Aiyee asitishwe kuchezea Simba, Yanga

18Mar 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Aiyee asitishwe kuchezea Simba, Yanga

KWA sasa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania kuna Mtanzania mmoja anaitwa Salum Aiyee, ambaye anashindana na wachezaji kutoka nje ya nchi kwenye kuwania ufungaji bora.

Aiyee anaichezea Mwadui FC akiwa amefikisha jumla ya mabao 15, akiwaburuza kina Meddie Kagere wa Simba aliyecheka na nyavu mara 12 na Heritier Makambo wa Yanga akiwa pia na idadi hiyo ya mabao.

Hawa wawili ni wachezaji kutoka nje ya nchi, lakini Aiyee ni Mbongo.

Kutokana na kufanya vema, tayari anatabiriwa kuwa msimu ujao huenda asiichezee Mwadui na tayari baadhi ya klabu zimeshaanza kumnyemelea.

Nimesoma na kusikia baadhi ya wachambuzi wakimuasa kuwa awe makini asijiunge na timu za Simba na Yanga kwa sababu zitakwenda kushusha kipaji chake.

Hii ina maana klabu hizi mbili zina tabia ya kushusha vipaji vya wachezaji wengi nchini.

Binafsi, huu nauita ni uchambuzi, au mtazamo wa kukariri zaidi kuliko uhalisia. Na huu mtazamo huwa unatolewa zaidi mitaani na vijiweni na kuletwa moja kwa moja mezani bila ya kufanyika upembuzi yakinifu.

Na wengi wanaokariri, huwa hawaiingizi Azam kwenye ile tabia wanayodai ni kuua vipaji vya wachezaji kutoka klabu ndogo.

Wao wanaamini wachezaji kama hawa wenye uwezo wakienda Simba au Yanga ndiyo wataua vipaji, lakini wakienda Azam vipaji havifi.

Lakini tumeona mchezaji Mbaraka Yusuph akiwa kwenye ubora wake akienda Azam akapotea, vile vile Waziri Junior akitoka Toto African na kutua Azam, akazimika mpaka alipoibukia Biashara FC ndipo alipoanza kung'ara tena.

Hapa nilitaka kuweka sawa tu kuwa eti mchezaji akienda Azam basi kipaji chake hakifi ila zile timu kubwa tu.

Mimi namshauri Aiyee kama anajiona ana uwezo wa kuchezea Simba, Yanga au hata Azam na wameleta ofa nono basi asisite kwenda kwa sababu zinazotajwa.

Simba na Yanga haziui vipaji vya wachezaji na hazijawahi kufanya hivyo hata siku moja, ila wachezaji wenyewe ndiyo wanaoua vipaji vyao.

Mchezaji anapotoka timu ndogo mikoani kwenda timu kubwa anapaswa aongeze mazoezi mara dufu kwa sababu sasa atakamiwa na kila timu na si kama kule alikotoka.

Wachezaji wengi wa mikoani badala ya kufanya hivyo, wao wanabweteka wanapofika hapo kutokana na kusifiwa na mashabiki, pamoja na pesa wanazopata ambazo ni nyingi kuliko walikotoka.

Baadhi ya wachezaji hujiingiza kwenye starehe, kiburi na kuona wamemaliza kila kitu, hapo kiwango kinaanza kupungua.
Mchezaji anayejitambua kipaji chake hakiwezi kufa atakapojiunga na Simba na Yanga.

Ndiyo maana tumeona kina Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin wakitoka Mtibwa Sugar na kwenda Simba, lakini uwezo wao ukaongezeka mara ndufu, mpaka sasa mmoja wao yupo nchini Misri akisakata soka la kulipwa.

Simon Msuva alijiunga na Yanga akitokea Moro United na sasa anacheza soka la kulipwa nchini Morocco.

John Bocco, Erasto Nyoni, Hassan Dilunga, Mohamed Hussein Tshabalala wamejiunga na Simba wakitokea timu mbalimbali na hadi leo ni wachezaji wa kutegemewa. Wangeogopa kwa sababu eti Simba inashusha viwango wasingefika hapo na walipo.

Fesal Salum 'Fei Toto' ametoka Zanzibar, hakuogopa kipaji chake kufa, anaingia Yanga na hadi leo ni kiungo tegemezi kwenye uwezo wa hali ya juu.

Wakati mwingine tunaogopesha wachezaji kwa vitu ambavyo havipo, badala ya kuwapa tahadhari ya wao wenyewe kujiangalia, kujichunga na kujilinda.

Aiyee kama atapata timu na kuridhika nayo kimaslahi asiogope kwenda kwa sababu hapo ndipo maisha yanapoanzia kwa kuwa hata Mbwana Samatta akijiunga na Simba akiwa mdogo, ikiwa na mastaa kama Mussa Hassan Mgosi, Patrick Mafisango, Felix Sunzu, lakini hakuogopa, alipambana na hadi leo tunajua mafanikio yake.

Aiyee anatakiwa ajiogope mwenyewe kwa kufanya vitu visivyotakiwa kwenye maisha ya soka na si kuogopa klabu yoyote ile duniani.