Biashara Machinga ni sawa, lakini si katika mazingira haya

16Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Biashara Machinga ni sawa, lakini si katika mazingira haya

JUHUDI mbalimbali zimekuwa zikifanyika kwa ajili ya kuwawekea wamachinga mpangilio mzuri wa kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi, wakati maeneo yao yakiandaliwa, lakini utekelezaji wake umekuwa ukikwama.

Unakwama kutokana na baadhi yao kuhama na kwenda kando ya barabara, hali ambayo ni hatari kwa usalama wao kwa kuwa  ajali za magari zikitokea zinaweza kuwakumba.

Hivyo kumekuwapo na wimbi la kuzagaa wamachinga maeneo mbalimbali mitaani na kuendesha biashara zao, wakiwamo hao wanaopanga kando ya barabara, hali ambayo ni hatari kwa usalama wao.

Hilo linatokana na ajali za magari zinapotokea, ni rahisi kwao kugongwa au biashara kuathiriwa, kwa kuwa mazingira kama hayo ya kupanga biashara maeneo hayo ni rahisi kufikiwa.

Kutokana na hali hiyo, sasa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, linawataka kuacha kufanya biashara ndani ya barabara kwa ajili ya usalama wao na mali zao.

Binafsi ninaamini kwamba uamuzi huo ni mzuri na wenye lengo la kuokoa maisha ya wafanyabiashara hao, kwani mazingira wanayofanyia shughuli zao si salama na pia si vyema kusubiri majanga yatokee ndipo kitafute ufumbuzi.

Mratibu wa Polisi Makao Makuu Kikosi cha Usalama Barabarani, Mosi Ndozero, anasema, machinga wamekuwa wakihatarisha maisha yao kwa kufanya biashara barabarani.

Anachosema ni ukweli mtupu, kwani wapo wanaopanga biashara zao kandokando ya barabara kuanzia asubuhi hadi usiku na wengine waliopo sokoni, huwafuata wenzao wa barabarani wakati wa jioni.

Badala ya kufanyia biashara sokoni, barabara zinageuzwa kuwa masoko, hivyo bahati mbaya ikitokea ajali, ni rahisi watu wengi kukumbwa, hivyo suala la wamachinga kuondoka kwenye maeneo hayo nadhani lina umuhimu wake.

Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kinasema kimekuwa kikitoa elimu kwa wamachinga kuhusu haki, wajibu na madhara ya kufanya biashara hizo kwenye mazingira hayo, kwa nini hali bado?

Rai hiyo kwa wafanyabiashara hao ya kutofanya biashara kandokando ya barabara, ingefaa kuchukuliwa kwa uzito wake na wahusika kwa lengo la usalama wao na wa wateja wake.

Mbali na kuhatarisha maisha yao kwa kupanga biashara kandokando ya barabara, wamachinga pia wamekuwa wakisababisha kero kwa 'kuvamia' njia za waenda kwa miguu na kupanga biashara zao.

Kwa kauli hiyo ya Kikosi cha Usalama Barabarani, ingekuwa ni vyema sasa kila mdau kushiriki ili kuhakikisha wamachinga wanafanya biashara zao katika mazingira rafiki kuliko ilivyo sasa.

Ingawa wamachinga wanatakiwa kufanya biashara kusumbuliwa katika maeneo waliopo, baadhi yao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo vibaya kwa kusogea hadi kandokando ya barabara na kupanga bidhaa zao.

Wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wa mikoa hawana kuchukulia kwa uzito kauli ya kikosi hicho kwa ajili ya usalama wa wafanyabiashara hao, kwani usalama ni muhimu zaidi.

Viongozi hao walishaelekezwa kuwatengea masoko kwa ajili ya wamachinga ili waondokane na mazingira hayo, lakini hilo ni kama halijatekezwa, hivyo wanapotakiwa kutoka barabarani, viongozi wajitokeze na kutenga masoko.

Jukumu la kutenga masoko kwa ajili ya wamachinga ni lao na hawawezi kulikwepa, hivyo ni vibaya kujitokeza na kulipatia ufumbuzi wa kudumu sakata la kuzagaa ovyo kwa wamachinga mitaani.

Ni hivi karibuni, Watanzania wameambiwa kuwa wamachinga wameingiza serikalini Sh. bilioni 46.71 zilizotokana na vitambulisho vya ujasirimali vilivyotolewa na serikali mwaka 2018.

Kwa mantiki hiyo, wana umuhimu katika maendeleo ya taifa, kwa kuwa ni miongoni mwa walipa kodi, hivyo suala la kuwatengea masoko rasmi na kuwahimiza kufuata sheria ni la muhimu.

Hadi Kikosi cha Usalama Barabarani kufikia kuwaambia wasifanyie biashara barabarani, ni wazi kwamba sasa inatosha ili wasije kukumbwa na ajali za magari kikosi hicho kikaonekana hakifanyi kazi.