Ajabu ya maajabu kwa waandishi

09Aug 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Ajabu ya maajabu kwa waandishi

‘AJABU’ 1. jambo lisilo la kawaida linaloshangaza, kustaajabisha na kufurahisha. 2. Tamko linaloonesha kiwango cha kushangaza; -a kigeni, -a pekee, -a kioja. Pia isiyoaminika; -a kimiujiza.

‘Maajabu’ ni mambo ya kushangaza, mambo yasiyo ya kawaida; mastaajabu.

Waandishi wa leo hupenda mno kutumia maneno yaliyo tofauti na maudhui (wazo linaloelezwa katika maandishi au katika kusema) yake. Hawatumii kamusi ili kujua matumizi sahihi ya maneno watumiayo.

“Siku mbili za maajabu ya Chirwa” ni kichwa cha habari katika gazeti la michezo. Chini ya kichwa hicho kuna habari yenye paragrafu 13 lakini sikuona ‘maajabu’ ya Chirwa!

Paragrafu ya kwanza imeandikwa: “Straika wa Yanga, Obrey Chirwa, amerejea jijini Dar es Salaam kwa kishindo baada ya kutoweka kikosini na kurudi kwao Zambia kufuata baraka za familia yake kwa ajili ya kuja kuitumikia timu hiyo ya Jangwani.”

Mwandishi: “ … amerejea kwa ‘kishindo’ …” Hebu tuone maana ya ‘kishindo.’ 1. Vurugu, ghasia, kelele; kitendo kinachofanywa kwa makusudi kumkera au kumkasirisha mtu au watu hasa kama ni washindani. 2 sauti ya kitu kilichoanguka. Je! Chirwa alirejea ‘kwa kishindo?’

Tena mwandishi asema “ … baada ya kutoweka kikosini …” Tuone maana ya ‘toweka.’ 1. Kitendo cha kuondoka na kwenda mahali pasipojulikana; tokomea. 2. Ondoka mahali ghafla bila kuonekana; potea kabisa.

Chirwa hakutoweka bali aliaga. Hakuondoka kwenda mahali pasipojulikana. Aliaga kwenda kwao Zambia. Waandishi wasipotoshe matumizi ya maneno.

Waandishi pia hushindwa kuandika mtiririko mzuri wa sentensi ama kwa kujaza maneno mengi au sentensi kuandikwa shelabela/shaghalabaghala yaani bila mpango maalumu.

“Hatua ya Chirwa kwenda nchini kwao Zambia kuaga imekuja siku chache baada ya kusajiliwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara akitokea Zimbabwe katika kikosi cha Platinum F.C. kinachoshiriki Ligi Kuu nchini humo.”

Ingeandikwa: “Chirwa amekwenda kwao Zambia baada ya kusajiliwa na Yanga. Alitokea Zimbabwe kwenye timu ya Platinum F.C. inayoshiriki Ligi Kuu humo nchini.”

“Picha kamili ipo hivi wakati akija Dar, Chirwa alitokea Zimbabwe ambako alikuwa akiitumikia timu yake ya zamani ya Platinum mara baada ya kufika Dar akaenda moja kwa moja Uturuki kujiunga na wenzake kujiandaa na mchezo dhidi ya TP Mazembe, mechi hiyo ilipomalizika akawaambia viongozi wa Yanga anaomba siku mbili akamalizane na familia yake ikiwa ni pamoja na kukutana na viongozi wa Chama cha Soka cha Zambia (FAZ).”

Mwandishi katuandikia sentensi moja tu ya maneno 67! Sentensi hii haikuonwa na mhariri? Msomaji aliyoipitia kusahihisha hakuona udhaifu na tatizo la mwandishi?

Ingeandikwa: “Alipokuja Dar kutoka klabu ya Platinum ya Zimbabwe, Chirwa alikwenda uturuki kuungana na wenzake katika maandalizi ya kupambana na TP Mazembe jijini Dar es Salaam.

“Baada ya mechi ambayo Yanga ilifungwa 1-0, Chirwa akaomba ruhusa kwenda kwao Zambia kuiaga familia yake na kukutana na viongozi wa Chama cha Soka Zambia (FAZ).”

Nimeyagawa maelezo ya mwandishi katika paragrafu mbili na kuondoa maneno yasiyokuwa muhimu kama ‘picha kamili iko hivi,’ maneno ya mwandishi aliyoanzia paragrafu yake.

“Mara baada ya kutua Zambia, Chirwa alikuwa gumzo kubwa nchini mwake …”

Neno ‘mara’ maana yake ni urudiaji wa jambo kwa idadi ileile; ghafla, bila kukawia. Mwandishi hakuwa sahihi kutumia neno ‘mara.’ Angeandika: “Baada ya kutua Zambia Chirwa alikuwa gumzo.”

“Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alilithibitishia (jina la gazeti) juu ya kurejea kwa Chirwa kikosini huku akisema nyota huyo ataungana na wenzake katika mazoezi yatakayoanza kesho.”

Sentensi ingeandikwa: “Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alilithibitishia … kuhusu Chirwa kurejea kikosini akisema ataungana na wenzake mazoezini kesho.”

“Alisema wameamua kubaki Dar kutokana na kambi waliyoamua waweke kisiwani Pemba kuota mbawa kutokana na Uwanja wa Gombani hivi sasa kufanyiwa marekebisho.”

Ingeandikwa: “Alisema watabaki Dar kwani kambi ya Pemba imeshindikana kwa sababu uwanja wa Gombani unafanyiwa marekebisho.”

“Awali, TFF kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Celestine Mwesigwa, ilimwandikia barua Muro iliyosainiwa Juni 29 ya kumtaka msemaji huyo wa Yanga kwenda kujitetea kwenye Kamati ambayo ilipanga kukaa Julai 2 mwaka huu, kujibu shutuma zinazomkabili.”

‘Kamati … ilipanga kukaa’ ni tafsiri ya Kiingereza. Kwa Kiswahili kamati ‘haikai’ bali inakutana.

Ingeandikwa: “TFF ilimwandikia Muro barua kumtaka akajibu tuhuma dhidi yake kwenye kikao kitakachofanyika Julai 2 mwaka huu.”

Angalizo: Masahihisho yote haya yanatoka kwenye ukurasa wa pili wa gazeti nililolipitia!

Methali: Mgomba changaraweni haupandwi ukamea.
[email protected]
0715/0784 33 40 96