Barabara mijini zifagiliwe usiku kupunguza adha kwa watumiaji

26May 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Barabara mijini zifagiliwe usiku kupunguza adha kwa watumiaji

KWA miji mikubwa nchini ufagiaji wa barabara kubwa na za mitaa mbalimbali ni jambo muhimu na halikwepeki au kuahirishika.

Tumekuwa tukishuhudia ufagiaji mara nyingi ukifanyika majira ya asubuhi hadi mchana.wakati shughuli nyingi zikiendelea.

Miji mikubwa nchini ikiwamo Arusha, Mbeya, Tanga, Mwanza na Dar es Salaam mwenendo huo umekuwa ukifanyika.
Mkazi yeyote jijini Dar es Salaam mara nyingi atashuhudia wafagiaji wa barabara wanafanya usafi huku wengi wao wakikumbana na changamoto lukuki.

Kimsingi, iwapo ufagiaji wa barabara hizi hasa kubwa, ungefanyika majira ya usiku ni kwamba ingewapunguzia adha wafagiaji na watumiaji wengineo wa barabara.

Kwa nchi zilizoendelea licha ya kutumia magari maalum ya kufagilia, kudeki shughuli hii hufanyika majira ya usiku, ili kupunguza ama kuondoa usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.

Barabara ni moja ya miundombinu muhimu kwa ajili ya kusafirisha watu na mizigo au bidhaa zao kwa ajili ya kurahisisha matumizi yao.

Kwa Jiji la Dar es Salaam majira ya asubuhi hadi jioni, barabara huwa na purukushani za hapa na pale.

Baadhi ya wafagiaji jijini hukumbwa na mengi, ikiwamo kukoswakoswa na magari, bodaboda, kudhalilishwa kwa maneno kutoka kwa watu wasio wastaarabu na wengineo kuchafua barabara wakati mfagiaji anashuhudia ikiwamo kutupa chupa tupu za maji, juisi, karatasi iliyokwanguliwa vocha na hata mifuko ya plasitiki.

Wafagiaji hao hukumbana na kusanyiko la mchanga pembezoni mwa barabara, kutokana na mazingira ya jijini kuwa ni ya ukanda wa bahari.

Ili kuwafanya watekeleze majukumu yao vyema, wanahitaji vifaa maalum kama vile fyagio ngumu, mabuti, vifunika pua, matoroli na koleo imara zitazohimili uzito wa shughuli yenyewe.

Kwa mujibu wa wataalamu, wafagiaji hawa wana changamoto kubwa ya uwezekano wa kupata maradhi mbalimbali kama vile Kifua Kikuu (TB), nimonia, mafua na mengineyo yanayotishia usalama wa afya zao.

Baadhi yao huambukizwa maradhi haya kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya kuwakinga na vumbi (mask) kwa kuzivaa puani pamoja na glavu za mikononi, kofia na mabuti.

Kinachotokea ni wafagiaji hawa wengi wao, hasa akinamama wanatumia mbinu mbadala ya kujifunika kichwa, pua kwa kutumia mitandio au kanga.

Ifike wakati wafagiaji hawa waboreshewe mazingira wanayofanyia kazi, kwa kupatiwa vifaa maalum vya kuwakinga na jamii kutambua umuhimu wao.

Madereva wa vyombo vya moto wawe makini wanapoona ishara ya kutambulisha kuwa kuna kazi ya kufanya usafi inaendelea. Wafagiaji hao huweka alama ya barabarani na kuvaa makoti yanayoakisi mwanga ili kumrahisishia dereva kumuona kwa haraka.

Wakati hayo yakiendelea kufanyika, ni muhimu kuwa na utaratibu maalum wa kuhakikisha kuwa barabara hizi zinafagiliwa majira ya usiku yaani kuanzia saa nne usiku na kuendelea.

Pia barabara hizi ziwe na taa ili kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo kwa ufanisi pamoja na usalama wa wafagiaji hawa.

Pia, kwa usalama zaidi wafagiaji hawa wanaweza kujigawa katika makundi kwa maeneo ya jirani, kuliko kumuacha mfagiaji mmoja katika umbali wa mita kadhaa hasa katika maeneo yaliyoshamiri vitendo vya kuhatarisha maisha ni muhimu wakapewa ulinzi.

Utaratibu huu utaondoa adha ya watumiaji barabara wegine majira ya asubuhi na mchana pia itawapunguzia vikwazo na changamoto wafagiaji hao ambao mara nyingine husababisha foleni, kutokana na madereva kulazimika kutumia barabara upande mmoja wakati upande mwingine ukifagiliwa.