Asante Rais kusikia kilio kodi simu, tuvute subira

23Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Asante Rais kusikia kilio kodi simu, tuvute subira

TOZO za miamala ya simu iliyoanza kutumika hivi karibuni, iliibua malalamiko kutoka kwa wananchi na kusababisha Rais Samia Suluhu kuguswa nayo ameagiza mawaziri husika kutafuta suluhisho.

Baadhi ya watumiaji simu walilalamikia kuwa makato ni makubwa wakati wa kutuma na kupokea fedha na kuona huduma hiyo kama mzigo mkubwa kwao na kutaka yafanyike mabadiliko.

Miongoni mwa yaliyosemwa na wananchi ni kwamba, huduma ya simu kwa sasa imekuwa ni moja ya huduma muhimu kwa Watanzania, hivyo haipaswi kuongezewa kodi na tozo hizo.

Badala yake, wakaishauri serikali kubuni njia za mapato kwa taifa, ili kuboresha huduma za kijamii kuliko kuumiza wananchi kwa ntozo za simu ambazo baadhi ya watu hawana uwezo wa kuzilipa.

Pamoja na nia nzuri ya serikali ya kuweka tozo hiyo kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii, lakini ushirikishwaji wa Watanzania katika mchakato wa upatikanaji wa sheria hiyo ulikuwa mdogo.

Kutokana na sintofahamu hiyo ya miamala, baadhi ya wananchi wakashauri kwamba serikali ingeweka kiwango cha fedha cha kuanza kukatwa tozo, angalau kianzie miamala ya Sh. 50,000.

Ushauri huo ulilenga kutowatoza Watanzania wa hali ya chini kwenye mzunguko rasmi wa kifedha, pia wakaiomba serikali kupunguza kiwango cha kodi kilichopo kwa kuwa makato yaliyowekwa ni makubwa sana.

Malalamiko hayo yalisababisha Rais aingilie kati na kuagiza mawaziri husika kutafuta suluhisho, ambalo Watanzania wanaendelea kulisubiri ili waendelee kupata unafuu waliokuwa wakiupata kwenye miamala ya simu.

Kwa kuwa Rais ameshaingilia kati, basi ni vyema wananchi kuwa na subira, ili hatimaye malalamiko yao yaweze kupatiwa ufumbuzi ili kuondoa mkanganyiko ambao ulijitokeza siku chache zilizopita.

Wakati kilio hicho kikiwa kinafanyiwa kazi, ipo haja pia ya kutoa elimu ya mlipa kodi ili kusaidia wananchi kutambua umuhimu wake na kuona fahari kulipa kodi, kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Hiyo inatokana na kwamba, ni wajibu wa Watanzania kuhakikisha serikali inakusanya kodi kwao, ili kuwahudumia, kwani ulipaji kodi unawezesha serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Maendeleo ndiyo hitaji kubwa la wananchi, lakini hayawezi kuja bila kulipa kodi, hivyo wananchi wakipata elimu ya kutosha ya mlipa kodi, watailipa bila kusukumwa na hata tozo za miamala halitaleta shida.

Ikumbukwe kuwa ulipaji kodi unasaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja na taifa kwa ujumla, pia huduma zote za kijamii zinatolewa kupitia kodi ambazo serikali hukusanya kutoka kwa wananchi.

Lakini, unapotokea utata kama huo ulio kwenye tozo za miamala ya simu, ni wazi kwamba kuna jambo linaloweza kuwa halijakaa vizuri aidha wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha ya mlipa kodi, au vinginevyo.

Ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, shule, miundombinu ya barabara, umeme na mingine mingi, hutegemea kodi, hivyo kila Mtanzania awe na elimu ya mlipa kodi.

Kodi pia inatumika katika mishahara ya watumishi na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na elimu ya msingi na sekondari bila ada, huduma hizo na nyingine nyingi, ni vyema wananchi wakaelimishwa kujua umuhimu wake.

Vilevile ni vyema kodi ikawa rafiki kwa mlipaji, ili asikwepe wala kulalamika, ingawa inawezekana wakawapo watu wanaolalamika kwa sababu zao nyingine kwa lengo la kutaka kukwepa.

Suala la kuendelea kuwaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ni la msingi, ili kila mmoja wao aone fahari kuilipa kwa ajili ya maendeleo yake na ya taifa lake kwa ujumla.

Pamoja na hayo, kuwa na subira kwenye tozo la miamala ya simu ni muhimu kwa kuwa kilio kimeshasikika na kinaendelea kufanyiwa kazi, kwa kuzingatia kwamba, subira huwa inavuta heri.