Ama kweli fedha fedheha

28Mar 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ama kweli fedha fedheha

ILISEMWA na wahenga kuwa “fedha fedheha” wakiwa na maana fedha huweza kuleta mambo ya aibu baina ya binadamu. Methali hii yaweza kutumiwa kutuonya kuhusu maovu yanayoweza kusababishwa na fedha.

Pia walisema “Fedha ilivunja nguu, milima ikalala.” Maana yake fedha zina uwezo wa kuivunja milima na vilima. Methali hii yaweza kutumiwa kupigia mfano uwezo wa fedha. Mtu akiwa na fedha anaweza kufanikiwa kufanya mambo ambayo asingeweza kuyafanya wala kudhania kuyafanya.

‘Uongozi’ ni dhamana ya kusimamia jambo kwenye taasisi au penginepo; madaraka anayopewa mtu kusimamia au kuongoza shughuli. Hii si kazi rahisi kwani inahitaji hekima na kujitolea kwa hali na mali. Kuna wakati kiongozi hupaswa kutumia fedha zake ili kuweka mambo sawa kwa kile anachokiongoza.

Kwa hali yoyote iwayo, umwonapo mtu anayegombea nafasi yoyote ya uongozi, siasa (ubunge, udiwani au hata serikali za mitaa), michezo, hasa kandanda n.k. anagawa fedha au ‘zawadi’ ili achaguliwe, tambua mtu wa namna hiyo hafuati uongozi bali anafuata fedha ili ajinufaishe kwa jasho la wengine. Mtu wa namna hiyo hafai kupewa uongozi.

Janga (balaa) hili ndilo linaloisumbua Yanga na kusababisha wadhamini wao, GSM, kuchukizwa na kuandika barua ya kusimamisha misaada isiyo kwenye mkataba. Baadhi ya viongozi wanailalamikia GSM kwa madai kuwa inaingilia mambo ya uongozi! Wanataka fedha zinazotolewa na GSM wakabidhiwe viongozi ili wazigawe kwa wachezaji, badala ya GSM kuzigawa!

GSM wanasema fedha wanazotoa hazimo kwenye mkataba hivyo wanatoa kwa mapenzi yao. Kwamba ingawa wataendelea kuwa na Yanga, hawatatoa fedha zozote nje ya mkataba wao na klabu. Ni yale yale ya “Fedha ilivunja nguu milima ikalala.”

Sasa matawi ya Yanga yanatofautiana na baadhi ya viongozi wanaotaka GSM iwe inakabidhi fedha zake kwa uongozi wa klabu.

Viongozi wa aina hiyo ni wale niliowataja huko juu kuwa hugombea uongozi ili kujinufaisha badala ya klabu. Viongozi wa aina hii wanapaswa kuogopwa sana kwani kilichowapeleka Yanga si kuiletea maendeleo, bali Yanga ndio iwaendeleze katika mambo yao!

Tabia hii haikuanza leo kwani imekuwa mazoea ya baadhi ya viongozi wanaotaka kujinufaisha kwa fedha za wadhamini badala ya kuinufaisha klabu. Huko nyuma watu waliojitolea kusaidia maendeleo ya Yanga walijitoa walipogundua badala ya kuinufaisha klabu, waliwanufaisha viongozi waroho!

Kama mtu anajitolea kuwapa wachezaji hela ili wafanye vizuri, kwa nini alazimishwe kukabidhi hela hizo kwa viongozi wa klabu? Viongozi wanaodai kuwa anayewapa wachezaji fedha anakwenda kinyume cha klabu ilhali jambo hilo halimo kwenye mkataba, wana maana gani?

Enyi mliogombea uongozi kwa lengo la kujinufaisha, bora mjiuzulu mapema kabla ya kufukuzwa. Wafadhili wengi waliotaka kuibeba Yanga kwa hali na mali walijitoa baada ya kugundua fedha zao zinaliwa na viongozi walioingia klabuni kujinufaisha badala ya kuinufaisha klabu na wachezaji. Wakigundulika, wafukuzwe!

Viongozi wanaotaka GSM iwape wao fedha badala ya kuziwasilisha kwa wachezaji ambao ndiwo wanaostahiki, wao ndio waondoke Yanga ili wakaanzishe klabu yao.

Kuna wakati Reginald Abraham Mengi (Mungu amrehemu) alitaka kuifanya Yanga iwe ya kimataifa na kujitegemea yenyewe. Kwa maana hiyo alimtoa mchumi wake (naye Mungu amrehemu) kufungua ofisi klabuni Yanga ili afanye maandalizi ya kuiendeleza Yanga.

Baadhi ya viongozi walioona wamenyimwa fursa ya kutafuna fedha za klabu, wakawaweka wale waitwao ‘makomandoo’ kumvuruga Mengi pale alipoandaa mkutano wa Yanga na kumtukana. Akaona hakuna sababu kuwasaidia watu wasiokuwa na shukrani, akaondokea palepale Uwanja wa Uhuru.

Huo ni mfano mmoja tu bila kuwataja wengi waliojitolea kwa hali na mali kuisaidia Yanga lakini viongozi walaji wakatumia fursa hiyo kujinufaisha badala ya kuinufaisha klabu na wachezaji!

Mwaka jana kuna kiongozi fulani alithubutu kuliambia gazeti moja la michezo kuwa “kupiga pesa” si vibaya ila usizidishe! Kwa lugha ya mitaani, ‘kupiga pesa’ maana yake ni kula hela. Ndivyo baadhi ya viongozi walaji wanavyotaka kufanya kwenye klabu ya Yanga! HAWAFAI, HAWAFAI, HAWAFAI! Mwenye masikio asikie.

Kama kuna viongozi walioingia Yanga kwa lengo la kula hela, bora wajiondoe wenyewe wakatafute sehemu za kula magendo lakini watambue siku watakapokamatwa, watakuwa wageni rasmi kule Segerea wakisubiri mbivu na mbichi kwenye Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

“Epuka maovu nayo yakwepuke.” Unapoyaepuka mambo mabaya huwezi kufikwa na ubaya wowote. Methali hii yatufunza kujitenga na mambo mabaya yanayoweza kutuletea madhara.

[email protected]
0784 334 096