Afya pia inategemea maji, wanajamii tuvilinde vyanzo

16Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Afya pia inategemea maji, wanajamii tuvilinde vyanzo

MAJI ni muhimu kwa viumbe vyote duniani. Serikali kupitia kampeni yake inasema ‘Maji ni Uhai.’ Maana yake ni kwamba, bila ya maji, hakuna uhai unaofanyika.

Pia, ni hitaji la kiafya na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo inakuwa muhimu kutunza na kulinda vyanzo vyake.

Vilevile, upatikanaji majisafi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na usafi wa mazingira, ni sahihi mno katika kulinda afya za umma.

Hiyo ni kwa sababu, matumizi ya maji machafu yanachangia milipuko na kuenea magonjwa. Hapo panatajwa maradhi kama kuhara na kipindupindu.

Hapo ndio sababu ya kuwapo haja ya kuharakisha uwiano wa mgawanyo wa maji, kati ya sehemu moja na nyingine ndani ya jamii.

Juhudi zimefanyika kwa ajili ya kuhakikisha huduma hiyo inatosha nchini, lakini bado yapo baadhi ya maeneo nchini, upatikanaji maji ni changamoto kubwa kwao.

Kuna baadhi ya maeneo ambayo huduma hiyo inapatikana, kukiwapo changamoto zake. Watu hawalindi mindombinu ya maji na hawazingatii usafi wa mazingira yao, kwa ajili ya afya kwa ujumla.

Suala la kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, ili kutoa huduma endelevu katika maeneo ya vyanzo vyake kwa jamii ya maeneo husika, ni jambo la msingi.

Mahali pa aina hiyo panapoachwa, matokeo yake ni hatari. Uimarishaji na uhifadhi wa mazingira kwenye vyanzo vya maji au katika visima vya maji, kunaweza kuboresha afya ya jamii kwa kuzingatia usafi wa mazingira na elimu ya afya.

Kwa ujumla, afya ya jamii inalindwa na jamii yenyewe kuhamasishana kuhusu matumizi bora ya vyoo, kutotupwa takataka ovyo na umuhimu wa upatikanaji huduma ya maji ya kutosha na salama.

Hivyo, ni vyema sasa jamii ikatambua umuhimu wa kulinda vyanzo, visima na mabomba ya maji yaliyopo kwa ajili ya usalama wa afya na mengine ya maendeleo.

Pamoja na jitihada za kiserikali kuendeleza huduma za maji kuanzia miaka ya 1970, ni jambo linaweza zikakwamishwa na baadhi ya wasiojua umuhimu wa kulinda vyanzo hivyo, visima na mabomba ya maji.

Lengo la Sera ya Maji ya mwaka 1991, lilikuwa ni kufikia mwaka 2002, serikali iwe imewapatia wananchi wote majisafi na salama katika umbali usiozidi mita 400. Hata hivyo, bado haijatimia.

Jambo muhimu zaidi ni pale huduma za maji zilizopo zikalindwa, badala ya wananchi kujiweka kando wakiamini siyo jukumu lao kulinda huduma hiyo kwenye maeneo yao.

Katika bajeti iliyoko sasa, wizara husika imetenga Sh. 733,284,075,000 kuboresha huduma za maji nchini, hivyo fedha hizo zitakapofikishwa katika huduma, jamii iwe tayari kulinda miundombinu ya maji.

Upatikanaji maji salama katika jamii, ni muhimu kwa ajili ya kupambana na umaskini na matatizo ya afya, kwani watu maskini ambao wengi wao wanaishi vijijini, wana nafasi finyu ya kupata huduma hiyo.

Kama nilivyoeleza awali, baadhi yao wanapopata huduma hiyo huwa ni wazembe kuitunza, hali ambayo kwa namna moja au nyingine, inachangia kuendelea kuwapo huduma duni ya maji.

Ikumbukwe kwamba magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya maji yanaweza kupatikana zaidi katika sehemu ambayo watu wanatumia maji yasiyo salama, wakati mwingine kwa kuchafuliwa wanajamii yenyewe.

Hivyo, umuhimu wa kulinda na kutunza vyanzo, visima na mabomba ya maji uko palepale kwa afya ya jamii husika na siyo kusubiri kutoka sehemu nyingine kuja kusimamia ulinzi.

Majisafi na salama ni yapi? Ni yale yasiyokuwa na uchafu na yako sahihi kiafya na kinyume chake ndiyo yasiyofaa kwa matumizi na hata mtumiaji kuishia kuhara na maradhi mengine kama kipindupindu.

Kuna njia mbalimbali za usafi katika vyanzo vya maji ikiwamo, kutumia visima vyenye mifuniko na kuhakikisha vinafunikwa baada ya kuteka maji, kunasaidia kuepuka taka kuingia visimani.

Ni bahati mbaya, kuna maeneo ambayo jamii haijaweka ulinzi katika visima vyao na hata inavifanya visiwe salama. Wapo wanaoiba mifuniko kwenda kuviuza kama chuma chakavu.

Hivyo ni tabia iliyozuka katika siku za karibuni, baada ya kuzuka tabia hiyo ambayo iko dhahiri inaweza kumalizwa kwa jamii yenyewe kutambua na kuthamini huduma ya maji, inapopewa ulinzi stahiki.