Bodi ya Utalii nchini ipanue wigo zaidi wa kujitangaza

22May 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Mjadala
Bodi ya Utalii nchini ipanue wigo zaidi wa kujitangaza

ZIPO jitihada mbalimbali za kutangaza vivutio vya utalii kitaifa na kimataifa, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalii na hivyo mapato yatokanayo na sekta hiyo.

Utalii ni sekta ya kwanza nchini kuchangia pato la taifa kutokana na hifadhi za taifa, mapori ya akiba, maeneo yaliyohifadhiwa, utalii wa maeneo ya historia na wa asili.

Jitihada za kutangaza utalii zimefanyika ikiwamo kushiriki kwenye maonyesho ya kidunia, ambayo huleta pamoja watu kutoka maeneo tofauti duniani ambapo Tanzania hupata nafasi nzuri katika ramani ya dunia vivutio vyake kuzidi kufahamika.

Kutokana na jitihada hizo, Tanzania ilipokea hivi karibuni watalii zaidi ya 1,000 kutoka Israeli na wengine 300 kutoka China.

Kimsingi, utangazaji upo wa namna nyingi, mathalani kupitia mashirika makubwa ya ndege, treni za miji na majiji mbalimbali, mitandao ya kijamii, tovuti, majarida makubwa na yanayosomwa na watu wengi.

Pamoja na hatua hizo, Mjadala unaona kwamba jitihada hizo zinapaswa pia kufanywa kwenye soko la ndani kwa maana ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

ATCL inapaswa kuwa na majarida yenye kuelezea utalii Tanzania, ili abiria anapopanda ndege hizi, iwe kwa safari yaa ndani au nje ayasome na hivyo kuvutika kutumia fedha zake kwenye utalii.

Hivi karibuni, nilipanda ndege ya ATCL kwenda na kurudi jijini Dodoma. Miongoni mwa abiria walikuwa ni raia wa kigeni ambao wamekuja nchini kwa shughuli mbalimbali za uwekezaji, lakini pia kuonana na viongozi wakuu jijini humo.

Ndani ya ndege hiyo kulikuwa na majarida lakini sikuona jarida lolote linaloelezea vivutio vya utali vilivyopo nchini.

Badala yake kulikuwa na majarida ya bidhaa na vitu vingine ambavyo ni muhimu, lakini ingependeza zaidi kama yangekuwapo pia ya kutangaza vivutio vya utalii.

Vilevile, nilitumia usafiri wa Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish) katika moja ya safari zangu ambapo kulikuwa na jarida la Skylife, ambalo zaidi ya kurasa nane ndani yake zilikuwa zinatangaza utalii wa Kenya.

Katika jarida hilo kuna maelezo juu ya uhamaji wa wanyama kwenda Maasai Mara wakishawishi watalii kuitembelea hifadhi hiyo.

Kwamba watembelee ili waone uhamaji wa makundi makubwa ya nyumbu, lakini pia wanyama wakubwa watano wanaopatikana hapo.

Katika habari hiyo yenye kichwa ‘Masai Mara: The Home of safari, kuna picha mbalimbali za makundi ya nyumbu yakikatiza mto Mara na ushiriki wa jamii ya Masai kwenye utalii wa asili, huku kukiwa na picha ya mtoto wa Kizungu akifundishwa kuwinda na kijana wa Kimasai.

 Jarida hilo huandikwa kwa lugha mbili za Kiingereza na Kituruki, lengo likiwa kuwafikia watu wengi zaidi wanaozungumza lugha hizo.

Pia nilitembelea Jiji la Geneva, Switzerland. Huko nako Kenya inajitangaza vyema na zaidi ikibainisha kwamba kwamba ukitembelea nchi hiyo utauona na kuupanda mlima Kilimanjaro kirahisi.

Katika moja ya treni inayofanya safari zake za kila siku kwenye jiji la Geneva ilikuwa na mabango ya kulitangaza Shirika la Ndege la Kenya, pamoja na vivutio vya utalii vilivyopo nchini humo, ukiwamo muonekano wa mlima Kilimanjaro na theluji yake.

Aidha, wameweka mabango ya hoteli na maeneo ya mapumziko kwa watalii, yakisema kwamba wataona wanyama na baada ya hapo watakuwa na eneo zuri la porini kwa ajili ya mapumziko yao.

Haya yote yanafanyika wakati Geneva imepokea wageni zaidi ya 500 kutoka mataifa mbalimbali duniani, wanaohudhuria mkutano wa wadau wa Umoja wa Mataifa wa kupunguza athari za maafa (United Nation Disaster Risk Reduction- UNDRR).

Treni yenye matangazo hayo hufanya safari zake kati ya eneo liitwalo Nations ambako kuna ofisi zote za Umoja wa Mataifa, kuelekea katikati ya jiji la Geneva.

Hii ni mbinu ya kutangaza vivutio na kuteka soko la Ulaya, kwani ni rahisi kwa mtalii kuelewa atakachokipata akiitembelea Kenya.

Kwamba ataona vivutio vyote vinavyotangazwa kwa maana ya uhamaji wa makundi makubwa ya wanyama na mlima Kilimanjaro, hivyo kutumia muda mwingi na fedha zaidi nchini humo.

Mjadala unaona kuwa kazi nzuri imefanywa na Bodi ya Utalii Tanzania, lakini bado jitihada zaidi zinahitajika kujitangaza.

Hiyo ni pamoja na kupata nafasi kwenye majarida makubwa ya mashirika ya ndege kama Turkish, lenye zaidi ya ndege 500 zinazokwenda maeneo yote ya dunia.