusaidia kulima, kuvua, biashara, kuolewa au kuozeshwa kwani yote hayo hayanufaishi familia wala watoto.

Uhamasishaji wa mtoto kupenda shule ama elimu unaanzia nyumbani, kutokana na ukweli kwamba, mwalimu wa kwanza wa mtoto ni mzazi mwenyewe au mlezi.

Lakini hao wote wakiwa ni maadui wa elimu, ni wazi mtoto hawezi kusoma na hata akibahatika kupelekewa shule, hawezi kuwa na maendeleo mazuri darasani, kwa kuwa hana mtu wa kumhamasisha kupenda shule.

Kimsingi, elimu bora inahitaji ushiriki wa wazazi na walezi, lakini pia jukumu lao kuhakikisha watoto wanapata elimu na siyo kuacha wahudhurie shule tu na kisha kushawishiwa kufanya vibaya katika mitihani.

Wazazi na walezi wana nafasi kubwa na wajibu wa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shule na kujifunza, kuwa na nidhamu ili waweze kufanya vizuri katika masomo na hatimaye watimize ndoto zao za baadaye katika elimu.

Wapo wazazi na walezi wenye shauku ya kuona watoto wao wanafanya vizuri katika masomo, lakini kuna wanaofurahia kufeli kwa watoto wao, hali inayoonyesha kuwa hawaoni umuhimu wa elimu.

Kwa ujumla mtindo huo unakwamisha maendeleo ya watoto wao kielimu, hivyo ni vyema ukatafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili wahusika wasiendelee kuvuruga ndoto za baadaye za watoto wao kwa kuwatungia sheria ndogo ndogo za kuwabana wahusika ikibidi washtakiwe.

Ni wakati wa kutambua kuwa fedha zinazotumika katika elimu bure zinatokana na makusanyo ya kodi kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo wananchi wenyewe ambao ni wazazi na walezi hivyo washirikiane na serikali kufanikisha lengo jema la taifa la kuona kuwa kila mmoja anasoma.