Bravo Rais Samia uhuru wa habari

07Apr 2021
Mhariri
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Bravo Rais Samia uhuru wa habari

JANA Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa tumaini jipya kwa sekta ya habari kwa kutaka uhuru wa vyombo vya habari kuwapo nchini, kwa kufungulia vyombo vilivyopo kifungoni kwa muda mrefu na kusisitiza usimamizi wa sheria na kanuni za taaluma hiyo.

Tunampongeza Rais Samia kwa kauli yake yenye matumani makubwa kwa sekta ya habari na wanahabari wenyewe, kwa kutambua kuwa taifa lisiloongea ni taifa mfu, maana yake unapozuia watu kuongea, unatengeneza taifa la hofu na huwezi kujua yanayoendelea upande wa pili.
 
Hili ni tumaini jipya kutokana na uhalisia kwenye vyombo vya habari kuwa kwa sasa badala ya kuajiri Watanzania, kulipa kwa wakati na kuchangia uchumi wa nchi, pamoja na kuisaidia serikali kama jicho muhimu, ilijikuta katika kufubaa kiasi cha kuelekea kushindwa kujiendesha.
 
Hadi sasa kuna magazeti, vituo vya TV na redio nyingi ambavyo vipo kifungoni kwa makosa mbalimbali, na baadhi viko kwenye kifungo cha maisha, huku waliokuwa wameajiriwa wakiwa nyumbani, kushindwa kusaidia wategemezi wao na kulipa kodi mbalimbali za nchi.
 
Kauli ya Rais Samia imekuja kwa wakati sahihi, ambao Mei 3, kila mwaka vyombo vya habari vitaadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari dunia, ambao msukumo mkubwa ni kuhakikisha siyo tunakuwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari, lakini vinavyotimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo na taratibu zilizopo.
 
Vyombo vya habari ni muhimili wa nne wa nchi, yaani baada ya serikali, Bunge na Mahakama, na wajibu wake mkubwa ni kuelimisha, kuburudisha, kukosoa na kutengeneza ajenda ambayo ikitekelezwa vizuri utasaidia sana serikali, kwa kuwa ni jicho lake katika mambo ambayo haiwezi kuyaona.
 
Upo ushahidi wa namna vyombo vya habari vimesaidia kuibua madudu mengi ya kuisadia serikali kuchukua hatua, hivyo kuvibana vyombo vya habari kiasi cha kushindwa kujiendesha, kuajiri na mengine mengi ni kuwaumiza Watanzania na hata kuikosesha serikali mapato.
 
Leo hii vyombo vya habari vina idadi kubwa ya wahariri na waandishi, ambao walikuwa ndani ya vyombo vya habari, lakini wako nje ya ulingo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, na sasa kwa kupewa uhuru maana yake vitaweza kuibua habari mbalimbali za kuisaidia serikali pamoja na kuwasemea wanyonge kuhusiana na kero wanazokumbana nazo.
 
Iwapo kutakuwa na vyombo vya habari imara, vitalisaidia taifa kusonga mbele, na vitakuwa mjenzi mzuri wa taifa kwa kuwa tunaamini jicho lake ni kali, ambalo litakwenda kuona yaliyo nyuma ya pazia, ambayo yataisaidia kutafutiwa ufumbuzi.
 
Ni muhimu sana viongozi wakakubali kukosolewa kwa kuwa siyo wakati wote wa kusifiwa na unapokosolewa basi unasaidiwa kurekebisha pale ambako mambo hayako sawa.
 
Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania ambayo ndiyo sheria mama inasema kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake, anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi, anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake na anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.
 
Wajibu huo ndiyo unavipa nguvu vyombo vya habari kutimiza wajibu wake, lakini wakati mwingine vimejikuta katika wakati mgumu kiasi cha vingine kufungiwa na sasa mamia ya watu wako nyumbani kwa kuwa hawana ajira.
 
Vyombo vingi vya habari ni vya sekta binafsi na vina mchango mkubwa kwa taifa, lakini vinaposhindwa kujiendesha maana yake hata kodi kidogo vilivyokuwa vinalipa haitakuwapo, na idadi ya wasio na ajira itaongezeka.
 
Tunampongeza rais kwa kuona umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na kutamka kuwa viachwe, inaonyesha ni muumini wa uhuru wa kujieleza, nasi vyombo vya habari tunamwahidi ushirikiano thabiti katika kuliongoza taifa.
 
Pamoja na uhuru huo tunamwomba Rais Samia kutupia jicho eneo la matangazo ili kuhakikisha sekta binafsi nayo inapata matangazo kiushindani kama vilivyo vyombo vingine vya habari, na kwa kuwa wote wanachangia katika uchumi wa nchi, jambo  ambalo litapunguza kama siyo kumaliza ukali wa maisha.