Aliyeanzisha chokochoko kuvunja ndoa hupata mgawo?

30Nov 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Aliyeanzisha chokochoko kuvunja ndoa hupata mgawo?

WATU wengi wamekuwa wakijiuliza ikiwa mmoja wa wanandoa aliyepelekea ndoa kuvunjika kama anastahili mgawo wa mali? Mfano, mwanamke katika ndoa anaanzisha chokochoko makusudi ili ndoa ivunjike apate mgawo wa mali aendelee na maisha yake.

Au mwanamume kwa tabia zake mbaya za ulevi au kutokuwa mwaminifu anapelekea ndoa kuyumba hadi kuvunjika na hapo basi, swali la msingi linapoibuka kuwa tuachane kila mmoja apate mgawo wake, licha ya kwamba kuna mhusika wa kuanzisha sakata.

Siku za nyuma kupitia safu hii , tulichapisha makala iliyozungumzia kuhusu namna ndoa inaweza kufikia tamati au ukomo na pengine kuvunjwa na misingi inayozingatiwa na mahakama katika kugawa mali kwa wanandoa (mke na mume) kwa mujibu wa sheria, hapa nazungumzia Sheria ya Ndoa Sura na. 29, 1971.

Kifungu cha 114 cha Sheria ya Ndoa ambayo hata hivyo Mahakama ya Rufani ilishataka ifanyiwe marekebisho na kuondoa kipengele cha mtoto kuolewa chini ya miaka 14, kwa ujumla sheria hiyo, inaeleza misingi ya kuzingatia wakati wa kugawana mali pale ndoa (baina ya wawili, mke na mume) inapovunjika.

Lakini bado tena katika kifungu hicho, kifungu chake kidogo cha 2(b) kinaeleza kwa kina kuwa kitu kikubwa ambacho kinapaswa kuzingatiwa wakati wa kugawana mali ni mchango wa kila mwanandoa katika kupatikana kwa mali zinazotakiwa kugawanywa.

Yaani kila mwanandoa awe mume au mke kwa nafasi yake ameshiriki kuchangia kwa namna moja au nyingine au kwa kiwango gani katika kufanikisha upatikanaji wa mali husika?

LA MUHIMU

Tafsiri ya mahakama kuhusu mchango wa mwanandoa katika kupatikana kwa mali za pamoja: inajumuisha ‘mchango wa pesa', majukumu aliyokuwa nayo au nguvukazi': halikadhalika, kazi za nyumbani anazofanya mama au baba mara nyingi hizi hufanywa na mwanamke kama kufua, kupika, kulea watoto, kutunza nyumba na zenyewe zinahesabika kama mchango mkubwa na wa kutosha katika kufanikisha upatikanaji wa mali zote ambazo zitachumwa na mwanaume au mwanamke moja kwa moja kulingana na nani hasa mwenye nguvu ya kipato zaidi.

Mwongozo au tafsiri hiyo inatokana na Shauri la Rufaa maarufu namba 9 la mwaka 1983, TLR 32 kati ya Hawa Mohamed na Ally Sefu. Kimsingi, wenyewe ndiyo msimamo hasa wa sheria, kila linapokuja suala masuala yanayohusika na kugawana mali.

Sasa, tukirejea katika msingi wa mada yetu ya leo. Mahakama kupitia kesi ya Robert Aranjo na Zena Mwijuma [1985] TZHC 5; (14 Machi 1985); 1984 TLR 7 (TZHC) inatupatia ‘jibu’ kama ifuatavyo.

Katika shauri hilo Robert Aranjo alikata rufaa Mahakama Kuu ikiilalamikia Mahakama ya Mwanzo na ya Wilaya kwa kumpatia mke wake robo ya mali kama mgawo anaostahili wakati mwanamke huyo ndiye aliyesababisha ndoa yao kuvunjika; huu ni baada ya mke kuamua kuondoka mwenyewe nyumbani kwa sababu anazozijua mwenyewe.

Hivyo basi, Robert aliamini kuwa mwanamke huyo asingestahili kupata mgawo huo wa mali aliyopatiwa, kwani yeye ndiyo hasa sababu ya ndoa yao kuvunjika.

Jaji Maina kama alivyokuwa kipindi hicho, alisisitiza kuwa suala la nani amesababisha ndoa kuvunjika halina uhusiano wowote na suala la nani anatakiwa kupata nini.

Hivyo basi, katika mambo yanayozingatiwa wakati wa kugawa mali pale ndoa inapovunjika swali la nani amesababisha ndoa ivunjike halina nafasi. Na kusisitizia kuwa kinachozingatiwa na kuangaliwa ni kile kilichoelezwa katika kifungu cha 114 cha Sheria ya Ndoa Sura na. 29, 1967 ambacho ni pamoja na mchango wa mwanandoa katika kupatikana kwa kila mali husika.

ANGALIZO

Mwisho, kwa kuzingatia hayo kwa wale wote ambao, kwa njia moja au nyingine, walikuwa wanatatizwa na suala husika jibu sahihi linapatikana kupitia maudhui ya makala haya.

Aidha, suala kinzani linaweza kuwapo na hoja zikaibuliwa mfano katika mazingira mengine kama vile sababu au chokochoko zilizopelekea ndoa kuvunjika au masuala ya dai la fidia kwa mwanandoa; lakini siyo kwa kuzuia kupata haki ya gawio la mali iliyochumwa na wanandoa.