Barabara zilizoharibika kwa mvua zikarabatiwe

02Feb 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Barabara zilizoharibika kwa mvua zikarabatiwe

KWA muda mrefu sasa tangu baadhi ya maeneo au vipande vya barabara baadhi havizidi hata mita 200 kuchakaa kwa kuibuka mashimo lakini bila kukarabatiwa.

Miongoni mwa maeneo hayo ni Magengeni, jirani na hospitali ya Mwananyamala na Makumbusho jijini Dar es Salaam. Yameharibika kiasi ambacho hata gari la wagonjwa likiwa limebeba mgonjwa ili kumuwahisha hospitali hospitali hiyo ama ile ya Taifa Muhimbili, anaweza kuzidiwa zaidi.
Uchakavu wa barabara za baadhi ya maeneo jijini ni suala linalohitaji kuangalia zaidi kwa kufanyiwa ukarabati na si kusubiri bajeti kubwa ya serikali inayotarajiwa kupangwa mwezi Juni mwaka huu.
Kama barabara ilikuwa ni ya kiwango cha lami ,ikiharibika mashimo yake huwa ni mabaya zaidi na yanayosumbua zaidi kuliko hata barabara iliyokuwa ya vumbi.
Barabara ambazo zimeharibika kutokana na mvua za msimu ama kutokana na ujenzi wa kiwango cha chini zikarabatiwe angalau hata kwa kukwanguliwa ili kuzifanya zipitike kwa urahisi.
Uchakavu wa barabara hizi, unapunguza hadhi ya jiji kwani haiendani na mandhari ya majiji mengi yanavyokuwa ama yanavyotakiwa kuwa.
Pia barabara za pembezoni ambazo ni mbovu na chakavu zikarabatiwe kwani husaidia kupunguza foleni katika barabara kuu kwa kupunguza baadhi ya magari yanapita huko.
Mara nyingi jijini Dar es Salaam ,baada ya mvua au mvua inaponyesha unakuwepo msongamano mkubwa wa magari.
Baadhi ya watumiaji wa barabara jijini, husema kuwa sababu ni magari mengi kukwepa barabara za pembezoni ambazo mara nyingi hujaa maji, matope na kumfanya dereva kuwa na wasiwasi na usalama wa gari lake.
Barabara za pembezoni zinazohitaji ukarabati ni nyingi ili kuendana na hadhi ya mradi mpya wa mabasi yaendayo haraka Dart.
Mifereji ya maji machafu, iliyoziba taka ngumu katika barabara za pembezoni zimekuwa ni chanzo kwa baadhi ya wakazi kushawishika kutupa uchafu na kuongeza tatizo mvua ikinyesha.
Usafiri mpya wa Dart, ukianza kutumiwa na watu wengi, itakuwa ni msaada kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.
Halmashauri za manispaa jijini Dar es Salaam, zianze kuzikarabati barabara hizo, kwani mvua zinazoendelea kunyesha zimesababaisha kuharibika kwa baadhi ya barabara.
Yamekuwepo malalamiko ya muda mrefu kuhusu barabara za wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam,kwa kuwa na barabara mbovu zinazopitika kwa matatizo .

Kwa mfano barabara ya kuelekea Polisi Mabatini na ile ya Akachube ya Kijitonyama, Biafra zimekuwa ni korofi kama ilivyo katika barabara nyingine ambazo sio rahisi kuzitaja zote.
Barabara hizo, baada ya ujenzi kukamilika ndani ya muda mfupi zilianza kubomoka kwa kasi kuanzia muda wa miezi mitatu hadi miezi sita.

Wakati hayo yakitokea baadhi ya barabara katika mitaa tofauti jijini zimeanza kujengwa kwa kuwekwa zege ili kuziongezea uimara .

Maeneo hayo ni yale ambayo ni korofi kama vile barabara ya Kairuki, na barabara nyingine iliyopo Mikocheni ili kukabiliana na tatizo hilo.

Kwa sasa ifike mahali barabara zikarabatiwe ili kuendana na hadhi ya jiji.