Bila kuukataa tutarajie kuwa na kizazi cha ovyo

25Nov 2018
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Bila kuukataa tutarajie kuwa na kizazi cha ovyo

VITENDO vya ushoga ni moja ya changamoto kubwa ambayo inaelezwa kuwa imeota mizizi ndani ya jamii na inachangiwa na mmomonyoko wa maadili na mienendo mibaya wakati inayowahusisha, wazazi, shule, vyuo, jamii na hata mitandao ya kigeni.

Tupende tusipende ushoga hauvumiliki na hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema Tanzania ni hekalu la Roho Mtakatifu haiwezi kuukubali ushoga na kuwaonya wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja.

Anasema sheria inakataza watu wa jinsi moja kufanya mapenzi kinyume cha maumbile na pia inaharamisha wanaume kufanya vitendo vya kujamiiana kinyume na kwamba serikali imekuwa ikipambana kwa nguvu zote na makundi hayo yanayoshiriki katika vitendo vya mapenzi ya jinsi moja, wakihamasisha ama kuhalalisha au kufanya yaonekane kama kitu cha kawaida.

Anakitaja kifungo chake kuwa ni zaidi ya miaka 30 jela, pia anaahidi kuendelea kupambana vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na kwamba, mwanamume atakayethibitika kufanya ushoga ataadhibiwa kisheria.

Waziri huyo alikuwa akizungumzia moto uliowashwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda, kuhusu vita dhidi ya ushoga mkoani mwake ambao kwa wiki kadhaa uliibua mijadala mingi.

Ninaamini kwamba kila mkazi wa Dar es Salaam akishiriki katika vita hii, ushoga unaweza kupungua kama siyo kuisha, mwaka juzi Makonda, alitangaza vita dhidi ya ushoga, lakini akajikuta akipigwa vita na baadhi ya watu kana kwamba vitendo hivyo ni halali. Katika maandiko matakatifu, ushoga unakatazwa tena ni kinyuma na maadili.

Japo mambo haya yanadaiwa kufanywa kuanzia kwenye familia, shuleni na maeneo mengine, hivyo kila mmoja anatakiwa kuhakikisha anahusika katika kupambana navyo.

Kwa wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam wasimwachie Makonda peke yake bali wasaidie katika malezi mema ya watoto ili wasijihusishe na vitendo hivyo, ambavyo ni kinyume na maadili mema ya Kitanzania. Zama hizi za utandawazi zimekuja na mambo mengi yakiwamo mazuri na mabaya, kwa hiyo ni vyema Watanzania wakachukua mazuri na kuacha mabaya ili kuepuka kujiingiza katika vitendo visivyofaa katika jamii.

Kupitia utandawazi, wapo wale wanaotaka kuwa huru kwa kufanya hata vitendo vichafu kama hivyo vya ushoga, lakini ninaamini kwamba uhuru huwa una mipaka. Kuwapo kwa vitendo vya ushoga ni kuvuka mipaka, kwani Tanzania hakuna ndoa ya jinsi moja bali mbili, yaani mke na mume, lakini sasa wamejitokeza watu wanaohalalisha ndoa ya jinsi moja.

Vitendo vya ushoga visipodhibitiwa taifa linaandaa kizazi cha ovyo cha baadaye kisichokuwa na maadili mema, kwa hiyo vita ya ushoga isiwe ya mtu mmoja au watu wachache bali wote washiriki .Katika kupigana na vitendo vya ushoga, wazazi wamekuwa wakielekezwa kutoruhusu watoto wao wa kiume kulala chumba kimoja na mgeni wa kiume ikiwa ni njia mojawapo na kuhakikisha wanakuwa salama.

Hii inatokana na ukweli kwamba kwa sasa kuna tatizo kubwa la malezi ambapo inadaiwa kuwa baadhi ya mashoga walifundishwa na ndugu, jamaa, marafiki, wafanyakazi wa kiume nyumbani kwao au wageni waliokuwa wakifadhiliwa na familia husika.

Wapo pia baadhi yao ambao mwanzoni walikuwa watoto wema, lakini kutokana na tamaa ya kutaka maisha mazuri wakarubuniwa na watu wenye pesa na kujikuta wameshajiingiza katika tatizo hilo la ushoga, lakini pia kuna wengine waliolazimishwa tena kwa kutumia silaha, ama kufanyiwa uovu huo na ndugu zao tena wanaowategemea lakini kwa sababu hawana maadili wakawaingiza kwenye uharibifu na sasa ni waathirika.