Avumaye baharini papa kumbe wengine wapo

02Dec 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Avumaye baharini papa kumbe wengine wapo

ANAYESIFIKA majini ni samaki aitwaye papa kumbe kuna wengine pia.

Methali hii yaweza kutumiwa pale makosa yanapotokea ambapo analaumiwa mtu fulani tu kumbe kuna wengine waovu na ambao hawajulikani.

Pia yaweza kutumiwa kwa mtu aliye hodari wa kufanya jambo kisha akatokea mwingine anayemzidi.

Kati ya Simba, Azam na Yanga timu ipi itazitangulia zingine na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayodhaminiwa na Vodacom msimu huu?

Nazitanabahisha (kumbusha) timu hizo kuwa “Atupaye tope hujichafua naye.” Mtu anayetupa au anayerusha tope huishia kujichafua. Ni kwamba anayejihusisha na ubaya au mabaya huishia kujiharibia sifa zake. Yaweza kutumiwa kwa mtu anayesema mabaya kuwahusu watu wengine yakamrudia mwenyewe.

Siku zote timu za Simba na Yanga huharibiwa na   mashabiki wasiokuwa na msaada wowote kwa vilabu     zaidi ya kuwa “domo kaya samli kwa mwenye ng’ombe.” 

Maana yake mtu anayesemasema sana (domo kaya)     hufananishwa na mwenye ng’ombe anayeisifia samlin yake.

Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu mwenye tabia ya kujisifusifu au anayevisifu vitu vyake sana hata kama vitu hivyo vina hitilafu au dosari.

Nayafananisha maneno ya mashabiki wa Simba na    Yanga na mafuriko yanayoleta maafa makubwa kwa binadamu. Kwa waliopata kukumbwa na mafuriko    wanajua maafa yake. 

Kuna waliozolewa na mafuriko, kadhalika walioangukiwa na nyumba baada ya maji kuzingira nyumba zao na kuingia ndani. Hao ndiwo wanaojua tamu na chungu ya mafuriko.

Mashabiki hudhani kuwa Simba na Yanga zitatawala   kabumbu la Tanzania milele kumbe sivyo. Brazili    iliogopewa na nchi zingine zote zilizoshiriki michuano ya  Kombe la Dunia. Sasa yaonekana timu ya kawaida kama zingine na yafungwa bila wasiwasi. 

Kuna timu 16 zinazoshindana kuwania ubingwa wa    Tanzania Bara na kila moja yataka kufanya hivyo. Lazima   tukubaliane na wahenga kuwa “mwenye kisu kikali ndiye     mla nyama.” Hapa hakuna mchezo wa ‘pata potea’ bali    timu iliyojiandaa vizuri ndiyo itakayokuwa bingwa.

Kuthibitisha unachosoma sasa, iangalie timu ya Singida United utaelewa ninachoandika humu. Hii ni timu  iliyoingia kwenye michuano ya Ligi Kuu msimu huu     lakini imeweza kuziacha nyuma timu 10 zilizokuwepo.

Nadhani hali hii inawafanya viongozi wa Yanga wajiulize mara mbili mbili ni kwa nini walimruhusu kocha Mholanzi,

Hans van der Pluijm, aliyewaletea mafanikio klabuni kwao kwenda Singida United. Bila shaka udenda unawatoka wakiona jinsi Singida United inavyosakata soka la kifundi. Lipuli nayo imeziacha nyuma timu 8 za zamani ikishika nafasi ya saba: Mbao, Majimaji, Kagera Sugar, Ndanda, Mbeya City, Ruvu Shooting, Mwadui na Stand United.  

 Tazama sasa jinsi mashabiki wasivyojua mpira hudunda na zikutanapo timu mbili kuna kushinda, kufungwa na sare.Katika mechi zilizochezwa juma lililopita, Yanga iliyokuwa wenyeji wa Prisons ya Mbeya ilitoka sare ya 1-1 kwenye uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam.

Baada ya sare ile mashabiki wa Simba wanaofahamu    msimamo wangu (Yanga) walinisakama kwa maneno  meengi ya kijinga (mniwie radhi) na ya kushangaza. 

Wakadai kuwa eti Yanga ilikuwa ifungwe mabao 6-0.     Kwamba timu ikitaka kuishinda Yanga, eti ichezeshe    wachezaji pungufu!

Jamaa walisema maneno mengi wakisahau kuwa    “mwenzio akinyolewa chako (kichwa)  kitie maji.”  Methali hii hutumiwa kumpa ushauri mtu ambaye mwenzake amefikwa na tatizo au shida kwamba anapaswa kujitayarisha au kutahadhari asije akakumbwa na shida hiyo.

Siku iliyofuata, Jumamosi kama ya leo, Simba (si wa porini, bali wa Msimbazi; ukipenda waweza kuwaita Simba ‘watu’) ikaingia uwanja wa Uhuru kupambana na timu ngeni kwenye michuano hiyo inayoitwa Lipuli.

Dakika ya 10 tu tangu mchezo uanze jamaa wa Msimbazi wakapata bao. Minong’ono na tambo za mashabiki zikaanza kuwa Lipuli wangefungwa mengi. 

He! Dakika tatu baadaye wakiwa wanafurahia kupata bao la kuongoza, Lipuli wakasawazisha!Mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na nahodha wa Lipuli ulitinga kimiani huku mlinda mlango wa Simba akiusindikiza kwa macho. Hakuweza kunyanyua mguu wala mikono yake.

Jumatatu ya wiki hii, Azam iliwakaribisha Mtibwa Sugar kwenye uwanja wao wa nyumbani, maarufu Azam   Complex. Mambo yaleyale yaliyotokea (kitendo cha   kutokea bila kutarajiwa) kwa Yanga na Simba yakaitokea    pia Azam ilipofungana na Mtibwa Sugar 1-1.

Timu zote tatu --- Simba, Yanga na Azam --- zilizotabiriwa kushinda, lakini utabiri wa vyombo vya habari haukutimia. Sijui kama waandishi wa magazeti ya michezo wanajua kuwa “Mdharau mwiba mguu huota tende” na “Ukubwa wa pua si wingi wa kamasi.”

Bila kutafuna maneno, tukubaliane kuwa Ligi Kuu yamsimu huu inasisimua ndio maana hizo ziitwazo timu kongwe hushinda kwa mbinde (taabu kubwa katika kufanya jambo) na wakati mwingine ‘hubebwa!’. Enyi mashabiki na baadhi ya wanachama wa Yanga na Simba mnaoshabikia kama vipofu, msikubali kutekwa na kutawaliwa na uzandiki (hali ya unafiki, hali ya umbeya; usongombwingo, uheke, uongo.)   

 [email protected]    0715/0784  33 40 96