Bajeti elimu ifanikishe TEHAMA vijijini

17May 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Bajeti elimu ifanikishe TEHAMA vijijini

MATUMIZI ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanatajwa kuwa nyenzo muhimu kwa walimu na wanafunzi ili kuwaongezea uelewa zaidi kuhusu masuala ya teknolojia ya kidijitali madarasani.

Kutokana na umuhimu huo, kumekuwapo na juhudi mbalimbali za kuhakikisha watoto wanaanza shule ya msingi hadi vyuo vikuu wakiwa tayari wamefundishwa somo la TEHAMA.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa juhudi hizo, ufundishaji wa somo hilo unakwamishwa na changamoto ya ukosefu wa umeme kwenye baadhi ya shule, hasa za vijijini ambazo nyingi hazina nishati hiyo. 

Serikali imejitahidi kupambana na mazingira hayo kwa kufanya kila liwezekanalo, ili kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo, ili wanafunzi wote wa mijini au vijijini wapate fursa ya kujifunza somo hilo muhimu. 

Tangu mwaka 2005 TEHAMA ilianzishwa kwenye mtaala mpya wa Elimu ya Msingi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ili kumpa mwanafunzi maarifa na stadi za matumizi ya habari. 

Lakini inawezekana ukosefu wa nishati kwenye baadhi ya shule ukawa kikwazo, kwani hata kama shule itakuwa na vifaa vya TEHAMA kama kompyuta wanafunzi hawawezi kujifunza somo hilo kwa vitendo kwa ukamilifu. 

Ni imani yangu kuwa, kasi ya usambazaji umeme ikiongezeka, huku ikienda sambamba na uwapo kwa vifaa vya kufundisha somo hilo, ni wazi litawasaidia wanafunzi kuanzia mijini hadi vijijini. 

Kwa kuwa ahadi ya serikali ni kwamba, hakuna kijiji kitakachoachwa bila umeme, basi ni vyema nishati hiyo ikaharakishwa kusambazwa kwa kasi iwezekanavyo ili kufanikisha ufundishaji wa TEHAMA. 

Hilo likifanyika kwa ufanisi, wanafunzi wa shule za vijijini hawatabaki nyuma katika somo hilo, bali wote watakuwa wanakwenda kwenye uwiano na wenzao wa mijini katika uelewa unaolingana, kutokana na kujifunza kwa vitendo badala ya kubakia na nadharia zaidi. 

Jitihada zinazofanywa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ziwezeshe nishati hiyo kwenda shuleni badala ya kuishia katika nyumba za wanavijiji au katika maeneo ya biashara, shule nazo ziwe sehemu ya mradi huo.

 

Inawezekana idadi ya shule imeongezeka zaidi mijini na vijijini pia kupitia fedha za UVIKO-19, hivyo kila shule mpya kama ilivyokuwa ya zamani nayo inahitaji kipaumbele. 

Hata hivyo, ni jukumu la bajeti ya Wizara ya Elimu iliyopitishwa wiki iliyopita  kufanikisha upatikanaji umeme kwenye shule mpya na za kale ili kufikia hatima ya kufundisha TEHEMA nchi nzima.

 

Hayo yakifanyika, wanafunzi wa shule za vijijini hawatakuwa nyuma kwenye somo hilo huku wadau wa elimu nao wakishirikishwa ili kuhakikisha shule za huko zinakuwa na nishati na vifaa vya kufundishia somo hilo kwa tija na manufaa zaidi. 

Wadau wa elimu wakishirikishwa, wanaweza kusaidia kupatikana kwa nishati hata ya sola na kompyuta kwenye shule hizo za pembezoni kwa kujitolea kuchangia fedha, vifaa na mafunzo au  kununua vifaa hivyo ambavyo ni muhimu zama hizi za sayansi na teknolojia. 

Njia hiyo pamoja na kuwajengea uwezo walimu wa somo hilo, kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano duniani, wanaweza kufundisha kwa ukamilifu  na hivyo kuwafanya wanafunzi kupiga hatua kwenye elimu na maarifa yatokanayo na kufahamu TEHAMA. 

Hiyo ni njia mojawapo ya kuwapo kwa mazingira rafiki ya ufundishaji na ujifunzaji wa somo hilo kwa shule zote nchini, bila kujali kwamba ni za vijijini au mijini, kwani wanafunzi wote wanahitaji kufunzwa na kuelewa somo hilo lililopo kwenye mtaala. 

Pamoja na hayo, ufundishaji wa TEHAMA kwa kutumia Kiswahili,  ambayo ni njia bora, kwani lugha hiyo inasaidia kujenga saikolojia ya kujiamini na kujithamini na kujiongeza zaidi miongoni mwa wanafunzi.