Bajeti ya awamu ya tano tuone vyanzo vipya ?

19Mar 2017
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Bajeti ya awamu ya tano tuone vyanzo vipya ?

BUNGE la Bajeti linatarajiwa kuanza mkutano mwezi ujao likiwa na kazi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoidhinishiwa fedha kwenye bajeti ya mwaka 2016/17, kuangalia matumizi ya fedha za umma, pia kujadili na kupitisha bajeti ya serikali ya mwaka mpya wa fedha wa 2017/18.

Kila Wizara italielezea ilivyotekeleza miradi ya maendeleo kwenye fedha zilizotengwa na bajeti pamoja na majukumu mbalimbali ambayo yalijitokeza katika mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30.

Aidha, itaainisha changamoto na mipango ya kutekeleza bajeti mpya, inayoanza kutekelezwa Julai mosi mwaka huu. Imezoeleka kuwa miaka ya nyuma baadhi ya wizara hazipati fedha kama zilivyopitishwa bungeni na kusababisha utekelezaji wa miradi kuwa chini ya viwango, ama usifanyike kutokana na madai ya kukosa fedha au kupata pungufu.

Lakini cha kushangaza bajeti ambayo hupwaya ni ya miradi ya maendeleo tena cha kushangaza ndiyo ni pesa za eneo linalogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa sababu inashughulika na ujenzi wa miundombinu, usambazaji maji, kujenga shule na hospitali na kugharamia kazi za kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya Mtanzania.

Kikubwa kinachoelezwa ni ukosefu wa fedha au kutopelekwa kwa wakati, hali hiyo naweza kuifananisha kama kuwadhulumu wananchi hazi zao kwani kama walitakiwa kupata majisafi na salama wataendelea kuteseka na kuumia.

Kingine kinachojitokeza katika bajeti za serikali ni vyanzo kubakia vile vile kwa miongo yote kwa wengine wanasema sehemu kubwa ya fedha za bajeti inatokana na bidhaa za ‘anasa’ kwani inategemea pombe iwe kali au laini, sigara, vinywaji baridi, magari na mafuta.

Pengine ndiyo maana bajeti haileti unafuu kwani hivyo vyanzo haviwezi kuleta fedha za kuiwezesha nchi kutekeleza miradi ya maendeleo kikamilifu.

Katika bajeti ya mwaka jana hali ya kutegemea kodi za ‘anasa’ ilijiri na kilichoongezeka kwenye vyanzo vya mapato ni pamoja na kukata kodi kwenye viinua mgongo vya wabunge na viongozi wengine wa serikali baada ya kustaafu, iligusa pia miamala ya simu na huduma za kiutalii.

Si hivyo tu, serikali iliendelea kubana matumizi kwa kupunguza ama kufuta baadhi ya safari za nje zisizokuwa na tija, kuondoa sherehe na maadhimisho yanayomaliza fedha kwa kulipana posho na kununua vyakula na vinyaji.

Posho hizo zilikuwa mrija wa unyonyaji uliokausha hazina ya taifa. Ni wazi kuwa bado unahitajika ubunifu wa hali ya juu ikiwamo kurejea ripoti mbalimbali za wataalamu ambazo zimeelekeza vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaiwezesha serikali kupata kodi ya kusaidia kuondokana na utegemezi kwa wahisani na kukopa kunakoongeza ukubwa na mzigo wa deni la taifa.

Mathalani Bajeti ya Tanzania kila mwaka imekuwa tegemezi kwa wahisani ambao wakati mwingine huleta masharti magumu na kugoma kuendelea kusaidia utekelezaji wa bajeti licha ya kuahidi kuwa watatoa fedha kiasi fulani.

Ni lazima kuwepo ubunifu katika kupanga na kutekeleza bajeti ya nchi, kwa kuhakikisha inaondokana na utegemezi kwa kiasi kikubwa kwa kutumia vyanzo vya mapato vya ndani vitakavyosaidia kutunisha mfuko wa serikali.

Bajeti ya msingi na ambayo inamaana kwenye maisha ya Mtanzania wa kawaida ni ya maendeleo ambayo inajielekeza kwenye miradi ya maji, afya, elimu na miundombinu ambayo ina manufaa ya kwa wote.

Mtanzania wa kawaida anaposikia bajeti imepitishwa ni Shilingi trilioni 29.4 hawezi kuelewa maana ya namba hizo pasipo kuona manufaa ya moja kwa moja katika eneo analoishi.

Mathalani, alikuwa hana maji sasa anayapata, alitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya anazipata karibu na pia kila zahanati, kituo cha afya na hospitali anayoingia anapata wataalamu, vifaa tiba na dawa, siyo kuambiwa aende kumuona daktari na kutakiwa kujinunulia dawa hata kama alichangia mfuko wa afaya ya jamii.

Mtanzania huyo anataka kuona miundombinu ya barabara inayopitika kwa kipindi chote cha mwaka, anapotaka kusafirisha mazao yake analifikia soko, lakini ikiwa atatumia jasho kuzalisha na anapotaka kuuza anashindwa kulifikia soko kwa wakati na hata akipeleka mazao sokoni yameshaoza, haelewi mabilioni yanayotolewa kwenye bajeti.

Wabunge nao watimize wajibu wao wa msingi kwa mujibu wa muhimili huo kuwa ni kuisimamia serikali kikamilifu na siyo kuwa chini yake.

Kuna mihimili mitatu nchini nayo ni serikali, bunge na mahakama , kila mmoja una majukumu yake ya msingi ambayo hayatakiwi kuingiliwa na yeyote, inapotokea nguzo moja inashindwa kutekeleza kazi zake na kuendeshwa na nyingine upo uwezekano wa hatari kulinyemelea taifa.

Hivyo, lazima uwepo na uhuru wa utekelezaji wa majukumu kwa kila muhimili, inapofika katika Bunge kuisimamia serikali. Itikadi ziwekwe kando na kuwe na usimamizi wa uhakika kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha utekelezaji wa bajeti unakwenda kwa kadri ulivyopangwa na siyo vinginevyo.

Tutafakari!