Azam ipo ipo tu, haina presha

29Jun 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Azam ipo ipo tu, haina presha

BAADA ya muda mrefu kupita ikishika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, hatimaye Azam imeteremka hadi kwenye nafasi ya tatu.

Kwa sasa nafasi ya pili inashikiliwa na Yanga iliyofikisha pointi 60, huku Azam ikiwa imesalia pointi zake 59.

Hii ni baada ya Yanga kuichapa Ndanda mabao 3-2 na Azam kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Biashara United mjini Musoma.

Ingawa bado Ligi Kuu inaendelea na Azam inaweza kumaliza ikiwa kwenye nafasi ya pili, lakini kwa sasa iko kwenye wakati mgumu kwani imekuwa haipati matokeo mazuri.

Kwa muda mrefu, Azam ilikuwa inashika nafasi ya pili tena kwa pointi nyingi, lakini Yanga ambayo msimu huu haikuonekana ipo vizuri, tena ikiwa na sare nyingi sana, lakini imejivuta hadi kufika kwenye nafasi ya pili.

Hata kama Azam itarejea tena kwenye nafasi ya pili, lakini kwa jinsi ilivyo itapata shida sana. Ukizitazama timu hizi mbili, Yanga na Azam ni vitu viwili tofauti.

Azam inaonekana iko vizuri zaidi, ikiwa na wachezaji wenye vipaji na uwezo wa hali ya juu, pia kitimu inaonekana iko vizuri zaidi na ni timu yenye uwezo hata ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Kwa upande wa Yanga msimu huu, bado inaonekana inajikongoja tu. Siyo ile Yanga iliyozoeleka.

Huwezi kulinganisha uwezo wa wachezaji mmoja mmoja wa Yanga na wa Azam.
Bado Yanga ina wachezaji wa kawaida sana na ni wachache ambao wana uwezo mkubwa na kuweza kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Azam.

Tatizo ni nini hata Azam imeshindwa kufukuzana hata na Simba huko juu kileleni kwenye mbio za kutwaa ubingwa, achilia mbali kukutwa na kupitwa na Yanga?

Ni kwamba Azam pamoja na kwamba ni timu yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa, lakini inakosa watu wa kuwasukuma.

Inakosa watu wa kuwapigia kelele pale wanapofanya vibaya. Inakosa watu wa kuwakumbusha majukumu yao na kuwafanya wapambane kwa ajili yao. Si wengine ni mashabiki.

Kinachozitofautisha timu za Simba, Yanga na ile ya Azam ni mashabiki.

Mfano Yanga ambao kwa misimu miwili sasa haijakaa vizuri, lakini inapambana kwa sababu nyuma yake kuna mashabiki wanaoisukuma.

Hata kama ina wachezaji wa kawaida, lakini kuichezea Yanga inabidi upambane kufa na kupona kusaka ushindi ili kuwafanya wawe wa furaha.

Na hata wanapoukosa, wachezaji wa timu hiyo wanaona joto la jiwe. Mashabiki wanawashambulia kwa maneno mengi, hivyo wanapokwenda kwenye mechi inayofuata wanakuwa wamejiandaa kisawasawa.

Ikumbukwe ni majuzi tu, mashabiki wa Yanga walikuwa wakimpigia kelele Gnamien Yikpe na hata David Molinga kuwa hawawaelewi.

Lakini mechi iliyofuata dhidi ya Namungo, Molinga alirekebisha makosa yake, akajituma na kufunga magoli mawili.

Hata Simba, inaweza kushinda hata mechi sita mfululizo, lakini ya saba ikitoa sare, tayari mashabiki wanakuja juu na kuwatupia lawama wachezaji wao kuwa wanaishi vizuri, wanapata mishahara mizuri, lakini hawajitumi. Mechi inayofuata wachezaji wanafanya kila njia ili kupata ushindi.

Hili halipo kwa Azam. Hata wao waishi na kupata stahiki zao zote, lakini hawapati ushindi mara kwa mara kwa sababu, wakishinda sawa, wakifungwa poa na hata wakitoka sare hakuna tatizo.

Hakuna mtu wa kuwapigia kelele. Hakuna mtu wa kuwauliza. Wachezaji wanapanda basi na kuondoka kama vile hakuna kilichotokea. Hata mechi inayofuata inakuwa hivyo hivyo.