Bandari Dar ni nyanya mbona haiachi kuoza!

03Dec 2017
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Bandari Dar ni nyanya mbona haiachi kuoza!

KAMA ilivyo ada ya Rais John Magufuli, hivi karibuni aliibuka ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kuwapo kwa magari madogo 50 ya kubebea wagonjwa yaliyokwama hapo kwa muda mrefu.

Kufuatia hali hiyo akatoa wito moja kwa Mamlaka za  Mapato  (TRA) na Usimamizi wa Bandari (TPA)  pamoja na Jeshi la Polisi kumpa taarifa juu ya sababu za magari hayo kukwama  kwa muda mrefu tena ni kinyume cha sheria.

 

“Nataka magari yote yaliyokaa muda mrefu kupita muda uliopangwa kisheria yaondolewe haraka, kama ni kupigwa mnada yauzwe, kama ni kufanywa mali ya umma yachukuliwe na serikali  na kwamba haiwezekani  kuendelea kutunza magari ya watu  kwa miaka 10 tena wengine hawajulikani," anaagiza Rais Magufuli.

 

Pia ametaka  magari yote ambayo yamekaa bandarini hapo kwa muda mrefu yaondolewe kwa kufuata utaratibu za kisheria na kwa uwazi akimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)  Valentino Mlowola, kuchunguza  magari yote yaliyokwama bandarini hapo baada ya kuagizwa kwa majina ya taasisi za serikali na kuwabaini wote walioshiriki katika uingizaji huo.

 

Siku chache baadaye, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ,  akafanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo naye akakuta madudu mengine kama ilivyokuwa kwa Rais Magufuli.

 

Madudu hayo aliyoshtukia Waziri Mkuu ni ya wajanja kutaka  kupitisha bure matrela 44 ya kubebea makontena bila kulipiwa kodi huku waliosuka mpango huo wakidaiwa kutumia jina la Waziri Mkuu.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, matrela hayo yaliingizwa nchini kutoka Uturuki na kwamba wahusika walijaribu kutumia jina la Waziri Mkuu kuyapitisha bure, hivyo kutaka kusababisha upotevu wa mapato na pia kutishia kuharibu ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Uturuki.

 

Imekuwa ni kawaida viongozi wakuu wa serikali kufanya ziara za kushtukiza za mara kwa mara bandarini hapo ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, lakini inaonekana bado kuna wajanja wachache ambao wanaendelea kufanya kazi kwa mazoea.

 

Kwa sasa serikali imefunga kamera zaidi ya 400 zenye uwezo wa kuonyesha matukio yote yanayotokea nje na ndani ya bandari hiyo na hasa katika eneo la kupakulia mafuta.

 

Hatua hii ya serikali ya kufunga kamera na pia viongozi wake kufanya ziara za mara kwa mara ingetosha kuwashtua wale wanaofanya kazi kwa mazoea na kufuata taratibu ili kuepuka kuingia kwenye matatizo.

 

Miaka ya nyuma baadhi ya watumiaji wa bandari hiyo walikuwa wakiilalamikia kutokana na matukio mbalimbali yakiwamo ya upoteaji wa mali zao, lakini tangu serikali ya awamu ya tatu ianze kazi kumekuwa na mabadiliko makubwa.

 

Ninaamini kwamba kama wahusika wangesoma alama  za nyakati kwamba hii ni serikali nyingine wasingeendeleza madudu ambayo wamebambwa nayo na kujikuta kwenye matatizo.

 

Umefika wakati sasa watambue kuwa mtindo wa kuishi kiujanjaunja hauna nafasi kwenye serikali hii na badala yake wahusika wafuate utaratibu kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria na uwazi kama alivyosema Rais Magufuli.

 

Mwanzoni mwa uongozi wake  Rais Magufuli alifanya ziara zaidi ya mbili za kushtukiza katika ofisi na wizara mbalimbali za serikali kwani mara kuapishwa, asubuhi yake alifanya ziara ya ghafla Wizara ya Fedha na kujionea hali halisi, haikuishia hapo tena Hospitali ya Taifa Muhimbili na kukuta changamoto  za ukosefu vitanda vya wagonjwa na dawa.

 

Rais amekuwa akifanya ziara za aina hiyo maeneo mbalimbali na hasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, sehemu ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikidaiwa kuwa kichaka cha wajanja wachache kujinufaisha kwa kujitajirisha  kupitia miundombinu ya bandari.

 

Ziara hizi za ghafla zilipaswa kuwa somo kwa wale walizoea kuendekeza madudu na kutambua kuwa serikali hii haina mchezo na hailei 'wapigaji madili’ bali inataka kila jambo litendeke kwa haki.

 

Niseme tu kwamba enyi wa bandarini someni ishara za nyakati, acheni kuendekeza mtindo wa kuishi kiujanjaujanja, kwa sababu hamjui siku wala saa ambayo viongozi wa serikali watafanya ziara za kushtukiza.

 

Rais alishasema kuwa kasi yake siyo ya nguvu ya soda, kwa hiyo mkidhani kwamba kuna wakati itapungua mtajikuta mnanaswa kila mara kama ambavyo imekuwa ikitokea anapowazukia hapo bandarini.