BAKITA wanaridhia upotoshwaji huu?

14May 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
BAKITA wanaridhia upotoshwaji huu?

WATAKA kujua upotoshaji wa Kiswahili unaosemwa kuwa ni ‘Kiswahili cha kisasa?’ Soma magazeti ya michezo.

Wataka kuchafua lugha azizi (-a thamani) ya Kiswahili? Usipitwe na magazeti yetu ya michezo.

Wataka kujua mseto wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza (Kiswangereza)? Usipitwe na safu hii ya ‘Tujifunze Kiswahili’ kila Jumanne kwenye gazeti maarufu la Nipashe, Mwanga wa Jamii.

“Maneno hataki maneno mbofumbofu” ni kichwa cha habari kwenye moja ya magazeti yetu ya michezo. Nimejaribu kutafuta na kuuliza maana ya ‘mbofumbofu’ kutoka kwa watu mbalimbali nikapata jibu nisiloridhika nalo kwamba eti maana yake ni ‘mbovumbovu.’

Kama ndivyo, ingeandikwa: “Maneno hataki ubabaishaji” yaani maneno ya kudanganya.

“Mavituz ya Mane yampagawisha Fowler.” Kiswahili hakina neno ‘mavituz’ wala wingi wa vitu si ‘mavituz’ kama alivyoandika mwandishi wa gazeti la michezo. ‘Kitu’ ni umoja (kitu hiki) na ‘vitu’ ni wingi (vitu hivi). Hakuna ‘mavitu’ wala ‘mavituz.

‘Kitu’ ni chochote kinachoweza kubainishwa kwa kutumia milango ya fahamu: kuonekana, kushikika, kuonjwa n.k. Aidha jambo, mali au fedha; chochote ambacho si mtu wala mnyama. Pia ni mnyama mweusi wa jamii ya paka.

“Aliyewapa maujanja Simba aibukia AFCON” ni kichwa kingine cha habari kwenye gazeti la michezo. ‘Ujanja’ ni uwezo wa mtu wa kubuni mbinu za kufanya au kukwepa jambo kwa urahisi. Pia ni hali ya kuwa na hila, tabia ya kudanganya; ghiliba, akili, werevu. Neno hili halina wingi; hivyo ni kupotosha lugha isemwapo au iandikwapo ‘maujanja.’

“Madogo 10 AFCON usiwapime, wanakinukisha majuu buana.” Kichwa hiki cha habari hakieleweki ila kwa aliyekiandika! ‘Madogo’ latokana na ‘dogodogo’ yaani –sio na kiwango kikubwa: biashara ndogondogo yenye mtaji mdogo; viwanda vidogovidogo; –sio enye umuhimu mkubwa; mambo yasiyokuwa muhimu sana. Mambo madogomadogo.

‘Usiwapime’ ni kukataza kiumbe kupimwa kama vile kujua uzito, urefu au kuwachunguza damu ama choo. Pia kadiria au linganisha hoja ili kupata inayofaa. Hapa pia twapata neno ‘pimajoto’ yaani chombo chenye zebaki ndani ya kioo kinachotumiwa kupimia joto la mwili. Aidha ‘pimamaji’ ni chombo cha ujenzi au useremala chenye maji ndani ya kioo kitumikacho kupimia usawa wa kitu.

‘Kinukisha’ maana yake nini? ‘Nuka’ ni toa harufu mbaya, aghalabu kwa sababu ya kuoza. ‘Nukia’ ni toa harufi nzuri ya kupendeza kama ya marashi; firidi. Kitendo cha jambo kukaribia kutendeka au kutokea. ‘Nukisha’ ni kumfanya mtu anuse harufu nzuri au mbaya.

‘Majuu’ ni wapi? Ni nchi gani duniani yaitwa ‘majuu’? Eti kwa Kiswahili cha kihuni ‘majuu’ ni Ulaya! Kumbe kuna siku Tanzania itaitwa ‘Tanzia’ yaani taarifa ya kifo inayopelekwa mahali pengine! Kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Maana yake ukishangaa kutokana na miujiza ya Musa utashtuliwa na matendo ya Firauni.

Sielezi maana ya ‘buana,’ ‘bhana’ wala ‘bana’ kwani nimeeleza mara nyingi sana kwenye makala zangu lakini ni kama nawapigia mbuzi gitaa … hawachezi wala kujifunza ila kukodoa (toa macho pima, fumbua macho na kuyakaza sana)!

 “Abdi Banda mambo ni fire.” Ina maana mwandishi angeandika: “Abdi Banda mambo ni moto” isingeeleweka bila kuchanganya neno la Kiingereza (fire) lenye maana ya moto?  ‘lay a fire;’ (koka moto). ‘set on fire’ (choma moto, tia moto, unguza) na ‘catch fire’ (shika moto).

“Meneja wa Samatta kuwapa shavu wachezaji kibao.” ‘Shavu’ ni sehemu ya uso kati ya jicho na taya la mtu. Kiungo cha samaki atumiacho kuvutia hewa. Kichwa alichoandika mtangazaji maana yake ni kwamba meneja wa Samatta amewapa wachezaji wengi ‘shavu.’ Ina maana baadhi ya wachezaji hawakuwa na mashavu?

Kutokana na waandishi kutumia maneno ovyo na kuchanganya Kiingereza, baadhi yao wanashindwa hata kujua matumizi sahihi ya maneno ya Kiswahili! Soma hii: “Mwanamke auawa akitaka kubakwa.” Niliposoma kichwa hicho cha habari, nilishangaa kuwa mwanamke ameuawa ‘akitaka’ kubakwa!

‘Taka’ ni kitu kinachosababisha mahali pawe pachafu; uchafu. Kwa muktadha ninaoujadili, ‘taka’ ni kuwa na haja ya kitu au jambo fulani. Je, ni sahihi kuandika: “Mwanamke auawa akitaka kubakwa?” Kwa maana hiyo mwanamke huyo ‘alilazimisha abakwe’ lakini akauawa kwa kuwa aliowalazimisha wam-bake sio mabasha (wanaume wenye tabia ya kulawiti)? Ingeeleweka kama ingeandikwa: “Mwanamke auawa akikataa kubakwa.”

“DC awavaa wanaogushi vitambulisho.” Neno ‘vaa’ maana yake ni kufunika mwili kwa nguo; weka mapambo katika sehemu ya mwili: vaa ushanga, vaa pete, vaa mkufu, vaa saa n.k. ‘Vaa’ pia ni kibao kwenye chombo cha baharini kama dau, mashua ama jahazi kitumikacho kufungia nanga. DC ‘aliwavaaje’ binadamu wenzake?

Kiswahili hakina neno ‘gushi’ bali kuna ‘ghushi’ yaani kitendo cha kuchanganya kitu kilicho bora na duni; kitendo cha kudanganya kwa kuiga maandishi au saini ya mtu. Kwa hiyo hakuna ‘wanaogushi’ vitambulisho bali wapo wanaoghushi vitambulisho.

Methali: Eleza haja upate haja.

[email protected]

0784  334 096