Ajali ya wanafunzi Arusha iamshe mamlaka zilizolala

14May 2017
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Ajali ya wanafunzi Arusha iamshe mamlaka zilizolala

SERIKALI imechukua hatua dhidi ya mmiliki na Mkuu wa Shule ya Lucky Vincent, mkoani Arusha, kwa kosa la kuzidisha abiria kwenye gari ililokuwa limewabeba wanafunzi na walimu 35 ambao walifariki.

Ni ajali mbaya kutokea nchini kwa wanafunzi 32 kufariki kwa wakati mmoja, walimu wawili na dereva na kuacha wanafunzi watano majeruhi na mmoja aliyenusurika.

Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda mkoani Manyara kwa ajili ya mtihani wa majaribio, ikiwa ni miezi mitano kabla hawajafanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. Wapumzike kwa amani watoto wetu, walimu na dereva. Amina.

Sina sababu ya kueleza kwa undani ajali hiyo wala hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika, na kutoeleza lolote ambalo tayari lipo mahakamani, bali kuzieleza mamlaka kuwa ajali hiyo iwe ni mwanzo wa ukaguzi endelevu kwenye shule binafsi nchini.

Shule nyingi hutumia usafiri wa mabasi ya wanafunzi kusafirisha kutoka makazi yao iwe nyumbani, mabwenini au kwenda safari za masafa . Ndiyo yanayowatoa shuleni na kuwarudisha nyumbani na pia kuwasafirisha kutoka kwenye makazi na kuwapeleka shuleni.

Kwa upande wa safari za shuleni wazazi hutoa fedha kulingana na umbali, ambayo hupangwa na shule na huongezeka kila wakati kwa kuwa gharama za uendeshaji hubadilika ikiwamo kupanda kwa bei ya mafuta na vipuri.

Hakuna viwango sahihi vya usafiri bali shule huamua kwa kadri wanavyoona na kuwa sehemu ya malipo muhimu ambayo mzazi anatakiwa kuyafanya kabla mtoto wake hajaendelea na masomo.

Pamoja na kulipa fedha hizo bado huduma ni mbovu kwa sehemu kubwa; kwanza mabasi mengi yanayotumika kubeba wanafunzi ni mabovu, yanabeba zaidi ya uwezo wake na mbaya zaidi hukamatwa na polisi na kuachiwa.

Ni kawaida kabisa kukuta gari la wanafunzi limeegeshwa likitengenezwa (ingawa ni kawaida kwa chombo cha moto kuharibika), na wakati mwingine kukamatwa na polisi wa usalama barabarani lakini huachiwa bila kuchukua hatua.

Ninawaza kwa sauti kuwa tukio la Arusha lisiwe linafanyika kwa shinikizo au utaratibu wa kukimbizana na matukio bila kuwa na hatua za kudumu zinazolenga kukomesha tabia fulani.

Ni vyema kukafanyika ukaguzi wa kushtukiza kwenye mabasi yanayobeba wanafunzi, mathalani kwa Dar es Salaam wanafunzi ‘hushindiliwa’ kama mizigo kwenye mabasi hayo, huku wakubwa au wanaoonekana wanene au warefu zaidi ya wenzao wakitakiwa kuwapakata wengine.

Ni kawaida kabisa kwenye nafasi ya watu wawili kukuta wamekaa wanafunzi wadogo sita, wengine wamesimama, madirisha yako wazi watoto wanacheza na hakuna usimizi thabiti.

Kwa jiji la Dar es Salaam kipindi cha joto wanafunzi hupata shida kutokana na kubanana huko, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kuambukizana magonjwa kama kifua kikuu (TB) na maradhi kama tetekuwanga.

Zipo shule ambazo kufika kwake magari hupita kwenye barabara za vumbi, mfano maeneo ya Madale, Kimara na Mbezi ambako kuna udongo mwekundu, cha ajabu magari mengine baadhi ya vioo vimevunjika na hakuna viyoyozi na hivyo wanafunzi kulowa vumbi wakati wa kwenda na kutoka shuleni.

Hali hii ni mbaya sana kiafya kwa kuwa mtoto mdogo hawezi kujikinga na vumbi na anapolivuta kwa muda mrefu upo uwezekano wa kupata maradhi ya kifua na macho na wakati mwingine minyoo kwa vile mayai yake huishi kwenye vumbi.

Magari kama Noah hutumika kusafirisha wanafunzi na huko hujazwa hadi kwenye buti, na magari hukimbizwa sana, wakati mwingine unapishana na gari la wanafunzi na kujiuliza dereva aliyepewa kazi hiyo alipimwa akili kwanza au la.

Ni vyema serikali ikakunjua makucha yake na kukagua shule zote binafsi, na kufanya hivyo nyakati za asubihi mara wanafunzi wanapofika shuleni na wakati wanaondoka na kuchukua hatua bila kuoneana haya wala kuruhusu nguvu ya fedha.

Tukio la Arusha liwe mwanzo wa serikali kuzifuatilia shule hizo ili kuokoa wanafunzi hawa, na siyo kusubiri ajali ambayo kwenye majeruhi au vifo idadi inakuwa kubwa kuliko inayopaswa kuwepo ndani ya gari.

Bila kufanya hivyo, ipo siku litatokea tukio ambalo litagharimu maisha ya wanafunzi wengi hasa kwa Dar es Salaam ambalo nina uzoefu nalo na mwendelezo wa tukio la Vincent ikawa ni kuchukua hatua kwa walimu na mmiliki.

Pia, shule zibanwe kuajiri madereva wenye sifa na kuwe na ufuatiliaji wa karibu kwao kuwa wanapoendesha gari hawajatumia kilevi chochote.

Pia, kuhakikisha taratibu zote muhimu za kusafirisha wanafunzi zinafuatwa ikiwamo kuwa na mwalimu, gari kuwa kwenye hali nzuri kwa maana ya uimara wake, muonekano kwa maana ya madirisha yote kuwa sawa na kuwalinda wakiwa safarini.

Tutafakari!