Bodaboda vipi mnazidi kulikaribisha hata hili?

18Jan 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Bodaboda vipi mnazidi kulikaribisha hata hili?

USAFIRI wa bodaboda una sifa kuu mbili. Moja, ni wa haraka, lakini upande wa pili ni kinyume chake, una hatari kubwa.

Wakati suala la haraka linaangukia katika kasi muundo wa vyombo vyenyewe vilivyo, hatari inaangukia kwa kiasi kikubwa tabia na mwenendo wa waendeshaji usafiri huo wa kukodi. Kila mmoja ana la kwake kueleza kuhusu walakini huo wa madhara, lakini inaangukia majumuisho maneno ‘mbaya’ na ‘hatari.’

Pia, imeshakaririwa na jamii kuhusu tabia ya bodaboda kuvunja sheria za usalama barabarani, kwa makusudi, wanalijua wazi ni kosa.

Nianze na hili linalonikera katika njia za mabasi ya mwendokasi, jijini Dar es Salaam, ambako kuna alama za pundamilia, mwendesha bodaboda akiwa na abiria anatakiwa kumshusha ili avuke na abiria kwa miguu na baada ya hapo, anapanda bodaboda upande wa pili, kuendelea na safari.

Kinachoshangaza ni pamoja na kuwapo katazo hilo, bado madereva wa bodaboda wanapita mahali hapo wakiwa wamebeba abiria.

Nadhani, ni vyema tukajiuliza, mwendesha bodaboda anakuwa hajui sheria yenye katazo au ameamua kupuuzia.

Naenda mbali, abiria je? Naye hajui hilo katazo au amepuuzia? Hilo ni katazo la kutiliwa maanani, kwani ni mazingira ambayo yanaweza hata kuzalisha umauti.

Inatakiwa, abiria na madereva, nyote kwa pamoja mfuate sheria ili kuepuka changamoto za ajali na sheria inayoweza kutokea .

Tukija katika hilo la bodaboda kubeba abiria ‘mshikaki’na kupita barabarani kabla taa hazijaruhusiwa, ni hatari nyingine.

Kumbe, kuna tabia ya baadhi ya madereva ambao hawaangalii taa na wanavuka bila ya kuruhusiwa. Hiyo ni hatari ya kukaribisha chochote kutokea na kuishia katika dhahama ya ajali.

Inatakiwa abiria na madereva wa bodaboda wazingatie sheria za usalama barabarani, kadri inavyowezekana, kwani ni wajibu wao wa msingi.

Tumekuwa tukishuhudia katika ajali nyingi, watu wanapoteza maisha au kuangukia ulemavu wa kudumu. Hayo yote ni matokeo ya uvunjifu wa sheria za barabarani.

Inatakiwa sheria zifuatwe, kwani kama hazitafuatwa, tutarajie ajali nyingi zaidi katika maisha yetu.

Tumekuwa tukiambiwa ajali inapotokea, kuwahudumia majeruhi ni changamoto.
Inaelezwa kwamba, uhudumiaji majeruhi, unaigharimu serikali pesa nyingi, huku akiba kubwa ya damu nayo inaagukia huko.

Ili kulipunguzia taifa matumizi makubwa ya dawa, kunatakiwa kuwepo sheria zinazozingatiwa na kama kuna watakaoipuuzia, inakuwa suala la kujitakia.

Sote tunajua vyema, kila ajali zinapotokea, kuna athari kubwa kwa familia ambazo mtu wake amepata ajali.

Mtu aliyekuwa anajitegemea, anarudi tena katika zama za utegemezi,yatima wanaongezeka na kadhalika. Ni maisha mapya