Bongo na siasa zake ni balaa!

11Oct 2020
Joseph Kulangwa
Nipashe
FIKRA MBADALA
Bongo na siasa zake ni balaa!

UKIFANIKIWA kuishi Tanzania miaka mingi, usipofanikiwa kuwa kichaa, basi utakuwa msanii tu kwa vyovyote. Na kuwa msanii si lazima ukaigize majukwaani au luningani, redioni au hata kwenye kumbi za starehe.

Unaweza kujikuta msanii ukiwa na familia yako nyumbani kwako. Watoto ndio wataweza kubaini kuwa huyu baba au huyu mama, tayari zimemruka au ameshaingia katika kundi la maigizo au futuhi au komedi.

Utakuwa unajisemeasemea mwenyewe au hata kupiga teke makopo na mawe yanayokuwa mbele yako, wewe ukidhani ni burudani yako, lakini kumbe unawakwaza wenzio. Ukishamaliza hiyo unaingia ngazi nyingine sasa, unakuwa mwanasiasa.

Ukishakuwa mwanasiasa, utaanza kusema ya uongo na ya kweli. Kuna wakati utazidisha ya uongo na ukibaini umegundulika, ndipo utaanza kusema ya ukweli ingawa kwa kiwango kidogo sana.

Utasikia mtaani watu wanaanza kulalamika kuwa kumbe siasa si hasa, na ukitaka kuwa mwanasiasa lazima ujiandae kusema uongo, ndipo utakubalika na wengi. Ukitaka kuwa mwanasiasa, lazima ujiandae pia kuwa mwigizaji, uwe msanii.

Mwaka huu tulishuhudia wasanii wengi wakiingia kwenye kinyang’anyiro, baadhi wajumbe wakawapiga spana na wengine lakini wachache sana wakapenya, na sasa wanahangaika majukwaani kukampeni, huku wakichanganya na usanii.

Hawa ni wale wanaovutia wapiga kura kwa kuwaimbia nyimbo, kwa sababu wana kipaji cha kuimba, wasio na kipaji ndio wale wanaoongopa sana, mpaka washangiliwe na kupigiwa makofi. Wakiona hawaridhiki utawasikia wakihoji: “Wangapi mtanipigia kura, mikono juu?”

Hebu tazama picha hili; ni mfano tu msijenitoa macho, wanaomwunga mkono mgombea wa chama tawala, wanafanya hivyo wakitaja maendeleo aliyowaletea katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano.

Wanamwunga mkono wakitaka apewe mingine kama hiyo, kwa sababu ya miradi aliyojenga. Wanataja kama anavyoitaja yeye. Amejenga reli ya kisasa, barabara za juu Dar es Salaam, bwawa la mitambo ya kuzalisha umeme, barabara kila mahali, umeme karibu kila kijiji, ndege za kumwaga.

 

Si uongo, hayo ameyafanya na kila mwenye macho haambiwi tazama. Lakini miradi hiyo hiyo inatumiwa na wengine wa upinzani kumpinga, tena wanaitaja hivyo hivyo, wanakiri ipo, lakini wanaitumia kumpinga!

Wakati yeye na kambi yake wanasema tumeweza kujenga miradi hiyo kwa fedha zetu wenyewe, wanaompinga wanasema kodi hiyo imetumiwa vibaya ni afadhali ingekwenda kwenye mishahara, ili mifuko ya watu ijae watu wale ubwabwa.

Akiwaambia tumejenga na kupanua viwanja vya ndege, wao wanaibuka na kusema ndiyo, mbona vingine havina faida na kwa nini umevijengea huko na si huku? Utadhani viwanja hivyo hazitui ndege, zinatua na haohao wanazipanda. Ndiyo, lazima wazipande kwa sababu wanasema ni kodi yao na hawana mbawa waruke wenyewe.

Sasa kama ni kodi yao ubaya uko wapi kuzinunua? Hawakosi majibu lakini, watayachakura kwenye mafaili na kuibuka wakisema mbona wakati unazinunua hukutwambia. Na wengine utawasikia wakisema hivyo na baada ya muda wanafanya bukingi ya kwenda Mwanza.

Hapo ndipo unaweza kuwajua Watanzania, na kwa kweli wanafurahisha na ukiwafuatilia saana ndipo nawe maisha yako yanazidi kurefuka, kwa sababu utakuwa unacheka tu na kupata furaha pekee unayoweza kuipata.

Hizo ndizo siasa zetu Wabongo, lakini jua kwamba kipindi hiki kikipita salama, basi tunasahau na kuwa wamoja. Tunasahau kabisa kauli tulizotoa kwenye kampeni za kuondoana kwenye reli hivihivi!

Tanzania au Bongo, kwa kweli raha sana, huyu akitaka alete maendeleo huyu anatia mguu anahoji kwa nini. Huyu akisema jamani maendeleo hayana chama, lakini nichagulieni mafiga matatu, huyu anatoa macho akisema haelewi.

Anataka kujua mafiga matatu kivipi wakati figa moja linaweza kuwa bovu, au hata mawili na moja ndilo likawa na uwezo wa kubeba sufuria la maji! Lakini ndio mchuano huo, akili mukichwa kwa wanaopiga kura, vinginevyo nao watalokota makopo kumitaa. Wengine hubebwa na kauli ya mafiga tu hawana uwezo. Alamsiki!