Barabara hii jijini Mwanza ni kero na hatari kubwa

07Nov 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Barabara hii jijini Mwanza ni kero na hatari kubwa

KWANZA kila mtu anajua pasipo ubishi, kwamba Mwanza ni jiji kubwa na kuna uwezekano mkubwa juu ya ukweli huo.

Hapa jijini Mwanza kuna mlolongo katika barabara zake. Katika Barabara ya Kiloleli, hadi sasa kunakabiliwa na mateso kwa wavukaji kutokana na kasi kubwa ya magari na bodaboda zinazokatiza mahali hapo.

Awali, kabla ya kuwekwa lami kwenye barabara hiyo, magari na bodaboda zilipita katika mwendo wa kawaida na daima hazikuwa na kasi inayoshuhudiwa leo.

Lakini, baada ya kuwapo mabadiliko, barabara hiyo haijawekwa lami na haikuwa na mwendokasi unaoshuhudiwa hivi sasa.

Ikumbukwe, ni barabara yenye kona nyingi, hali inayowafanya hata wavukaji kwa miguu, kukumbana na changamoto nyingi wakati wa kutafuta huduma mahali hapo, inayowalazimu kuvuka barabara.

Ni kawaida, kila kukicha tunashuhudia katika barabara hiyo kuwapo daladala barabarani zinazopakia abiria na kushusha, wakati pembezoni kuna mitaro.

Kutokana na kuwapo kona nyingi barabarani, ni hali inayosababisha hatari kwa wavukaji wanaojikuta wakikimbia ovyo, kuepuka, wasigongwe na magari.

Tukiwarejea wanafunzi wa shule za msingi wanaosoma Kiloleni na watu watokao katika nyumba za ibada, nao wakiwa katika makundi au mmoja mmoja wanakuwa katika mtihani mkubwa, wakati wa kuvuka.

Ni mtihani kwa wavukaji, watoto kwa watu wazima wanaolazimika kukimbia sana kuelekea upande wa pili.
Pia, kuna kundi la watu maalumu wanaopata shida kuvuka barabara hiyo.

Niseme maeneo ya Barabara ya Kiloleni, kuanzia eneo la Kona ya Bwiru hadi kufika Njia Panda Msikiti wa Kiloleni, kunatakiwa kutafutiwe ufumbuzi wa usalama barabarani, kuwawezesha watu wavuke mahali hapo salama na daima wasikimbie ovyo.

Hata kwa wasio na matatizo na viungo mwilini, bado imekuwa tabia ya kawaida, bado uvukaji kwao huendana na kusikiliza milio ya magari na wakijiridhisha hawapo, wanatoka mbio kuelekea upande mwingine.

Watu wazima wasio na matatizo, wanalalamika kila siku kazi yao imekuwa mchezo wa kukimbia kuelekea upande mwingine, wakihofia kugongwa.

Ndipo napatwa na maswali mengine yanayonijia pasipo majibu, kwa wale wenye kasoro za miili yao, jamii ya walemavu na wazee ni makundi yasiyoweza kukimbia katika kuelekea upande wa pili, wanapataje msaada?

Tikija kwa madereva wa bodaboda, nao ni kama vile utamaduni kwamba katika barabara hizo wanakimbiza pikipiki na wakizifanyia mbwembwe kama vile zinataka kuanguka. Hapo nashuhudia madereva hao hawana kofia na kawaida kuwaona wako ‘mishikaki.’

Ni kweli tunapenda maendeleo, lakini hili la barabara pamoja na uzuri wake wa lami, inatakiwa mamlaka husika kuweka vizuizi ambavyo vitasaidia watumiaji barabara hiyo kuvukwa kwa utaratibu unaofaa, ili kuwapunguzia adha ya hatari kukimbia ovyo.

Katika barabara ya Kiloleli, kuanzia kona ya Bwiru kuelekea njiapanda eneo la Kilielli, kuna kona mpaka liliko eneo la Kiloleli Msikitini, ambako hakuna matuta.

Maeneo ya Montessori, Kiloleni Shule ya Msingi, Matofali na Maduka Tisa, nashauri kwa sasa kinachotakiwa kufanyika, ni kuwapa utaratibu mbadala utakaowawezesha watu kuvuka kwa usalama zaidi.