Bei ya dhamana za serikali za muda mfupi

04Mar 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Bei ya dhamana za serikali za muda mfupi

Tunaendelea tena wapenzi wasomaji wa safu hii ya ‘Mtazamo wa Kibiashara’ na mada inayohusu uwekezaji kwenye hati fungani au dhamana za serikali kwa lugha nyingine.

Na kama tulivyoona huko nyuma kuwa, tunapoongelea dhamana za serikali, tunakuwa tukirejea dhamana za serikali za muda mfupi (Treasury Bills) ambazo huiva kuanzia siku 35, 91, 182 hadi siku 364.

Lakini pia dhamana za serikali za muda mrefu (Treasury Bonds), ambazo huiva kuanzia miaka miwili, mitano, saba, 10 na miaka 15.

Aidha, tuliona pia kwamba soko la dhamana hizo huendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia Kurugenzi yake ya Masoko ya Fedha, ambayo huendesha minada ya dhamana za serikali.

Kwa mfanyabiashara yeyote, awe wa kawaida au ngazi ya chini, wa kati na hata yule mkubwa, anaweza akashiriki kwenye minada hii ili mradi ana kiasi cha fedha kinachoruhusiwa kuwa nacho ili aweze kushiriki.

Na kama tulivyosema vile vile katika moja ya matoleo ya safu hii kwamba, kwa dhamana za serikali za muda mfupi, kiwango cha chini anachoruhusiwa mfanyabiashara au mtu mwingine kuwa nacho ili ashiriki ni shilingi 500,000, na kuendelea.

Na kwa upande wa dhamana za serikali za muda mrefu, kiwango cha chini cha fedha kinachoruhusiwa kuwa nacho ili mfanyabiashara ashiriki kwenye minada ya serikali ni Sh. millioni na kuendelea.

Tukaona vilevile kuwa, BoT ina mfumo ambao hufanya mchakato wa minada ya dhamana za serikali ujulikanao kama Central Depository System (CDS), lakini pia ina mawakala maalumu (Central Depository Participants).

Hawa ni mawakala maalumu ambao wameidhinishwa na BoT kushiriki kwenye minada hiyo ya serikali moja kwa moja. Kwa niaba yao, pia na kwa niaba ya wateja wengine.

Aidha, tukaangalia mawakala hao wametapakaa katika mikoa yote nchini na kwamba kwa mfanyabiashara yeyote ambaye hayuko jirani na benki kuu na anataka kuwekeza kwa kununua dhamana za serikali, anapaswa kuwasiliana nao.

Sasa tukiendelea kutokea hapa, ni kuwa, benki kuu hutoa tangazo la mnada kila siku ya Ijumaa kupitia vyombo vya habari, kwenye baadhi ya magazeti na televisheni.

Anachotakiwa kufanya mfanyabiashara au mwekezaji kwa maana hii, baada ya tangazo kutolewa, ni kujaza fomu maalum za zabuni kupitia kwa mawakala wao.

Mawakala hawa hujaza maelezo ya zabuni husika kwenye mfumo ule wa benki nilioueleza hapo juu, yaani Central Depository System (CDS), mfumo ambao unafanya mchakato wa minada ya dhamana za serikali.
Baada ya mawakala kujaza maelezo ya zabuni kwenye mfumo huo wa CDS, huziwasilisha fomu hizo BoT kiteknolojia ama kimtandao.

Bei ya dhamana za serikali za muda mfupi huuzwa kwa punguzo kwa kila shilingi 100.
Hiyo ina maana kuwa, kwa mfanyabiashara ambaye ana kiwango cha chini kinachoruhusiwa kushiriki kwenye uwekezaji wa dhamana za muda mfupi, yaani Sh. 500,000, atapata dhamana 5,000.

Hii ni kutokana na mahesabu, kwamba kwenye Sh. 500,000 ukigawa kwa bei ya shilingi 100 inayonunua dhamana za serikali, utapata dhamana 5,000.

TUKUTANE IJUMAA IJAO KWA UFAFANUZI ZAIDI