Azam ya Mapinduzi tuione Ligi Kuu

09Jan 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Azam ya Mapinduzi tuione Ligi Kuu

KATIKA mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanazania Bara na hata baadhi ya michezo ya mzunguko wa pili, mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC hawajafanya vizuri kiasi cha kujikuta ikiporomoka kutoka nafasi ya tatu mpaka ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Mbali na kuporomoka huko na kujikuta ikiachwa mbali na wapinzani wao wakubwa kwenye ligi klabu za Simba na Yanga, pia timu hiyo ilijikuta ikiwafungashia virago makocha wake wote wakiongozwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez kwa kile kilichoelezwa kufanya vibaya kwa timu ni sababu ya kuondolewa kwao.

Kwa sasa ligi imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.

Azam ni moja ya timu zinazoshiriki mashindano hayo huku ikionyesha soka safi na kuwa miongoni mwa timu zinazotabiriwa kuchukua ubingwa wa mashindano hayo kwa mwaka huu.

Mpaka sasa Azam na Simba (kabla ya mchezo wa jana wa Simba dhidi ya Jang’ombe Boys) ndio timu ambazo hazijapoteza mchezo wowote kwenye michuano hiyo ya mwaka huu.

Juzi usiku mashabiki na wadau wa soka walishuhudia mchezo mgumu ulikuwa ukisubiriwa na watu wengi, baina ya wababe wa Tanzania Bara, Azam dhidi ya Yanga.

Yanga iliingia uwanjani ikiwa na matumaini mengi, huku wachezaji wake wakijiamini zaidi hasa kutokana na matokeo waliyoyapata kwenye michezo miwili ya awali waliyokuwa wamecheza kabla ya mechi hiyo ya juzi usiku.

Kilichotokea katika dakika 90 za mchezo hakuna mdau au shabiki aliyetegemea kwani pamoja na wengi kuipa nafasi Yanga ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo, Azam walionyesha soka safi muda wote wa mchezo na kuwabana vilivyo Yanga iliyokuwa na kikosi chake kamili.

Ubora wa Azam kwenye mchezo huo ulikuwa katika safu ya ulinzi ambapo Frank Domayo wa Azam alimpiga ‘shoti’ mkata umeme wa Yanga, Zulu, na kuipa uhai timu yake kutawala katikati na kutengeneza nafasi zilizozaa mabao manne kwa Azam.

Ni wazi soka lililopigwa na Azam kwenye mchezo wa juzi ni la hali ya juu sana, waliwafunika kila eneo Yanga na kuzua maswali miongoni mwa mashabiki ni kwa nini soka lile la Azam halionekani kwenye michezo ya Ligi Kuu?

Hakuna ubishi kama Azam wangekuwa wanacheza vile walivyocheza juzi, basi wangekuwa miongoni mwa timu zinazokabana juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pengine inawezekana kweli mbinu za kocha aliyetimuliwa, Hernandez, hazikuwa zikifanya kazi ipasavyo ndani ya kikosi cha timu hiyo, kwani wachezaji aliokuwa akiwatumia wengi wao walicheza mchezo wa juzi na kuifanya Azam kucheza soka safi na la kasi.

Baada ya kuisambaratisha vibaya Yanga kwa ushindi wa mabao 4-0, mashabiki na wadau wa soka sasa wanasubiri kuona je, soka ambalo Azam wanalicheza Zanzibar katika michuano hii ya Mapinduzi litaonekana kwenye michezo iliyobakia ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara?

Na kama Azam wataonekana kubadilika kwenye michezo ya Ligi Kuu, hiyo itatoa jibu la moja kwa moja, kocha anayekaimu nafasi ya ukocha mkuu kwa sasa Iddi Cheche, atakuwa na kitu cha ziada na pia atakuwa anawafahamu zaidi wachezaji wa Azam.

Ni vema Azam ikaendeleza soka inalosakata Kombe la Mapinduzi, kwani vinginevyo itaonekana soka la Azam kwenye mchezo wa juzi usiku ilikuwa ni bahati waliyoamka nayo kuelekea kwenye mchezo ule.

Kwa upaande wa Yanga, sasa watakuwa wameamshwa na kipigo kile cha mbwa mwizi kutoka kwa Azam.

Ni wazi sasa kocha wa Yanga, George Lwandamina atakuwa ameonyeshwa udhaifu wa timu yake na haraka kuufanyia kazi.