Anwani za makazi zilindwe kuepuka kugeuzwa vyuma chakavu

22May 2022
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Anwani za makazi zilindwe kuepuka kugeuzwa vyuma chakavu

​​​​​​​WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Tekonolojia ya Habari, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaendelea kuhamasisha uwekaji wa anwani za makazi kwenye mitaa na nyumba mbalimbali nchini.

Kazi hiyo inafanyika kupitia mamlaka za serikali za mitaa ambazo ndizo zina mitaa, vitongoji na nyumba zinazokaliwa na wananchi, lengo ni kurahisisha utambuzi wa watu kwa maana ya nyumba zao na mitaa yao kwa urahisi zaidi.

Kupitia uwapo wa anwani za makazi sasa mtu anaweza kukueleza kwake kwa kukwambia njoo mtaa Fulani, nyumba namba Fulani, hivyo kuondoa utaratibu wa zamani wa kumweleza mtu kuwa nyumba yangu ina rangi fulani au iko karibu na kitu au jengo fulani.

Kwa sasa, hata kwenye Google Map (ramani mtandaoni) mitaa imeingizwa, maana yake mtu anaweza kuandika kwenye anwani yake kuonyesha hadi mtaa anapoishi.

Unapojaza maombi yoyote nje ya nchi utaulizwa namba ya nchi yako yaani +255, jina la mtaa na nyumba namba, mara nyingi Watanzania wengi walishindwa kujaza kwa kuwa havikuwapo lakini sasa vipo na ni wajibu wetu kuzitumia.

Yako maeneo kuna ubishani mkubwa kwamba wananchi hawataki kulipia anwani hizo kwa mfano kibao cha mtaa inatakiwa kuchangiwa Sh. 80,000 na kibao cha nyumba Sh.4, 000. Wanaokataa  ni wale ambao hawajaelewa umuhimu wake.

Naamini wakielimishwa wakaelewa namna vina manufaa kwa maisha yao ya kila siku. Wengi wanavichukulia ni vibao tu ambavyo havina kazi yoyote bali serikali inatekeleza mradi wake tu, hivyo ni wa serikali.

Hii inaonyesha elimu inahitajika sana, kwa kuwa wananchi wasiotaka nirahisi hata kuhujumu siyo kwa kuikomoa serikali bali kutoona umuhimu wake.

Kwa muda mrefu Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inahangaika kushughulikia wanaong'oa alama za barabarani kiasi cha kuamua kuweka vya zege ambavyo bado vimebomolewa na kutoa nondo iliyomo ndani.

Kwingine wamelazimika kuweka chuma kizito ili anayeng’oa au kukata achukue muda mrefu au asiweze kabisa, lengo ni kukabiliana na wahujumu wa miundombinu ya barabara.

Licha ya kuwapo sheria ya inayolinda miundombinu, watu bila woga wameendelea kung'oa kwa ajili ya kuuza vyuma chakavu.

Biashara ya vyuma chakavu imeshika kasi nchini hususan mijini ambako watu hupita kutangaza kuwa wananunua vyuma chakavu. Ukiwaita wanakuja na mzani wao wanapima na kununua ulivyonavyo. Wengine  wameiba hadi sufuria na vifaa vya watu vyenye chuma na kuviuza.

Sasa kwa anwani za makazi zinazowekwa lazima elimu itolewe kikamilifu,viongozi wa mitaa na vitongoji wahusishwe ili wawe mabalozi wa kulinda, ili inapotokea mtu amehujumu anapopeleka kuuza, mnunuzi akatae kwa manufaa ya nchi yake.

Ni muhimu serikali kufuatilia kwa karibu biashara ya chuma chakavu maana tumeona hata miundombinu ya reli na madaraja imehujumuiwa na kwenda kuuzwa kama chuma ambacho huuzwa kwa kilo.

Bila kulinda miundombinu hiyo ambayo ni ya chuma baada ya kumaliza kuweka kutakuwa na kazi ya kukamata wanaong'oa na huenda kuna maeneo vimeshaondolewa.

Nimeona eneo la Kiluvya Hills, vimewekwa vibao vya kimo cha mtoto, vyembamba kiasi cha kujiuliza ndicho kiwango kilichowekwa? Je, kuna kiwango sahihi kilichoandaliwa kwamba anwani zitakuwa zimelingana hivi au vinaruhusiwa kutofautiana?

Kibao kama hicho ni rahisi kuondolewa kwa kuwa hakina uzito,ni bora kuwa na kiwango sahihi,kama ni cha mtaa basi kiwe kama cha alama ya barabarani ambacho ni ngumu mtu kuking'oa na kwenda kukiuza, maana yake itamchukua muda mrefu kung'oa au kukata chuma husika.

Bila kutoa elimu kwa wananchi kupitia kwenye vikao vyao vya mitaa na vijiji ili atakayeharibu akamatwe kirahisi, bila hivyo ikifanyika tathimini baada ya miezi sita mitaa mingi itakuwa haina vibao vilivyowekwa kwa gharama kubwa.

Lazima wananchi wajue ndiyo utaratibu wa kidunia, nimeshatembelea Marekani, Ulaya na Asia kote mitaa ina vibao vizuri vya kisasa vinavyoonyesha mitaa husika jambo linalompa mgeni urahisi kujua anakoenda.

 

Ndiyo maana leo hii unaweza kwenda mji fulani ukapewa ramani ikakusaidia, au ndiyo maana wanapokuja wageni kutoka nje hupenda kutumia ramani kwenda maeneo na sasa ulimwengu wa kidigitali umeleta Google map (ramani mtandaoni) itakayomwelekeza mtu kufika anapotaka kwenda.

Mungu ibariki nchi yangu.