Asiyekubali kushindwa si mshindani

27Jun 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Asiyekubali kushindwa si mshindani

MTU asiyekubali kushindwa si mshindani. Methali hii hutumiwa kuwanasihi binadamu wakubali wanaposhindwa au kukiri udhaifu wao.

Wahenga walitwambia: “Kweli ingawa chungu niambie usinifiche.” Maana yake niambie ukweli hata kama una uchungu. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuwa na tabia ya kusema kweli au kuwa watu wasemao kweli.

Nimeona michezo ya Azam, Simba na Yanga ambazo ndizo timu kubwa nchini. Nakumbusha jinsi Azam ilivyocheza na Yanga Jumapili iliyopita na mchezo uliotangulia kati ya Simba na Mwadui ya Shinyanga, Simba iliposhinda kwa mabao 3-0.

Kwa maoni yangu, jinsi timu za Simba, Azam na Yanga zilivyo kwenye Ligi Kuu inayoelekea ukingoni, nathubutu (ingawa naumia moyo) kusema; kama jinsi zilivyo kwenye nafasi zake sasa, ndivyo zilivyo kwa namna zinavyocheza uwanjani.

Najua kuna watakaobisha. Wacha wabishe kwani kila mtu ana mtazamo na vionjo vyake. Ni dhahiri kuwa Simba wanajua kuumiliki mpira. Inapendeza jinsi wachezaji wanavyopasiana mpira uwanjani bila papara na namna wanavyofanya mashambulizi dhidi ya timu pinzani.

Kwa kuwa Simba ndio inayoongoza ligi kwa kuwa na alama 78, ni sahihi kusema wanastahiki kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo. Wamefunga mabao 67 na kufungwa mabao16 tu. Wamepata sare mara tatu na kupoteza mechi tatu na kushinda mechi 24.

Ingawa husemwa kandanda ni mchezo wa bahati, lakini kwa jinsi nilivyowaona wachezaji wa Simba walipopambana na Mwadui, nilivutiwa kwa namna walivyomiliki lile gozi la ng’ombe na kupeana pasi zenye uhakika, tena kwa mbwembwe. Hongera!
Kwa nini nisiwasifu ilhali mimi (Yanga), na wao (Simba), hatuivi hata tukipikwa chungu kimoja?

Wahenga walisema: “Kweli ikidhihiri, uwongo hujitenga.” Maana yake ukweli unapojulikana uwongo unajitenga. Twakumbushwa kwamba ukweli wa jambo fulani utokeapo, uongo unaolihusu hautambuliwi tena au hauna nafasi. Huweza kutumiwa kumnasihi anayejaribu kusema uongo wa waziwazi.

Mtu anapofanya jambo zuri ana haki ya kusifiwa na kupongezwa hata kama ni mpinzani wako. Usipomsifu au kumpongeza, wapo wengi watakaofanya hivyo na kukufanya wewe mwenye chuki kubaki ukikodoa.

Najua wenzangu wa Jangwani watanichukia ninapoeleza ukweli wangu kuhusu wapinzani wetu wa Msimbazi, lakini huo ndio ukweli wenyewe.

Wahenga walisema: “Kweli ndio fimbo ya kukamata” wakiwa na maana ya kweli ni silaha nzuri maishani. Methali hii yatukumbusha umuhimu wa kuusema ukweli hata kama kwa kufanya hivyo tutaishia kuchukiwa na wenzetu.

Hebu nitumie fursa hii kuwaambia wapinzani wetu (Simba) kuwa: “Angakaanga, tu chini ya gae.” Maana yake hata akikaanga vitu fulani sisi (timu ya wananchi) tuko chini ya gae alitumialo. Tutaishia kujua tu. Huweza kutumiwa kuelezea kuwa hamna siri inayofichika milele.

Ni kweli kwamba “Anayepanda kilele, hupiga kelele.” Maana yake mtu anayepanda hadi kileleni hupiga kelele kujitambulisha. Methali hii hutumiwa kumpigia mfano mtu aliyepata madaraka au cheo cha juu kisha akaanza kujivuna au kujishaua mbele za watu.

Nikumbushe tu kwamba Yanga inayojiita mabingwa wa kihistoria. Kwa nini? Kwa sababu ni timu pekee nchini kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nyingi zaidi.

Hata hivyo, “Hakuna refu lisilo na ncha.” Maana yake hakuna jambo lisilokuwa na mwisho. Methali hii hutumiwa kumliwaza na kumfariji mtu aliyefikwa na shida au jambo lolote zito kwamba avumilie kwa kuwa shida hiyo haitakuwepo milele.

Je, ndiko inakoelekea Simba sasa? “Hatua ndefu hufupisha mwendo.” Mtu atembeapo kwa hatua ndefu huikamilisha safari hata kama ni ndefu sana. Methali hii hutumiwa kumhimiza mtu anayefanya kazi ngumu na nzito kuwa ataishia kuimaliza, mradi aifanye hatua kwa hatua.

Kwa timu ya wananchi, methali ifuatayo iwatie nguvu: “Hauchi hauchi unakucha.” Mtu husema usiku hauchi, hauchi, lakini hatimaye jua huchomoza na usiku ukatoweka.

Timu zote mbili zinazoitwa ‘watani wa jadi’ ilhali ni ‘maadui wa jadi,’ hebu zisome methali ifuatayo, labda zaweza kujisahihisha na kuwa waungwana, yaani watu wenye tabia njema.

“Hasama (uadui) ndimi za moto.” Uadui au adawa ni kama ndimi za moto ambazo huchoma. Methali hii inatuhimiza tujiepushe na uadui unaoweza kutuletea maangamizo makubwa.

“Hasara humfika mwenye mabezo.” Maana ya ‘mabezo’ ni dharau au mapuuza yanayotokana na kudharaudharau.

Aghalabu hasara humpata mtu mwenye tabia ya kupuuzapuuza mashauri apewayo. Methali hii yatukanya tusiwe na tabia ya kupuuza mashauri tupewayo tusije kufikwa na hasara au madhara.

Mwisho wa yote kwa Simba na Yanga ni huu: “Mchimba kisima huingia mwenyewe.” Mtu anayemchimbia mwenzake shimo kwa dhamira mbaya huishia kuingia yeye mwenyewe.

Methali hii yaweza kutumiwa kumshauri mtu anayekusudia kumfanyia ubaya mwenzake kuwa huenda ubaya huo ukamrudia mwenyewe. Itakapokuwa hivyo atamlaumu nani?

TAFAKURI (Uwezo wa kuzingatia jambo).

[email protected]
0784 334 096