Bajeti iangalie vyanzo vipya, itufikirishe

08Jun 2016
Restuta James
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Bajeti iangalie vyanzo vipya, itufikirishe

LEO macho na masikio ya Watanzania yataelekezwa bungeni Dodoma ambako Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, atakapokuwa anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2016/17.

Serikali ya awamu ya tano imejikita kwenye kuimarisha uchumi na kipaumbele ni kujenga viwanda na kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinaboreshwa.

Jitihada zinazofanyika sasa ni kuzalisha umeme wa uhakika utakaosaidiana na vyanzo vya maji vilivyojengwa wakati wa serikali ya awamu ya kwanza.

Ni wazi kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuleta mabadiliko yatakayoleta neema na kujenga upya mfumo wa uchumi, haki na sheria nchini.

Kuimarisha huduma za jamii kama elimu, afya, maji na makazi; kuondoa umaskini, kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa na makazi bora.

Wakati bajeti ikisomwa leo, ni lazima wabunge wajikite katika hoja zitakazoleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa kujielekeza kwenye mbinu zitakazoondoa umaskini, maradhi, ujinga na rushwa.

Tangu alipoingia madarakani, Rais Dk. John Magufuli, ameonyesha dhamira ya kuondoa umaskini kwa mikakati na siyo nadharia kwa kusisitiza mabadiliko katika sekta zote kuanzia kwenye afya, elimu hadi uchumi.

Mikakati ya wazi ya Dk. Magufuli ni kupunguza matumizi ya serikali na mashirika yake na kuimarisha utendaji na uwajibikaji.

Kukuza pato la serikali kwa kudhibiti ukwepaji na misamaha ya kodi holela na kuhakikisha nchi inawekeza katika sekta muhimu na inapata gawio halisia kutoka wawekezaji

Kukuza uchumi kwa sera na sheria endelevu ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji hasa katika sekta za madini, kilimo, viwanda, ufugaji na uvuvi na kuondoa kodi kwa wanyonge.

Kuimarisha huduma za umma kama elimu, afya, maji, makazi na mazingira; hili limeonekana tangu alipoingia madarakani.

Tumeshuhudia kwenye elimu ambayo sasa inagharimiwa na serikali kuanzia chekechea hadi kidato cha nne.
Tumeona pia wananchi wakihamasishwa kujiunga kwenye bima ya afya ili waweze kupata tiba kwa wakati pale wanapougua.

Kwenye ardhi tumeona akikabiliana kupambana na migogoro kati ya wakulima, wafugaji na wawekezaji wengine kwa kufuta hati za mashamba pori ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu, nia ikiwa ni kuwagawia wananchi.

Pia Wizara ya ardhi imeanza kuimarisha mfumo wa umiliki wa ardhi kwa Watanzania na kudhibiti migogoro kwa kupima ardhi yote ya Tanzania na kumilikisha vijiji na wakulima kwa hati za serikali ili kuipa thamani.

Tunakumbuka pia ahadi ya kuboresha bandari zilizopo ili kurejesha biashara tulizopoteza kwa bandari za nchi jirani; kujenga kilometa 4,000 za barabara, kujenga reli ya kati kwa viwango vya kisasa, kufufua shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida, kujenga miundombinu ya kisasa na kuondoa misongamano ya magari hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha; na kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini.

Kwenye viwanda serikali imelenga kuiimarisha sekta hiyo ili iwe mhimili wa uchumi kwa uzalishaji wa bidhaa na ajira endelevu na mikakati inayoendelea inaweza kuifikisha Tanzania kwenye kusindika malighafi zote zinasindikwa kabla ya kusafirishwa nje ili kuongeza mapato na ajira.

Wanawake na Vijana, wanapewa kipaumbele kuanzia kwenye fedha za mikopo zilizotengwa kwenye Halmashauri na zile milioni 50 zinazotengwa kwa kila kata.

Mabadiliko yote hayo yanategemea kwa kiasi kikubwa fedha na fikra za wananchi katika kuchangamkia fursa zinazotengenezwa na serikali. Ni kufikiri na kutenda tofauti. Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kama kwamba hatuna dharura ya maendeleo.

Ili kuyafikia ni lazima watendaji wanaomsaidia Rais Magufuli wabadilike kwenye kupanga na kubuni vyanzo, kutoka kutegemea soda, sigara na pombe; tuangalie vyanzo vingine zaidi.

Tunazo rasilimali nyingi na hususani ardhi, ikipimwa tunaweza kupata kodi ya ardhi ikaongeza mapato.

Ari na utendaji wa Dk. Magufuli inatulazimisha Watanzania wote kufanya mabadiliko na tujiamini kuwa sisi kama Taifa tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe bila kutegemea wafadhili. Hii si ndoto.

Nchi nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini, tujifunze kutoka kwao. Inabidi tuache kuukubali na kuvaa umaskini.
Mungu ibariki Tanzania.