Bado CCM inazunguka haijaanza kutekeleza kiundani ilichokiahidi 2015

24Feb 2016
Richard Makore
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Bado CCM inazunguka haijaanza kutekeleza kiundani ilichokiahidi 2015

KAMPENI za mwaka jana zilitawaliwa na maneno matamu mengi ambayo nina imani ndiyo yaliyowavutia wapigakura wakaichagua CCM kuongoza nchi hii.

Maneno hayo ama ahadi hizo ni pamoja na kutatua kero za maji nchi nzima ili suala hilo libaki historia, kuijenga viwanda vingi nchi nzima ili kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda na kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima.

Ahadi nyingine za CCM na Dk. Magufuli ambaye ni Rais ni ni kuhakikisha kujenga reli kubwa kutoa Dar es Salaam hadi Kigoma na kupambana na watumishi wa sekta ya afya wanaoiba dawa na kuziuza katika mduka yao,.

Nyingine ni kuhakikisha inaanzishwa magakama ya mafisadi ndani ya siku 100 kwa hili najua limeshindikana kwa sababu hizo tayari zimepita, kupeleka umeme vijijini, kuwafukuza kazi Mgambo kwa kuwa wanawasumbua mama Ntilie na hili pia naona limeshindikana kwa sababu bado wanaonekana.

Ni jambo zuri Watanzania kuyakumbuka haya kwa kuwa ndiyo yaliyowashawishi na kujikuta wakipga kura kwa CCM na Dk. Magufuli.

Haya ni machache lakini yapo mengi sana hususani huko vijijini kuna vitu viliahidiwa ili kuhakikisha Watanzania wanaishi katika maisha bora.
Miaka 10 iliyopita kati ya 2005 hadi 2015, Watanzani tuliambiwa maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana, lakini sina hakika kama hilo lilitekelezwa vizuri.

Nimeyasema haya kama Muungwana ili Watanzania wawe wanayakumbuka kila wanapomuona, Dk. Magufuli akikatiza mitaa na wanapowaona Mawaziri wake popote.

Huenda inachukiza na inaleta ukakasi mtu ama chama kinapokumbushwa walichokiadi ingawa kumekuwa na maneno mengi yakiwamo yanayotaka Watanzania kuipa muda serikali.

Hata hivyo huo muda haijawahi kufahamika ni lini utafika sasa hizi ahadi zianze kutekelezwa kwa vitendo.

Nakumbuka 2010, Watanzia hususani wanaoishi kando kando mwa Maziwa makubwa waliahidi Meli mpya kwa ajili ya usafiri, lakini mpaka serikali ya awamu ya nne inamaliza muda wake hilo sina hakika kama hilo liliwahi kusemwa wala kutekelezwa.

Muungwana akiahidi ni vema akatekeleza kwa vitendo ili awe na nguvu ya kuahidi tena kipindi kingine.

Watanzania wamekaa kimya lakini najua wanajaribu kutafakari hizo ahadi, kwa kuwa huenda hawaoni dalili za jiji la Dar es Salaam, kumaliza msongamano wa magari, kero ya maji, mama Ntilie bado wapo mitaani, vijana bado hawan ajira.

Yapo mengi lakini cha msingi yale yaliyoahidiwa yaanze kutekelezwa ama mwanzo wake basi uanze kuonekana kama ambavyo utumbuaji majipu unavyoonekana pamoja na elimu bure ingawa ina changamoto.