Ahadi tamutamu za kampeni!

20Sep 2020
Joseph Kulangwa
Nipashe
FIKRA MBADALA
Ahadi tamutamu za kampeni!

JUZIJUZI hapa, niko mahali nimechanganyika na watu, wala sijui wanatoka wapi, lakini nikaamini tu sote ni Watanzania na tunajadili mustakabali wa maisha yetu, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

Niliwasikiliza, mara nikajikuta nakurupuka na kuropoka, eti heri kusiwe na mfumo wa vyama vingi vya siasa! Kwa kweli sikujua kwa nini yalinitoka hayo? Eti nikimaanisha heri turudi kwenye mfumo wa chama kimoja.

Nilipojitambua sikutaka kusahihisha, kumbe nisikilize nitapokewaje hata kama nimefanya kosa, kwa kuwa kundi lile la watu haiwezekani wote waniunge mkono kwa kauli hii yenye ukakasi kwa wengine.

Lakini palipo na wengi pana mengi, wapo walioniunga mkono ingawa kimya kimya. Lakini wasiovumilia nao wakawapo. Akaibuka mmoja akahanikiza, “unasema nini wewe bwege?” Huku kanitolea macho na mate yakimruka, nikashukuru tu kuwa Kovidi alishajiendea kwa maombi ya Watanzania.

Nilipomtazama nikaona bado ananikodolea macho ananiambia “we bwege sema unasemaje, hebu rudia?” Nikaona sasa kama ni bhita basi na iwe mura. Nikajikuta narudia viiile vile, “bora vyama vingi vifutwe!” Nikamsikia anasema “hii mijisisiemu mibwege sana”.

Kama akaonekana anashindwa bhita vile, nami nikapata nguvu huku nikiungwa mkono na wachache kweli kweli, tofauti na wale waliomwambia marehemu shemeji yangu Francis Nyalali, kwamba walitaka kuendelea na chama kimoja miaka ile ya tisini.

Nilipopata nguvu, nikaona kama mbwai na iwe mbwai, nikataka sasa nifafanue kile ambacho sasa ni vema nikihalalishe tu, kuwa ndio msimamo wangu pale, nikichelea kuubadii nisijeonekana popo au kinyonga.

Nikawaambia “hivi mnadhani mimi bwege kama alivyosema huyo mjinga wenu hapo? Nina hoja. Hivi si mnaona kampeni zilivyopamba moto, tunatafuta Rais, wabunge na madiwani, halafu mtu tu anaibuka na kuja na miahadi ambayo haiwezi kutekelezwa!

“Hivi hizi nyomi mnazoziona hapa, kuna mtu anaweza kupika ubwabwa na kuku akaja kugawia watu waliofurika uwanjani mathalan pale Zakhem, Kirumba, Kambarage na kwingineko huko? Semeni ukweli kama si hadhaa za kisiasa?

“Tuwe wakweli, hivi mnakubali mtu anasimama hapa anasema mkimpa nji atahamishia bahari Dodoma, kweli? Eti atajenga mitaro ya maji yatoke Bahari ya India hadi Dodoma kweli? Halafu mnakubali kabisa kuambiwa kuwa mkimpa nji atajenga daraja kutoka Dar es Salaam mpaka Zanzibar, eti kwa kuwa mnatapika sana kwenye boti za Bakhressa?”

Yule jamaa yangu nikaona kama anataka kunisogelea anibatue kibao, sikubabaika akaishia kuniuliza, “unamaanisha nani sasa?” Nikamjibu kwa upole “ndugu yangu sikuja hapa kutaja majina, kama wewe hujasikia hayo jikalie kimya, kwani wewe msemaji wao?”

Alipotulia nikaendelea, “humjasikia mtu anasema mkimpa ubunge eti atashona pazia la kuzunguka Mlima Kilimanjaro ili Kenya wasiuone?” He, nikaona wanaangua kicheko hata adui yangu naye sasa ndiye anafuta machozi ya kicheko kwa ukosi wa shati lake chafuuu. Nikashangaa!

Nikamchokoza nikamwuliza; “eti braza wewe hujasikia hayo?” Akanigeuka akanijibu, “achana na mimi!” Mwanzo sikuamini, lakini baadaye nikaamini kuwa kumbe napambana na mvuta msuba. Lakini waliokuwa karibu naye wakanielewa.

Akajitokeza mwingine ambaye niliona kama ananielewa, akasema, “aah we jamaa achana na siasa hizi, watu wanatafuta kula tu humo, wala hakuna kitu, hizo wanaomba kura za kula tu, hawatafanya hayo wanayosema. Ahadi ngapi hapa tunapewa kila miaka mitano lakini zinayeyuka? Tulishageuzwa mabozi tu.”

He, mara kusanyiko lile likageuka la siasa kabisa kabisa, watu wakajadili mambo ya siasa, waliosema makali wakawa wanaonyana pale pale. “Ohoo shauri yako mbu kibao wapo hapa we ropoka tu”. Ghafla yule adui yangu akanishika mkono na kuniweka pembeni na kuniambia, “ mh lakini mshikaji umetufumbua macho na masikio unajua!”

Eti akaniambia naye anatoka katika moja ya vyama vile ambavyo havikusimamisha mgombea urais, bali vinashangilia mgombea wa chama kingine, huku wakiomba huruma ya kuachiwa angalau wabunge. Akaniambia, “bora turudi tu kule tulikokuwa kabla ya 1992”. Sikumwamini nikasepa zangu.